Njia alizopita Best Naso akijitafuta kimuziki

Dar es Salaam. Mashabiki wengi wa Bongo Fleva wanamkumbuka Best Naso kwa nyimbo zake kali kama Mamu wa Dar (2009) na Narudi Kijijini (2013) ambazo zilifanya vizuri kipindi hicho lakini haikuwa rahisi hadi kufikia hapo.

Leo anatueleza safari yake ya muziki na maisha alivyokuwa akiishi mikoa mbalimbali kama Tanga, Kilimanjaro na Mara ambayo yote ina mchango mkubwa kumtengeneza Best Naso tunayemwona leo hii katika muziki.

Anasema muziki ndicho kitu alichochagua hadi kuacha shule licha ya jitihada kubwa za wazazi na walezi wake, alifanya vibarua viwandani ili kupata fedha za kurekodi jambo alilolifanikisha baada ya mapambano ya muda.

“Watu wengi hawajui nina pande mbili za familia, upande wangu mmoja mimi ni mtu wa Musoma mkoani Mara, upande wangu mwingine ni mtu wa Tanga upande wa mama yangu,” anasema Best Naso.

Anasema hadi kuja kugundua ana kipaji cha muziki ilikuwa mwaka 1997 alipoenda Moshi, Kilimanjaro sehemu moja inayoitwa ‘Nyumba ya Mungu’ kwa shangazi yake, huko alikuta vijana wanarap, wakawa wanamwandikia mistari halafu anachana tu.

“Baadaye kuna wimbo wa Mabaga Fresh unaitwa ‘Tunataabika’ ulitoka, kupitia ule wimbo ndio kwa mara ya kwanza kabisa kuandika mistari yangu kupitia melodi zake, na kisha nikaandika wimbo wangu wa kwanza, Kilema,” anasema Best Naso.

Mwaka 2004 alifanikiwa kurekodi wimbo wake ‘Kilema’ kwa Prodyuza Mchopa ambaye studio yake ilikuwa Banana, Dar es Salaam, ingawa kabla ya hapo alirekodi wimbo ‘Sinyorita’ kupitia kinanda tu kwa usaidizi wa Benja anayefanya muziki wa Injili.

“Nilirekodi kwa kumlipa Sh15,000 tena kwa kumuomba sana, nilikuwa mtoto wa nyumbani sifanyika kazi yoyote hivyo sikuwa fedha ya kulipa, Mchopa alikuwa ameajiriwa hivyo pia muda wake ilikuwa ni mchache, kwa hiyo nilimuomba sana,” anasema Best Naso.

Anasema alipata elimu ya msingi Manga Kibaoni, Tanga ila alipofika darasa la nne baba yake mdogo alimhamishia Vingunguti, Dar es Salaam ambapo ndipo alihitimu darasa la saba.

“Elimu ya Sekondari nilianza lakini baadaye nilikataa, kwa hiyo sikufanikiwa kufika hata kidato cha nne, nilishia kidato cha tatu kutokana na sijui ni utoto au ujana ndio ulikuwa unaanza na mambo yakawa mengi nikawa sitaki shule bali muziki,” anasema.

“Mzee wangu ilibidi anitafute chuo cha ufundi, nilikwenda lakini nacho kilinishinda pia, niligombana sana na walimu ikafikia hatua nikafukuzwa, ilikuwa pale Sinza nilikuwa nasomea ufundi magari,” anasema Naso.

Baada ya kushindwa sekondari na chuo cha ufundi, Best Naso akaamua kufanya vibarua viwandani ili kukusanya fedha kwa ajili kurekodi lakini hakufanikiwa kupata na mwisho wa siku akaondoka Dar es Salaam na kwenda Musoma, Mara.

“Baada ya kuwa nimerudi Musoma harakati zikaendelea na ninashukuru ndiyo nilianza kufanya vizuri na mwaka 2007 niliachia wimbo wangu ‘Tumaringa’ ambao ulifanya vizuri kiukweli na kunitambulisha,” anasema Best Naso.

“Nipo kwenye orodha ya wasanii wakubwa wanaofanya shoo nyingi ndani ya nchi yao, sio kanda ya ziwa pekee, Moshi, Arusha, Mbeya, Iringa, Mtwara, Dar es Salaam, Tanga kote nishafanya shoo, kila sehemu natumbuiza,” anasema.

Katika maisha yake muziki Best Naso alitoa albamu tatu ambazo zimemtangaza vizuri, albamu hizo ni Mamu wa Dar (2009), Narudi Kijijini (2013) na The Gift of Life (2021).

Anasema albamu ya Mamu wa Dar iliuza kwa kiasi chake ingawa hana kumbukumbu ni nakala ngapi zilizoingia sokoni ila anashukuru mauzo yake yalifikia takribani Sh6 milioni kiasi ambacho kwake kwa wakati huo aliridhika nacho.

Kwa upande wa albamu yake ya pili, Narudi Kijijini (2013) ilifanya vizuri kutokana na umaarufu wa wimbo huo lakini upande wa mauzo mambo hayakuwa mazuri kwani alipata takribani Sh2 milioni tu!.

Licha ya muziki wake kufanya vizuri katika jamii, hadi sasa Best Naso hajawahi kushinda tuzo yoyote hata zile za muziki Tanzania (TMA) zinazoandaliwa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kitu ambacho anashindwa kuelewa sababu ni ipi!.

“Kwa bahati mbaya zaidi kwa miaka yote ambayo nimewahi kuwa katika muziki sijawahi kushinda tuzo wala kuchaguliwa kuwania, sijui ni kwanini labda wana sababu zao binafsi maana wanaoandaa tuzo ni watu pia,” anasema Best Naso.

Ikumbukwe kuna majina makubwa katika Bongofleva kama Dully Sykes, TID, Mr. Blue, Juma Nature, Belle 9 n.k nao hawajawahi kushinda tuzo za TMA ambazo zilianzishwa mwaka 1999 na kufanyika hadi 2015 ziliposimama na kurejea tena 2022.