Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni ametoa matamshi kuhusiana na ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani na kusema kuwa, mwaka 2025 utakuwa mwaka wa utawala huo ghasibu kunyakua na kupanua udhibiti wake katika ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Smotrich ameeleza kuwa, tayari ametoa maagizo ya kuandaliwa mazingira ya kupanuliwa udhibiti wa utawala wa Israel katika ukingo huo. Amesema: “Katika kipindi cha urais wa Donald Trump, wakati umefika wa kutekelezwa udhibiti wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, na ninatumai kuwa Trump ataunga mkono hatua hii.”
Tamaa ya utawala wa Kizayuni ya kutaka kunyakua ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan si suala geni bali imekuwepo tangu siku nyingi huko nyuma. Takriban Waisraeli 490,000 wanaishi katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, licha ya kuwa ujenzi wa vitongoji hivyo umetambuliwa na Umoja wa Mataifa kama “ukiukaji wa sheria za kimataifa.” Pendekezo jipya la Smotrich linahimiza kuhuishwa mpango wa ujenzi wa vitongoji ambao ulisimamishwa mwaka 2020. Mpango huo ulijumuisha kunyakuliwa kwa karibu asilimia 30 ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Mipango ya kuunganisha sehemu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Israel ilisimamishwa kwa muda wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Donald Trump kutokana na kutiwa saini mikataba ya kurejesha uhusiano wa kawaida wa Israel na nchi za Kiarabu.

Trump, ambaye alitekeleza mpango unaojulikana kama Muamala wa Karne wakati wa urais wake uliopita na pia kutambua rasmi Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, sasa ameshinda uchaguzi wa rais wa Marekani kwa mara nyingine tena, ambapo viongozi wa Kizayuni wanautaja ushindi huo kuwa fursa nyingine ya kuendeleza njama zao za kunyakua na kukalia kwa mabavu ardhi zaidi za Wapalestina.
Nchi nyingi na maafisa wa mashirika ya kikanda na kimataifa wamekosoa na kulaani vikali kauli hiyo ya Smotrich, ambayo inapingana wazi na makubaliano pamoja na sheria za kimataifa, na kusisitiza kuwa Ukingo wa Magharibi ni sehemu ya ardhi ya Palestina. Stefan Seibert, balozi wa Ujerumani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), amejibu matamshi hayo ya waziri wa mrengo wa kulia wa Israel kuhusu kutwaliwa kwa Ukingo wa Magharibi na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
“Muhammad Ahmed al Yamahi”, Mwenyeketi wa Bunge la Waarabu, pia amelaani vikali kauli hiyo ya Smotrich na kusisitiza kuwa: “Matamshi haya yanaibua hatari kubwa kwa usalama, amani na utulivu wa eneo na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, haswa azimio nambari 2334, ambalo linalaani hatua zote za Israel za kubadilisha jiografia ya idadi ya watu, utambulisho na hali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina tangu mwaka 1967, ikiwemo Quds Tukufu. Jambo muhimu la kuzingatiwa hapa ni kwamba maneno ya Smotrich siku chache zilizopita yanabatilisha moja kwa moja madai ya baadhi ya viongozi na maafisa wa nchi za eneo kuhusu uwezekano wa kupatikana amani na kuishi pamoja na utawala huo haramu unaoukalia kwa mabavu Palestina, utawala ambao umejengeka kwenye misingi ya ugaidi na kukanyaga haki za watu wa Palestina.
Tunapasa kusema kuwa, matamshi ya karibuni ya Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni kuhusiana na kupanuliwa udhibiti wa utawala huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuzuia kuasisiwa taifa huru la Palestina, yanaashiria malengo na hatua za kikoloni za wavamizi hao na kufunikwa haki za kitaifa za watu wa Palestina.