Novatus amtikisa Mourinho Uturuki

Istanbul, Uturuki. Mtanzania anayekipiga Ligi Kuu nchini Uturuki, Novatus Miroshi ameendelea kuonyesha makali yake baada ya kufunga bao katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo akiifunga Fenerbahçe inayonorewa na kocha, José Mourinho.

Hata hivyo, bao alilofunga kiungo huyu alikutosha kuipa timu yake ushindi kwani walikuwa nyuma kwa bao moja, mpaka dakika 90 zinamalizika Göztepe ilikubali kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Fenerbahçe.

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ulker Sukru Saracoglu jijini Istanbul, Miroshi, mchezaji pekee Mtanzania anayekipiga Ligi Kuu Uturuki maarufu kama Super Lig, ameendeleza makali yake akicheza kwa kiwango cha juu tangu aliporejea kutoka katika majeraha.

Septemba mwaka jana kiraka huyo anayemudu pia kucheza nafasi ya kiungo alipata majeraha ya nyama za paja yaliyomuweka nje kwa wiki sita.

Mchezo wake wa kwanza baada ya kutoka kwenye majeraha ilikuwa Novemba 1, mwaka jana wakati Goztepe ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Gaziantep akicheza kwa dakika sita tu, lakini baada ya hapo amekuwa akianza na kumaliza dakika zote 90, kali zaidi akicheza nafasi ya beki wa pembeni na kufunga mabao.

Katika mchezo wa jana, alifunga bao la pili kwa Goztepe katika dakika ya 82 baada ya awali Juan Santos kuitanguliza kwa bao la dakika ya 25, wote wakimalizia pasi za Rômulo Cardoso, huku wenyeji wakipata mabao yao kupitia kwa Youssef En Nesyri aliyetupia mawili na Oguz Aydin.

Wakati Ligi Kuu ikiwa mzunguko wa 20, Novatus mpaka sasa amehusika katika mabao manne akifunga matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Goztepe inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 34 ikishinda mechi 10, sare mechi nne na ikipoteza mechi sita.

Miroshi alitambulishwa na klabu hiyo Julai 23 mwaka huu akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambako alicheza michuano ya UEFA Champions League.