Njia za kulinda mtaji katika biashara yako

Katika biashara kunakuwa na mtaji wa muda mrefu ambao unashikilia msingi wa biashara yako ya mahitaji ya kifedha ya muda mrefu na mtaji wa uendeshaji wa biashara ambao unaweza kuongezeka au kupungua kutokana na namna ambavyo unaendesha biashara yako.

Mtaji wa muda mrefu ni ule unaowezesha kuweka msingi wa biashara kama kununua mashine ama vifaa vya kudumu vya biashara, kununua teknolojia, mashamba, au kufanya ujenzi.

Mtaji huu unahusisha fedha nyingi ambazo zinaweza kuchangwa na wanahisa kwa muda mrefu, ama mikopo ya taasisi za kifedha ya muda mrefu (zaidi ya mwaka mmoja) au kupata mwekezaji wa nje kwenye biashara yako.

Mtaji wa uendeshaji wa biashara unaohusisha fedha ambazo biashara inazo ama inazihitaji ili kushughulikia mahitaji ya kila mwezi au kukabiliana na gharama zisizotarajiwa.

Mtaji wa uendeshaji unaweza kukadiriwa kwa kuangalia deni lako la sasa ama tarajiwa, kwa mfano kwa mwezi.

Madeni haya yanaweza kuwa ni madeni ya watoa huduma, ama malighafi, kodi za serikali, bili za maji/umeme/simu, mishahara, kodi ya pango, au mikopo inayolipwa ndani ya mwezi.

Unaweza kulinganisha deni lako kwa mwezi na jumla ya mali za uendeshaji ulizonazo kama fedha taslimu, bidhaa za kuuza, mauzo tarajiwa ya fedha taslimu na madeni unayodai na ulipaji wake.

Tofauti ya kati ya mali au matarajio ya mali na madeni yatakuonyesha ikiwa unaweza kumudu biashara yako kifedha katika uendeshaji wake au unahitaji kuimarisha hali yako ya kifedha.

Ni muhimu kujua kama una mali nyingi na uwezo wa kuendesha kulinganisha na madeni kwa wakati husika, kwani inakufanya kuwa na maamuzi kadhaa ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

Kudhibiti madeni kwenye biashara: Unaweza kukosa fedha kulipia madeni ya biashara yako kwa sababu unakuwa na biashara ambayo imekopesha wateja wake na wakashindwa kulipia deni lao kwa wakati. Ni vyema kuweka sera madhubuti na kukopesha wateja ambayo haitaathiri mtiririko wa fedha kwenye biashara yako.

Kupanga mipango madhubuti ya kibiashara:

Kuangalia mtaji wako wa uendeshaji unakufanya kupanga namna ya kuweka bei za bidhaa na huduma, kuongeza malighafi, ama kuongeza watenda kazi au kupanua biashara yako.

Ikiwa mali yako inazidi deni lako, una mtaji wa kufanya kazi wa ziada—labda wa kununua vifaa vipya au kuongeza wateja kwa kutangaza biashara yako.

Kuomba muda wa urejeshwaji wa mikopo ya muda mrefu:

Mikopo ya muda mrefu huwa inalipwa kutokana na shughuli za uendeshaji wa biashara wa kila siku. Hivyo kukosa kulipa deni la taasisi ya kifedha kwa mwezi linaweza kukuweka kwenye mazingira magumu ya uhusiano wako na taasisi hizo.

Ni vema kufuatilia mtiririko wa kifedha kujua iwapo mwisho wa mwezi au robo ya mwaka utakuwa una ziada ya mali (fedha na malighafi) ama utakuwa na madeni.

Hii itasaidia kujua unapangaje mbinu kufanya biashara yako iwe na tija au kuinusuru kutokana na kukosa mtaji wa uendeshaji.

Kutafuta mkopo wa muda mfupi:

Mikopo ya muda mfupi inasaidia kutatua changamoto za muda mfupi kwenye biashara, hasa mahitaji wa muda mfupi kama kulipia kodi, kulipa mishahara au kulipa wadeni wa biashara, na mara nyingine kununua bidhaa kwa muda mfupi kuweza kuendesha biashara yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *