Njaa tatizo kubwa kikapu, Dossi, Happy watimka

UKATA ndiyo sababu moja kuu inayofanya timu 11 zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), zisifanye vizuri kwa nyakati tofauti.

Kukosa fedha za kusajili wachezaji na kukosa fedha kuendeshea timu kiujumla, vinafanya wachezaji wacheze kwa kujitolea. 

Ukiondoa timu ya Dar City inayomilikiwa na mdau mmoja wa kikapu Mussa Mzenji, ndio angalau imekuwa na mafanikio kutokana na kupata mmiliki anayeisimamia.  

Timu ya Stein Warriors iliyopanda daraja mwaka huu, imeonyesha imejiandaa vizuri ikiwa na wadhamini wakubwa, lakini timu nyingine maarufu kama Vijana ‘City Bulls’, Kurasini Heat, Mchenga Stars, KIUT, Srelio na nyingine zimejikuta katika wakati mgumu.

Kwa mfano timu ya Vijana ‘City Bulls’ iliyokuwa bingwa wa BDL 2019, Savio (2016-2017) na Kurasini Heat (2020), hizi zote mambo yamebadilika na tangu wakati huo hazijafanya vizuri.

Kati ya timu hizo, timu ya Kurasini Heat ilishuka daraja 2021 kutokana na kukosa fedha hali iliyofanya  wachezaji karibu wote watimke.

Kasim Jumbe, kocha wa kikapu kutoka Ilala, alisema timu zinazoendeshwa na wanachama, mwendelezo wake unakuwa hauna uhakika.

“Msimu huu unaweza ukafanya vema, msimu unaofuata unaanza upya,” alisema Jumbe.

Katika hatua nyingine, Tausi Royals imefanya kweli baada ya kumsajili Tumaini Dossi na Happy Danfoard kutoka Vijana Queens kwa ajili ya Ligi ya Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL).

Usajili wa timu ya Tausi Royals kwa wachezaji hao kutoka Vijana Queens, ni wa pili kwao baada ya awali mwaka jana kuwasajili Diana Mwendi, Tukusubira Mwalusamba na Juliana Sambwe.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Daudi Maiga alithibitisha timu hiyo kuwasajili wachezaji hao.

“Tulianza mazoezi na wachezaji hao tangu Januari kwenye Uwanja wa Shule ya International Academy (DIA),” alisema Maiga.

Kwa mujibu wa Maiga, wamejipanga kutoa ushindani mkubwa katika BDL wakilenga kubeba ubingwa mwaka huu. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *