Novatus Miroshi anapita mule mule kwa Samatta

NI ndoto ya vijana wengi wa Kitanzania kufika levo ya Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ya kucheza Ligi kubwa barani Ulaya kutokana na rekodi aliyoweka.

Akiwa Mtanzania wa kwanza kuweka rekodi mbalimbali anatajwa kuwa ndiye mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini akiwa amezitumikia klabu mbalimbali kama TP Mazembe, Aston Villa na Genk kwa mafaniko makubwa.

Sasa ukiachana na mafanikio makubwa ya Samatta ndani na nje ya uwanja lakini mwenendo wa kiraka, Novatus Miroshi wa Goztepe ya Uturuki huenda akafikia rekodi ya nahodha wa Stars.

Hata hivyo Kelvin John anayekipiga Aalborg BK ya Denmark ambaye pia aliwahi kucheza KRC Genk na Miroshi walionekana kuwa nafasi kubwa ya kuvunja rekodi ya Samatta.

Lakini Novatus aliifikia rekodi ya Samatta ya kucheza Ligi ya Mabingwa akifanya hivyo na Shakhtar Donesk akiwa mchezaji wa pili kufanya hivyo.

Ukiangalia mwenendo wa kiraka huyo wa Taifa Stars ni kama anapita mule mule kwa Samatta ingawa hajafikia pakubwa lakini kama atakuwa na muendelezo mzuri anaweza kuvunja rekodi hiyo.

Mwanaspoti imekuchambulia baadhi ya rekodi alizoziweka Miroshi akimfukuzia Samatta licha ya kwamba nyota hao wanacheza nafasi mbili tofauti.

TIMU ALIZOPITA

Samatta alianza maisha yake ya soka la kulipwa akiwa na Simba kuanzia mwaka 2010/11 alipocheza kwa mafanikio alipofunga mabao 13 kwenye mechi 25 baada ya hapo TP Mazembe ya DRC Congo ikamsajili kwa mkataba wa miaka mitano kuanzia 2011/16.

Ndani ya misimu hiyo Samatta alifanikiwa kucheza mechi 103 za mashindano yote akafunga mabao 60 ikiwa miongoni mwa msimu aliofunga mabao mengi.

Akiwa na timu hiyo alifanikiwa kubeba ndoo ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2015 akicheza fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria ambapo Mazembe waliitandika mabao 4-1, huku Samatta akifunga nyumbani na ugenini.

Aliandika pia rekodi ya kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wale wanaocheza ndani ya bara hili Januari7, 2016 ikiwa mwaka mmoja tangu abebe ndoo ya Afrika.

Siku 28 baada ya kukabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, Nyota huyo alijiunga na KRC Genk akasaini mkataba wa miaka minne na nusu na kuandika rekodi nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ubelgiji na msimu wa kwanza tu akaifungia timu hiyo mabao 21 kwenye mechi 59 za mashindano yote.

Msimu 2017/18 hakuwa na msimu bora akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara na akamaliza na mabao nane kwenye mechi 35, lakini hakuishia hapo msimu uliofuata akapambana na kumaliza mfungaji bora wa Ligi ya Ubelgiji alipomaliza na mabao 20 akaandika rekodi nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuchukua kiatu cha dhahabu msimu ambao pia Genk ilitwaa ubingwa wa Ligi.

Tunaweza kuandika mengi hata kwa siku ngapi lakini tusimalize rekodi za nyota huyo ambae msimu 2019/20 kucheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa akifunga bao moja katika mchezo wa hatua ya makundi kwenye Uwanja wa Anfield, Genk ilipopoteza mabao 2-1 dhidi ya Liverpool.

Januari 2020, Samatta alitangazwa kuwa mchezaji wa Aston Villa akitokea Genk na Februari mwaka huo huo akafunga bao katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth, hakukawia na msimu huo akacheza fainali ya Carabao Cup dhidi ya Manchester City na kufunga bao lililomuwezesha kuweka rekodi nyingine.

