

Chanzo cha picha, Getty Images
Katikati ya moja ya dhoruba kali zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya siasa za Marekani, Kamala Harris anaselelea na kukata mawimbi pasi na shida.
Hali hiyo inaweza isidumu kwa muda mrefu.
Tony Fabrizio, moja kati ya wapiga kampeni waandamizi wa Donald Trump, anaiita hali ya kisiasa inayoendelea kama “Fungate la Harris” – ambapo muunganiko wa kuandikwa vizuri na vyombo vya Habari pamoja na mwamko wa kisiasa umekinyanyua chama cha Democrats na kukirudisha kwenye mstari.
Naam, na fungate kama ilivyo ada, hufikia kikomo.
Uhalisia wa maisha ya ndoa, kwa muktadha huu baina ya Bi Harris na wapiga kura wa Marekani, una namna yake ya kujipambanua. Lakini kwa sasa, bado sherehe zinaendelea na watu wanamimina shampeni.
Chama cha Democrats yawezekana sasa kimepata hisia ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kuzipata – matumaini. Upande wa pili wa shilingi, chama cha Republicans, ambacho kilishtushwa na tangazo la kihistoria la rais Joe Biden kubwaga manyanga, sasa wanajipanga upya na kuelekeza mashambulizi kwa anayetarajiwa kuwa mrithi wa Biden.
Yafuatayo ni maeneo matatu ambayo chama cha Republicans wamekuwa wakiyashambulia kumhusu Bi Harris, na kwa namna fulani, Democrats wanaweza kujaribu kuyakwepa.
1. Kumnasibisha Bi Harris na siasa kali za mrengo wa kushoto
Panda shuka za Bi Harris za kugombea tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha Democrats mwaka 2020 zipo wazi.
Katika kinyang’anyiro hicho ambacho Biden aliibuka na ushindi, Bi Harris alikuwa na mapungufu mengi ambayo yapo kwenye rekodi. Mapungufu hayo yanajumuisha kutokuwa na ujumbe ulionyooka, misigano ya ndani kwa ndani na kuwa mgombea ambaye alikuwa ni rahisi mahojiano yake kwenda mrama.
Kitu kimoja kikubwa kilitokea kwa Bi Harris ambaye kipindi hicho alikuwa ni Seneta. Katika kampeni zake – kama ilivyokuwa kwa wagombea wengine wengi wa Democrats – alijielekeza zaidi katika sera kali za mrengo wa kushoto ili kuwafikia kwa ukaribu zaidi wapiga kura wa mashinani katika chama hicho.
“Kulikuwa na shinikizo kubwa sana kutoka kwa wanaharakati wa ndani ya chama,” anaeleza Matt Bennett, kutoka Third Way ambayo ni taasisi ya uchambuzi wa sera ya mrengo katika chama cha Democrats.
“Ukiwa unapiga kampeni na kushindana katika ngazi za chini kabisa za kichama, vipaumbele vyako vya kisisasa vinakuwa tofauti kabisa kulinganisha na unapokuwa unashindana katika uchaguzi mkuu,” alisema Bw Bennet.
Katika midahalo na mahojiano yaliyofanyika mwaka 2019, Bi Harris aliunga mkono kuvunjwa kwa bima binafsi za afya na kupigia chapuo mfumo wa afya unaoendeshwa na serikali. Alipigia chapuo mabadiliko katika idara za polisi, ikiwemo kuhamisha fedha za bajeti ya polisi kwenda katika maeneo mengine ya kipaumbele.
Aliunga mkono pia kuhalalisha wahamiaji haramu kuingia Marekani na kuvunjilia mbali kikosi cha kupambana na wahamiaji haramu cha Ice.
Aliunga mkono pia kampeni na sera za kulinda mazingira ikiwemo kuzuia uchimbaji mafuta baharini.
Misimamo hii ya kisera, ambayo inaonekana ni ya kijamaa, sasa inaweza kumrudia na kumuandama.
David McCormick, ambaye anawania kiti cha Useneta katika jimbo la Pennsylvania kupitia chama cha Republican, ametoa tangazo la runinga linaloshambulia misimamo ya Bi Harris ya mwaka 2019 na kuinasibisha misimamo hiyo na mpinzani wake, Seneta Bob Casey kutoka chama cha Democrats.
Trump tayari ameshatoa video inayoitwa “KUTANA NA KAMALA HARRIS MWENYE MSIMAMO MKALI KUTOKA SAN FRANCISCO” ambayo inajumuisha sera nyingi alizounga mkono wakati huo.
Mchambuzi wa siasa wa kihafidhina Matt Walsh aliiita video hiyo kama ramani ya maelekezo ya namna ya kushambulia makamu wa rais, Bi Harris.
“Anaweza kujenga hoja, tena kwa usahihi kabisa, kwamba viongozi wazuri wanabadilisha msimamo wao kuhusu sera lakini hilo halibadilishi imani zao za kiitikadi za kisiasa,” anaeleza Bw Bennet na kuongeza “Hakuna msingi wowote wake wa kiitikadi uliobadilika.”
Ikiwa hatafanya hivyo kwa ushawishi, anaweza kupoteza uungwaji mkono na wapiga kura huru na ambao hawajaamua wamchague nani ambao wataamua matokeo ya uchaguzi katika majimbo muhimu ambayo hayana ushawishi wa moja kwa moja wa vyama hivyo vikuu vya kisiasa.
2. Kumuunganisha Harris na rekodi za Biden

Chanzo cha picha, Getty Images
Kura za maoni zaonesha kambia ya kampeni ya Biden ilikuwa ikiyumba kwa miezi kadhaa. Sera zake za uhamiaji hazikupendwa na wengi. Hata kama mfumuko wa bei umepungua na uchumi unaendelea kukua, bado wapiga kura wanamlaumu kwa gharama ya juu ya maisha.
Pia, kuendelea kwake kuunga mkono Israel katika vita vya Gaza, kulikuwa kunaendelea kupunguza uungwaji mkono wake miongoni mwa wapiga kura vijana.
Bi. Harris, katika nafasi yake kama makamu wa rais, kwa namna moja au nyingine kutajumuishwa katika rekodi za utawala wa sasa – ama kwa mazuri au mabaya.
Wafuasi wa chama cha Republican tayari wanajaribu kumuunganisha na suala la uhamiaji na kumtaja kama mtu mwenye kauli ya mwisho katika ulinzi wa mipaka ya Marekani katika utawala wa Biden – jambo ambalo sio sahihi lakini lenye kumharibia sifa.
Wanarejelea matamshi yake yaliyopita katika eneo la uhamiaji ambalo chimbuko lake ni mahojiano ya mwaka 2022, ambapo alisema kuwa “mpaka uko salama”.
“Kamala Harris pia kwa sasa anajulikana kama makamu aliyefeli ambaye alimpaka mafuta mkuu wake kwa mgongo wa chupa ili kupata nafasi ambayo kwa hali ya kawaida hangeweza kuipata huku wapiga kura wakikaribia kujionea kuwa, ndio mwanzo mambo yanazidi kuwa mabaya,” Taylor Budowich, ambaye anasimamia kamati ya kampeni yenye kuhusishwa na Trump alisema katika taarifa yake iliyodai kuwa watatoa dola milioni 32 katika matangazo yajayo ya televisheni yanayomlenga makamu wa rais.
Kulingana na Bw Bennett, Bi Harris hataweza kujitenga na rekodi ya Biden, lakini anaweza kuiweka katika mtazamo mpya kwa wapiga kura, hata wakati anakabiliana na siasa za Republican zinazolenga kummaliza kisiasa.
“Anachoweza kufanya ni kuweka mambo kwa njia ambayo ingekuwa vigumu kwa Biden, 81, kufanya,” anaeleza Bennet na kuongeza, “Anaweza kusema kwamba Trump anataka tu kuangazia mambo yaliyopita.”
3. Kushambulia rekodi zake kama mwendesha mashtaka
Katika mkutano wa kwanza wa hadhara wa kampeni yake ya urais, baada ya kuungwa mkono na rais Biden, Bi Harris moja kwa moja alielekeza mashambulizi kwa Trump.
Harris alisema kwamba alishawahi kuwa mwendesha mashtaka mahakamani na pia mwanasheria mkuu wa jimbo la California, na katika kazi hizo amekabiliana na “wahalifu wa kila aina”.
“Kwa hivyo nielewe ninaposema nawajua watu wa aina ya Donald Trump,” alihitimisha.
Craig Varoga, mshauri wa kampeni wa chama cha Democrats na mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Amerika, anasema uzoefu wa Bi Harris katika medani za kisheria na mahakama ndio turufu yake – ambayo alishindwa kuitumia kikamilifu alipogombea tiketi ya urais kupitia chama chake mwaka 2019, ambapo mabadiliko katika idara za polisi yalikuwa ni jambo la kipaumbele.
Hata hivyo, upande wa pili, wapiga kampeni wa Trump tayari wanaonesha ishara juu ya jinsi watakavyojibu mapigo katika eneo hili. Meneja wa kampeni wa Trump, Chris LaCivita, alipata umwamba katika chama cha Republican baada kugeuza turufu ya aliyekuwa mgombea urais wa Democrats na kuigeuza kuwa silaha ya kumuangamizia.
Mnamo 2004, mgombea urais kupitia chama cha Democrats John Kerry alikuwa akitumia rekodi yake ya kutukuka kama mpiganaji wa Vita vya Vietnam kama uthibitisho kuwa angelikuwa amiri jeshi madhubuti katika Vita vya Iraq.
Bw LaCivita aliongoza mfululizo wa matangazo ya mashambulizi yaliyotilia shaka uzalendo na ushujaa wa Bw Kerry, akishirikisha wanajeshi wanamaji ambao walipigana pamoja na Kerry kwenye boti za kivita zilizojulika kama ‘swift boat’ ambapo walipiga doria katika mito na pwani ya Vietnam.
Kampeni hizo zikazua msemo wa kisiasa uitwao “Swift-boating” – ambayo ina maana ya kummaliza mgombea kwa kumpokonya mgombea silaha yake ya kisiasa na kumshambulia nayo.
Sasa inaonekana kwamba kambi ya kampeni ya Trump inajiandaa kwa mashambulizi dhidi ya Bi Harris kwa kutumia rekodi zake alipokuwa mwendesha mashtaka.
Kwa upande mmoja, wanamshambulia kwa kusema alikuwa mgumu sana – haswa kwa wanaume weusi walioshtakiwa kwa uhalifu wa dawa za kulevya – na hili ni jaribio la kudhoofisha uungwaji mkono wake kutoka katika ngome yake ya wamarekani weusi.
Kwa upande wa pili, wanaorodhesha matukio ambayo Bi Harris aidha alichagua kutowashtaki ama alikubali kupewa msamaha watu ambao waliendelea kufanya uhalifu baada ya kuachiwa.
Bw Varoga anakiri kuwa Democrats walishindwa kukabiliana na mashambulizi ya Swift-boat ya mwaka 2004, lakini anasema wamejifunza kutokana na makosa na Bi Harris atakuwa tayari kukabiliana na mashambulizi.
“Ikiwa LaCivita anafikiri kuwa atafanikiwa kukizuzua chama kizima cha Democtrats kwa mara nyingine, basi anaweza kuishi na ndoto hiyo na kushindwa uchaguzi ,” alisema Varoga.