
Uvumbuzi wa teknolojia kama blockchain, akili bandia (AI), majukwaa ya malipo, na mifumo ya usalama wa kidijitali unatoa picha ya jinsi huduma hizi zitakavyokuwa rahisi zaidi, salama, na zenye kubadilika ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Teknolojia za malipo ya simu, kama pochi za kielektroniki (e-wallets) na QR codes kuongezeka kwake zitaendelea kupunguza hitaji la fedha taslimu huku matumizi ya fedha kidijitali yakiongezeka zaidi, kutokana na kutoa fursa za kuweza kufanya malipo ya papo kwa papo kununua bidhaa, kulipia huduma na mengine.
Mapinduzi haya yanatoa fursa kwa wateja, wafanyabiashara, kwa kuwezesha miamala kufanyika kwa urahisi na kwa haraka zaidi.
Vilevile, akili bandia itazidi kuwa nyenzo itakayotumika kutoa huduma za kifedha kwa kulingana na tabia au sifa binafsi za mteja na kuwezesha kutoa mapendekezo yanayolingana na tabia za kifedha za wateja.
Kwa mfano, kwa kutumia programu za akili bandia, robo-advisors, chatbots na uchakataji wa taarifa kubwa (big data) na nyingine, zitatumika zaidi kwenye utoaji wa huduma kwa wateja kupitia mfumo wa majibu ya kiotomatiki ambao unaweza kujibu maswali ya wateja kwa haraka na kwa usahihi, hata wakati ambao benki zimefungwa sambamba na kutoa ushauri wa kifedha kwa wateja kupanga malengo ya kifedha bila kuhitaji ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa washauri wa kibinadamu.
Kwa upande mwingine, utoaji mikopo na bima vitatolewa kwa urahisi na kwa muda mfupi zaidi, Takwimu za matumizi ya kifedha za wateja kwenye mifumo ya kimtandao zitatumika kupima uwezo wa kukopesheka au kustahiki kwa huduma za bima, kwa mfano, utoaji wa mikopo utazingatia taarifa za kihistoria za kifedha za mtumiaji ili kubaini uwezo wake wa kukopesheka (credit scoring), itasaidia kuwezesha mchakato wa kukopa kuwa wa haraka zaidi na unaotabirika.
Sambamba na hilo, kutokana na urahisi, kupunguza gharama na mchango wa teknolojia, ni jambo la kutarajia na dhahiri kuwa utoaji wa huduma za kibenki kwa njia ya benki wakala, benki mtandao zitaongezeka zaidi sanjari na uwezo wa mawakala hao kutoa huduma zote muhimu za kibenki kwa njia za kidijitali zaidi ilivyo hivi sasa.
Nchi mbalimbali duniani zinaonyesha mwelekeo wa kuzindua sarafu za kidijitali (Central Bank Digital Currencies (CBDCs), ambazo zitatumika sambamba na fedha za kawaida kama fedha halali katika kufanya malipo. CBDCs zitaleta uwazi zaidi na kudhibiti mzunguko wa fedha kidijitali kwa usalama na uwazi.
Mbeleni, kutokana na msukumo wa sarafu za kidijiti na maendeleo ya teknolojia yake, si ajabu siku moja tunaweza kuwa na sarafu ya kidijiti ya Shilingi ya Tanzania kama pacha na mwenza wa sarafu iliyopo katika mzunguko wa uchumi kama fedha taslimu, na iliyopo kwenye mifumo ya kielektroniki.
Vilevile, ili kuboresha usalama wa miamala na kuzuia ulaghai, teknolojia kama blockchain, utambuzi wa alama za kibayometriki zitatumika zaidi katika utoaji huduma za kifedha. Blockchain itasaidia katika kutunza na kusambaza data kwa usalama na ufanisi, huku alama za kibayometriki zikiwa mbadala wa nywila, kwa ajili ya kudhibiti usalama wa kufikia akaunti za kifedha.
Kwa miaka ijayo, teknolojia hizi zitaongezeka kutumika zaidi kama njia ya kukabiliana na changamoto za ulaghai na kupunguza nafasi za upotevu wa fedha kwa njia za kimitandao.