Noti zaongezwa Pamba Jiji iifunge Azam

Homa ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Pamba Jiji FC na Azam FC kesho, Jumapili, Februari 9, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, imezidi kupanda baada ya wachezaji wa Pamba kuahidiwa bonasi ya Shilingi 15 milioni ikiwa watapata ushindi kwenye mchezo huo.

Awali bonasi ya ushindi kwa wachezaji wa Pamba Jiji ilikuwa ni Sh10 milioni kwa mechi lakini dhidi ya Azam FC, watapata Sh15 milioni huku wafungaji wa mabao nao kila mmoja atapata Sh 250,000.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Pamba Jiji FC, Said Mtanda alisema kuwa anaamini ongezeko la bonasi hiyo, litawapa chachu wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri dhidi ya Azam FC.

“Tunataka boli itembee. Tunataka pointi tatu na tunazitaka kwelikweli. Kamati ya hamasa ambayo iko chini ya mkuu wa mkoa inaahidi bonasi ya milioni 15 kama vijana mtapata ushindi katika Uwanja wa Kirumba.

“Lakini pia mkitoa pointi moja tutatoa milioni saba. Na hii ni kazi endelevu kwa mechi zote zilizobaki mpaka ligi inakwisha. Lakini bonasi ndogondogo, goli la mkuu wa mkoa limeongezewa uzito leo. Mkuu wa wilaya ataweka hela, rafiki yangu hapa shabiki wa Pamba ataweka hela.

“Kwa hivyo tunaweza tukajikuta tunaondoka na fedha nyingi. Tunafanya kazi ili kupata fedha na nyinyi mko kazini tafuteni pesa. Na sisi tuna pesa tunatafuta watu wa kuzitumia. Kwa hiyo tunawahamasisha mzitoe fedha mifukoni mwetu kwa vile tunazo,” alisema Mtanda.

Mtanda alisema kuwa wana imani Pamba Jiji itaibuka na ushindi katika mchezo huo huku akitangaza kushushwa kwa bei ya kiingilio kwa jukwaa la mzunguko kutoka shilingi 2000 hadi 1000.

“Kwa hiyo mimi ninaamini kesho mtashinda na Inshallah kwa uwezo wa mwenyezi Mungu. Lakini mwisho tumesema wananchi wengi wapate fursa, kiingilio cha mzunguko kiwe 1.000 badala ya shilingi 2,000 ili kuwafanya kila mtu aweze kuja kwenye mechi ya kesho.

“Kwa hiyo wametangaza 2,000 lakini mimi na mwenyekiti wa timu na kamati tumeshauriana kwamba kiingilio kiwe 1,000 ili wananchi waweze kuja na kuangalia utamu wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Mtanda.

Timu hizo zinakutana zikiwa na morali baada ya kila moja kupata ushindi katika mechi yake iliyopita ambapo Pamba ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, huku Azam FC ikiifunga KMC kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wake wa nyumbani.

Ushindi kwa Pamba utaifanya ifikishe pointi 18 ambazo zinaweza kuisogeza hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 14 iliyopo sasa lakini hilo litatokea ikiwa Namungo FC itapoteza nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Azam FC iliyo na pointi 39, ikipata ushindi leo itabaki katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi lakini itapunguza pengo la pointi kati yake na Yanga inayoongoza kubakia pointi tatu na itabakiza pointi mbili kuifikia Simba iliyo katika nafasi ya pili.

Timu hizo zimewahi kukutana mara moja tu kwenye ligi ambapo ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana