Dar es Salaam. Benki ya NMB imeendelea kutanua sifa na kutangaza huduma zake kimataifa kwa kupata ushindi wa kihistoria kwa kushinda tuzo sita za kimataifa kutoka kwa majarida mawili mashuhuri duniani; Euromoney, linalochapishwa jijini London, Uingereza, na Global Banking & Finance Magazine lenye makao makuu yake New Jersey, Marekani.
Ushindi huo unaashiria kutambuliwa kwa ubora wa huduma, ubunifu na mchango wa NMB katika kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.
Miongoni mwa tuzo hizo ni pamoja na ile ya heshima ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika” inayodhibitisha mafanikio na maendeleo ya benki hiyo kwenye tasnia ya fedha nchini.
Tuzo ya Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika imetolewa jijini London katika hafla ya Euromoney Private Banking Awards 2025, na imeweka historia kwa kuwa ya kwanza kutolewa kwa benki ya Kitanzania.
Akizungumzia tuzo hizo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema ushindi huo ni hatua kubwa kwa benki yake na kwamba zitakwenda kuongeza chachu ya kuendelea kutoa huduma bora za kifedha nchini.
“Ni hatua ya kihistoria kwa tasnia ya fedha nchini. Tuzo hizi ni hatua muhimu katika kuisaidia Tanzania kujipambanua kama kiongozi wa kikanda wa ufadhili endelevu na utoaji wa huduma bora za kifedha,” amesema Zaipuna.
Amesema kuwa ushindi huo unadhihirisha jitihada za NMB za kuongoza mabadiliko na dhamira ya dhati ya kuyafanya masuala ya mazingira, jamii na utawala bora kuwa sehemu ya msingi wa huduma zake.
Kwa mujibu wa Zaipuna, tuzo nyingine ambazo NMB imenyakua ni pamoja na Benki Bora ya Uendelevu Tanzania, Benki Bora ya Wateja Maalum Tanzania (kwa mwaka wa tatu mfululizo), Benki Salama Zaidi Nchini Tanzania na Benki Kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii, pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu Bora wa Benki Tanzania kwa Mwaka 2025, ambayo imetolewa kwa Zaipuna.
“Ni heshima kubwa kutambuliwa na Euromoney na Global Banking & Finance Magazine kwa uongozi wetu katika uendelevu wa huduma zetu kwa wateja,” ameongeza Zaipuna, huku akiwataja wafanyakazi wa benki hiyo kuwa sehemu kubwa ya mafanikio.
Hata hivyo, amesema kuwa kwa NMB, tuzo hizo zitakuwa chachu ya kuongeza jitihada na hitaji la kimkakati linalochangia uimara wa biashara, kuchochea ubunifu, kuongeza ushindani, na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya kudumu.

Amesema kuwa kwa kufanya uendelevu kuwa kiini cha mkakati wake wa biashara, NMB inalenga kuhakikisha wateja wanaendelea kufurahia thamani ya kudumu na kuwa na athari chanya katika maendeleo ya jamii.
Kwa sasa, NMB inatajwa kuwa miongoni mwa benki bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na mtandao mpana na wateja wanaofikia milioni 8.6.
Kwa upande wake, Mhariri Mkuu wa Euromoney, Louise Bowman, akizungumzia tuzo hizo, amesema: “NMB imedhihirisha kuwa taasisi kinara wa maendeleo endelevu nchini Tanzania na barani Afrika kupitia mipango yake ya kimkakati inayozingatia uwiano wa uwajibikaji wa kimazingira, athari chanya kwa jamii, na ukuaji wa kifedha.”
Amesema kuwa tuzo hizo zinabainisha dhamira ya benki hiyo katika uendelevu wa mazingira na jamii, sambamba na kutoa masuluhisho bora ya kifedha yenye viwango vya kimataifa yanayowezesha wateja na kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa kutambuliwa huko ni uthibitisho wa maono ya kimkakati ya NMB katika kuendeleza ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, huku ikipanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania wote.