Villa mabo hayakuenda sawa na msimu huo huo akaenda Fenerbance ya Uturuki kwa mkopo ambao mwishoni mwa msimu 2020/21 alisaini mkataba wa kudumu wa miaka minne na nusu, lakini maisha yake hayakuwa mazuri aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara na mwisho wa msimu, akatolewa kwa mkopo kwenda Royal Antwerp, kisha Genk na baadae akauzwa PAOK ya Ugiriki ambapo yupo hadi sasa.

Muache Samatta ambaye ana rekodi za pekee Ulaya kuna mlinzi wa pembeni, Miroshi ambaye pia anafukuzia rekodi za nahodha wa Stars.

Novatus alianza kutambulishwa kwenye soka la kulipwa akiwa na Azam FC ambapo baadae wakamtoa kwa mkopo kwenda Biashara United ya Mara.

Mara baada ya kuwa na msimu bora akiwa na Biashara msimu 2019/20 akisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tisa na kuchukua tuzo ya mchezaji bora chipukizi, waajiri wake wa zamani Azam FC walimrejesha kwenye mipango yao kwa ajili ya msimu uliofuata.

Baadae akapata mualiko wa kwenda kujifunza nchini Israel kwenye klabu ya Maccabi Tel Aviv 2021/22 na kupata nafasi ya kufanya mazoezi na timu ya vijana wakavutiwa naye na Azam wakamuachia kwenda kutafuta maisha nchini humo.

Ndani ya mwaka mmoja, Miroshi alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo lakini hakucheza hata mchezo mmoja kutokana na changamoto ya namba akapelekwa kwan mkopo Beitar Tel Aviv ambayo ilionyesha nia ya kumtaka.

Msimu mmoja tu aliocheza Israel ulimpa shavu la kwenda Ubelgiji ambako alijiunga na Zulte Waregem 2022/23 akitumika kama beki wa kati na baadae akarudishwa kwenye nafasi yake ya beki wa kushoto.

Bahati mbaya Zulte ikashuka daraja lakini kiwango alichoonyesha Miroshi kilimfanya aanze kuhushishwa na timu za Ligi daraja la kwanza nchini England ndipo ikaibuka ofa ya kujiunga kwa mkopo Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Hapo sasa akafanikiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya UEFA Champions League dhidi ya FC Porto, chama lake likitandikwa mabao 3-1.

Mechi hiyo alianza na kumaliza dakika zote 90 na kumfanya aingie kwenye kitabu cha historia ya kuwa mtanzania wa pili kucheza michuano hiyo ya Ulaya.

Ukiangalia namna alivyopambana toka bongo hadi kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na sasa Goztepe ya Uturuki miongoni mwa nchi aliyocheza Samatta akiwa na Fenerbance.

Ukiachana na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo alichukua akiwa na Mazembe lakini ndio mchezaji wa kwanza Tanzania kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na timu mbili tofauti Ulaya.

Samatta pia ameweka rekodi ya kuwa staa pekee kufunga kwenye ligi nne barani Ulaya baada ya kuifungia PAOK mabao manne.

Kwa Novatus iko tofauti kidogo ingawa ana rekodi yake ya ubingwa akiwa ugenini kwa maana alipopita Biashara United na Azam FC hajabeba ndoo ya Ligi zaidi ya tuzo ya mchezaji chipukizi.

Ubingwa wake wa kwanza alikuwa na Shakhtar ikiwa ndio taji lake la kwanza na kucheza michuano hiyo mikubwa Ulaya na kumfanya awe Mtanzania wa kwanza kubeba taji hilo la Ukraine.

TAIFA STARS

Ubora na uzoefu wa Samatta kwenye kikos cha timu ya taifa kumefanya mashabiki wa Tanzania kuendelea kujivunia pengine hata akiachwa kwenye kikosi hicho kuuliza imekuwaje? nahodha huyo hayupo.

Sasa achana na Samatta kuna Miroshi wa Taifa Stars jamaa anajua kumwaga jasho, popote muweke muhimu aitumike bendera ya Tanzania.

Ni beki wa kushoto lakini kutokana na ubora alionao muda mwingine amekuwa akichezeshwa eneo la kiungo wa chini akitendea haki.

Kwa sasa ndio kiungo tegemeo Taifa Stars ambaye amekuwa na muendelezo mzuri kama ilivyo kwa Samatta ambaye amekuwa mhimili kwenye eneo la ushambuliaji.