NMB yaipiga jeki vifaa hospitali ya jeshi Arusha

Arusha. Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa tiba kwa hospitali ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kanda ya Arusha iliyoko Monduli mkoani Arusha vyenye thamani ya Sh3.1 milioni.

Vifaa hivyo ni pamoja na stendi za dripu, vitanda pamoja na magodoro kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaofika katika hospitali hiyo kupata huduma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo leo Jumatatu, Novemba 11, 2024, Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema taasisi hiyo imetenga zaidi ya Sh5.4 bilioni mwaka 2024 kwa ajili ya kuchangia huduma mbalimbali nchini katika sekta ya elimu, afya, mazingira na majanga.

“Leo tumekuja kutoa vifaa hivi kwa ajili ya kurahisisha huduma kufanyika katika hospitali hii tukitambua umuhimu wa afya bora kama moja ya kipaumbele chetu kwa maendeleo ya Taifa lolote duniani,” amesema Baraka.

Amesema Serikali inafanya kwa nafasi kubwa kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wakati na kwa ukaribu, hivyo wao kama wadau wa maendeleo, wana jukumu la kusaidia kuhakikisha mazingira na miundombinu yote ya afya inapatikana.

“Leo tunagawa vifaa hivi kama sehemu ya kutoa shukrani kwa wananchi wanaotuunga mkono kwa kufanya kazi na kufungua akauti zao kupitia benki yetu, tumetenga asimilia moja ya faida kuhakikisha inawarudia wananchi katika huduma mbalimbali wanazozihitaji,” amesema kiongozi huyo.

Akipokea vifaa hivyo, kamanda wa kikosi kinachosimamia hospitali hiyo ya jeshi Kanda ya Arusha, Luteni Kanali Jichola Masanja ameishukuru NMB na kusema hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya jeshi na taasisi hiyo ya kifedha.

“Kutupatia vitanda, magodoro na stendi za dripu zitawasaidia Watanzania wote wanaohudumiwa hapa na utasaidia kupanua wigo wa huduma, sisi kama wadau, tunaahidi kutunza vifaa hivi kwa manufaa ya wengi zaidi. Tunaomba ushirikiano huu uendelee si Arusha tu, na hata maeneo mengine nao wafaidike,” amesema mkuu huyo.