‘No reforms, no election’ pasua kichwa, Lissu akiri haijaeleweka

Dar es Salaam. Kampeni cha Chadema ya Chadema ya ‘No reform, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi) imeendelea kupasua vichwa makada wa chama hicho viongozi mbalimbali, huku Mwenyekiti Tundu Lissu akisema ni sawa na usiku wa giza kwa kuwa haijaeleweka.

Lissu amesema changamoto ya kutoeleweka kwa kampeni hiyo inawatatiza hata makada wa chama hicho kuwaelewesha wengine katika maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba Chadema haitasusia uchaguzi, bali itashinikiza mabadiliko ya mifumo ili mchakato huo uwe wa haki kwa vyama vyote.

“Hawajaielewa vizuri, kama hawajaielewa sawasawa, itakuwa ni vigumu kuelimisha wengine inavyotakiwa.

“Nataka hiki tukielewe sote kwa pamoja ili ukiulizwa mahali uweze kujibu, kwa sababu jambo usilolielewa ni sawa na usiku wa giza, siyo?  Na jambo ukilielewa nusunusu inakuwa kama giza giza… tukielewa sawasawa tutawaelimisha wengine,” alisema Lissu Februari 21, 2025 wakati wa maadhimisho ya jimbo la Kibamba (Kibamba Day), jijini Dar es Salaam, alikoalikwa akiwa mgeni rasmi.

Shaka aliyoonyesha Lissu ni mwendelezo wa namna kaulimbiu hiyo inavyowachanganya viongozi, wanachama na mashabiki wengine wa Chadema na hata nje ya chama hicho.

Tayari wamekuwapo kauli au tafsiri zinazotofautiana za wanasiasa kuhusu kaulimbiu hiyo inayozidi kushika kasi kwenye mijadala.

Tayari chama tawala CCM kimetoa kauli kuhusu kaumbiniu hiyo ambapo Amos Makalla, katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, amesema: “Kwa sheria zilizopo, mabadiliko yamefanyika, kinachozingatiwa hapa ni taratibu na sheria. Kwa hiyo mtu anayezuia uchaguzi ni mhalifu.”

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla (katikati) akifanya mahojiano maalumu na wahariri wa Gazeti la Mwananchi, alipotembelea Mwananchi Communications Ltd (MCL), leo. Picha na Sunday George

Februari 20, 2025, Mwananchi lilichapisha habari ikieleza baadhi ya makada wakiwamo wajumbe wa kamati kuu ya Chadema wakiwa njiapanda kama ama wajiandae na uchaguzi au la, huku wengine wakiingiwa hofu ya kukosa fursa ya kushiriki uchaguzi.

Makada hao walibainisha wazi kuwa hawajui iwapo wajiandae kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu au waendelee kusikilizia kauli ya chama inayosisitizwa na Lissu.

Lissu na baadhi ya viongozi wengine wa Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba “kwa sasa nguvu kubwa zielekezwe kupigania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi na si vinginevyo.”

Kabla ya Chadema kuibuika na kampeni hiyo iliyoanzia kamati kuu na kubarikiwa na Baraza Kuu kisha mkutano Mkuu, Katibu Mkuu John Mnyika alinukuliwa na gazeti hili akisema wakati wanadai marekebisho ya Katiba, vilevile wanajiandaa na uchaguzi na ndiyo maana wamefanya “Operesheni +255 Katiba mpya.”

Mnyika alisisitiza kuwa wataendelea na maandalizi ya uchaguzi na wakati mwafaka, kamati kuu itatathmini kama maboresho yaliyofanyika yanakidhi haja, kisha watatoa mwelekeo kwa Taifa.

“Mwenye nia ya kugombea udiwani, ubunge na urais, ajitokeze kwenye chama kwa mujibu wa mwongozo wa chama wa wagombea. Kwa hiyo, ninachosisitiza hapa ni kwamba kudai kwetu Katiba mpya hakutufanyi tubweteke kusubiri Katiba mpya,” alisema Mnyika.

Miongoni mwa walioitikia wito huo ni Lissu mwenyewe, wakati huo akiwa makamu mwenyekiti alipoandika barua kwa katibu mkuu kueleza nia yake ya kuwania urais Oktoba mwaka huu.

Makada wagawanyika

Wakati suala hilo likishika kasi, kiongozi kutoka Kanda ya Kati ya Chadema alisema: “Kwenye suala la ‘no reforms, no elections’ si wote wanaounga mkono, bali wengi wanataka chama kishiriki uchaguzi kwa sababu walishawekeza kwenye maandalizi ya uchaguzi wa udiwani na ubunge, hivyo msimamo huu unatuweka wengi wetu njiapanda.”

ADC yaizungumzia kinamna

Wakati Chadema kikishinikiza kutofanyika kwa uchaguzi endapo mabadiliko hayatafanyika, wenzao wa ADC wamepanga kushinikiza mabadiliko hayo kwa kushiriki uchaguzi mkuu ujao “ili kuwashawishi wananchi wakipigie kura kifanye mabadiliko hayo.”

Akizungumzia msimamo wa chama chake wakati akizindua tawi jijini Mwanza, Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaaban Itutu amesemema wanakuja na kaulimbiu ya “Kama Mbwai na Iwe Mbwai” kwenye uchaguzi ujao kupigania mabadiliko.

Itutu amesema anaamini kwa kuwa CCM imeshindwa kufanya ‘reforms’ (marekebisho ya mifumo), namna pekee ya kuifanya ni kuushawishi umma kuipigia ADC kura kwa wingi, kisha itafanya marekebisho hayo ikiwa madakani.

“Tunataka wananchi mkaamue kwa kukipigia chama cha ADC kura ili tuwaondoe CCM madarakani kwa sababu usipoingia kwenye uchaguzi hata haki ya kuingia madarakani hawezi kuipata. Kwa hiyo haki ya kwanza ni kuingia kwenye uchaguzi ili tuwashughulikie CCM,” amesema Itutu.

Ni kinyume cha sheria

Katika hali inayoonyesha kaulimbiu hiyo haijaeleweka hata nje ya Chadema, wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, Februari 21, Makalla alisema msimamo wao kuhusu ‘No reform, no election’ ni kuwa chama kimoja hakitaweza kuzuia uchaguzi kufanyika ma kuwa marekebisho ya sheria yalikwishafanyika.

Mwaka 2024 Bunge lilipitisha mabadiliko ya sheria tatu za uchaguzi ambazo ni Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Licha ya mabadiliko hayo kurekebisha baadhi ya mambo, kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), bado Chadema inaungana na wadau wengine kuonyesha wasiwasi kama yatawezesha kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Chama hicho kimekuwa kikitumia uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024 kama mfano kuonyesha namna wagombea wa vyama vya upinzani walivyoenguliwa na kukiwezesha CCM kushinda katika maeneo mengi bila ushindani.

Ufafanuzi wa Lissu

Hii si mara ya kwanza kwa Lissu kufafanua maana ya kaulimbiu hiyo, amefanya hivyo kwa nyakati tofauti kila anapopata fursa ya kuzungumza na wananchi na wanachama wa Chadema.

Katika ufafanuzi wake, Lissu anasema kaulimbiu ya hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi ina maana kwamba, kwa utaratibu uliopo hivi sasa wa kikatiba, kikanuni, kiserikali na kisheria, uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki.

“Uchaguzi huru na wa haki hauwezekani tena kwa utaratibu uliopo ambao wagombea wa upinzani wanaenguliwa pasipo sababu za msingi, ndiyo maana tunasema bila mabadiliko, hakuna uchaguzi,” amesema Lissu.

Anatoa mfano wa chaguzi za serikali za mitaa zilizofanyika kati ya mwaka 2024 na 2019 ambazo ziliacha vilio kwa upinzani tofauti na mwaka 2014 ambapo vyama hivyo, ikiwemo Chadema, vilipata viti vingi kwenye vitongoji, vijiji na mitaa.

Lissu amesema kuna watu wema na wasio wema watawauliza viongozi wa Chadema kuhusu kaulimbiu hiyo, hivyo amewataka wajibu kama aliyowaelekeza wakati akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

“Kwa mazingira ya sasa uchaguzi huru hauwezekani tena, kama hauwezekani Mungu hajasema tulale tuombe, bali tuipiganie nchi ni yetu sote. Tunaipigania kwa kuhakikisha tuna mfumo bora zaidi,” amesema.

Kuhusu Kibamba Day

Kibamba Day, shughuli inayofanyika kwa mara ya pili, imewakutanisha makada na viongozi kutoka kata mbalimbali za jimbo la Kibamba kwa lengo la kubadilisha mawazo, kujadiliana na kutengeneza uhusiano miongoni mwa wana Chadema.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba, Ernest Mgawe amesema wanachama wa Chadema Kibamba wamekuwa na utaratibu wa kuwa na Kibamba Day kwa kufanya shughuli zinazoambatana na matukio mbalimbali ya ujenzi wa chama.

“Leo ni mwendelezo wa kuwa na Kibamba Day ambayo mwisho wa siku tunakutana pamoja. Kibamba tumekuwa na umoja na upendo unaotokana na shughuli hii.

“Katika chaguzi kunakuwa na makundi, kundi linaloshindwa linakuwa na maumivu na linakuwa na maneno ya hapa na pale. Nikuhakikishie mwenyekiti, hadi tunaingia kwenye ukumbi hakuna makundi yoyote kwa sababu tunataka tufanye kazi za chama,” amesema.

Mgawe alisema: “Uchaguzi umekwisha, lazima tufanye kazi, jimbo la Kibamba lipo bega kwa bega kusimamia kaulimbiu ya ‘No reform, no election.”