No reform No Election kurindima Kanda ya Kusini kuanzia Aprili 4, 2025

Dar es Salaam. Kadri joto la uchaguzi wa mwaka 2025 linavyozidi kupanda, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na kampeni yake ya No Reform No Election, inayolenga kutoa elimu kwa umma ili kushinikiza kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huo. Na sasa, kampeni hiyo inahamia Kanda ya Kusini.

Mpango huo uliopitishwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema Januari 21, 2025, ulianza rasmi kutekelezwa Machi 23, 2025, katika Kanda ya Nyasa.

Viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu na Makamu wake, John Heche waliongoza kampeni hiyo kwa siku saba mfululizo kabla ya mapumziko kwa ajili ya sikukuu ya Idd.

Baada ya kuzinduliwa mkoani Mbeya kwa mikutano ya hadhara kwenye maeneo mbalimbali, viongozi hao waligawana majukumu, Lissu na timu yake waliendelea na kampeni katika mikoa ya Mbeya na Rukwa, huku Heche na timu yake wakielekea Njombe na Iringa.

Akizungumza leo Jumatano, Aprili 2, 2025, katika makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Aden Mayala amesema baada ya mafanikio ya kampeni hiyo Kanda ya Nyasa, sasa wanahamia rasmi Kusini.

“Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, itaanza mikutano yake rasmi kuanzia Aprili 4, 2025.

Awali, ratiba ilikuwa kuanza Kusini, lakini iliahirishwa ili kutoa fursa kwa waumini wa Kiislamu waliokuwa katika mfungo wa Ramadhani kusherehekea sikukuu ya Idd” amesema Mayala.

Amesema kampeni hiyo itaanzia mkoani Lindi, kisha itaendelea Mtwara na hatimaye Ruvuma, ambako wataanzia Wilaya ya Nyasa, Mbinga Mjini na kumalizia Songea Mjini.

“Tunawaalika wananchi wote, wapenzi na wanachama wa Chadema katika Kanda ya Kusini kujiandaa kuupokea ugeni huu mkubwa. Kupitia kampeni ya No Reform No Election, tutaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.

Hatutaki uchaguzi wa ovyo kama ule wa 2019, 2020, na 2024, ambao haukuwa wa haki na haukuzingatia misingi ya demokrasia,” amesema Mayala.

Amesisitiza kuwa Chadema haitasusia uchaguzi, bali inashinikiza kufanyika kwa mabadiliko yanayohakikisha ushindani wa haki kabla ya uchaguzi huo.

“Tunawaomba Watanzania wote wenye mapenzi mema na mabadiliko, iwe ni wanachama wa Chadema au la, waunge mkono jitihada hizi kupitia kampeni ya Tone Tone inayokusudia kukusanya fedha za kufanikisha mikutano hii,” amesema.

Mayala aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Songea Mjini, amesisitiza kuwa mabadiliko ya kweli yanahitaji mshikamano wa jamii nzima.

“Tunataka uchaguzi ambapo kura ya mwananchi itaheshimiwa kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea. Chadema si wahaini kwa kudai haki za msingi, na tumeazimia kuhakikisha mabadiliko haya yanatimia,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa wananchi wa Kusini wanapaswa kuwa tayari kwa mikutano hiyo ambayo itafanyika Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Ulinzi wa Mikutano

Kuhusu usalama wa mikutano hiyo, Mayala amesema chama tayari kimetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi katika vituo mbalimbali vya Wilaya (OCD) kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Tanzania.

“Tunaendelea kuhakikisha kuwa taratibu zote za kisheria zinazingatiwa. Tayari tumewasilisha taarifa kwa maafisa wa polisi wa wilaya husika, na wanajua kuwa mikutano inaanza rasmi Aprili 4, 2025,” amesema Mayala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *