

Chanzo cha picha, Balozi Burundi
- Author, Halima Nyanza
- Nafasi, Mwandishi,BBC Swahili
- Akiripoti kutoka Dar es Salaam
’….Mimi nilikuwa na hofu ya kwenda jeshini, mama yangu na baba yangu pia hawakupenda niende jeshini na kpindi hicho baba yangu alikuwa Tanzania akifanya biashara, hivyo nikaamua kwenda Tanzania kumfuata baba. Baba yangu alikuwa na nyumba Dar es Salaam eneo la Mnazi Mmoja, alikuwa na kibali cha kuishi Tanzania. Alikuwa Mfanyabiashara….’’’
Ni mwanzo wa mazungumzo yangu na Balozi wa Burundi nchini Tanzania Leontine Nzeyimana.
Anasema haikuwa rahisi kwake kufika katika nafasi zote alizowahi kushika lakini kutokana na jitihada zake binafsi anaona alistahili kushika nafasi hizo. Mbali na Diplomasia ni mwanasiasa. Amewahi kuwa Waziri wa Burundi wa Afrika Mashariki na pia Mbunge wa kuchaguliwa katika mkoa wa Makamba, unaopakana na Tanzania.
Mwaka 1993 mpaka 2005 Burundi ilikuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Makabila makubwa nchini humo Wahutu na Watutsi waliingia katika uhasama.

Mgogoro huo ulianza baada ya uchaguzi wa vyama vingi tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka kwa Wabelgiji mwaka 1962, na vita hivyo vilimalizika baada ya kuapishwa kwa Pierre Nkurunziza Agosti 2005. Inakadiriwa idadi ya watu waliokufa katika vita hivyo ni laki tatu.
Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe ndiyo vilivyomlazimisha Balozi Leontine Nzeyimana kuondoka nchini mwake.
‘’Machafuko yalipoanza mimi nilikuwa shule, nikamaliza sekondari na kufanya vizuri kwenda chuo.
Ulikuja utaratibu kwamba huruhusiwi kuanza chuo hadi upitie jeshini, kwa vile ulikuwa ni wakati wa vita na walikuwa wanataka wanajeshi wengi wa akiba wa kuweza kufanya kazi tofauti wengine wakienda uwanja wa mapambano.
Lakini kutokana na hofu yake ya kuingia jeshini na wazazi wake pia hawakupenda, ilimlazimu kuondoka nchini mwake na kwenda Tanzania, ambako baba yake alikuwa akiishi huko kutokana na biashara alizokuwa akizifanya na alikuwa akikaa katika eneo la Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha picha, ubalozi Burundi
Ufadhili wa Masomo ya Chuo Kikuu nchini Tanzania na kushiriki siasa za siri
Akiwa nchini Tanzania, Balozi Leontine Nzeyimana alipata bahati ya kupata ufadhili wa masomo ya chuo Kikuu, hivyo kujiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini kilichopo mkoani Iringa, nyanda za juu kusini mwa Tanzania.
‘’Baada ya kukaa Tanzania nikapata bahati ya kupata Scholarship (ufadhili) iliyotolewa na mke wa Rais aliyeuawa, Florence Ndadaye. Ndadaye Foundation (wakfu wa mke wa Rais wa Burundi aliyeuawa mwaka 1993). Mpaka leo tunamshukuru.’’
Wakati alipokuwa akisoma chuo kikuu, kipindi cha likizo jijini Dar es Salaam ndipo alipoanza harakati za kisiasa na kutafuta amani ya nchi yake.
‘’….Wakati nasoma nilikuwa najishughulisha na siasa hapa Tanzania kwa siri kwa sababu ilikuwa si dhahiri…wakati mwingine wapiganaji walikuwa wakija hapa Tanzania. Na walivyoanza mazungumzo rasmi nikawa nao pamoja kwenye mazungumzo. ‘’ Nilikuwa bado mdogo tunatumwa kazi kutokana na uzoefu wetu na umri wetu, lakini nilihusika kwa njia moja ama nyingine katika hiyo kazi….’’
Baada ya kumaliza shahada ya kwanza nchini Tanzania alifanikiwa pia kuendelea na masomo ya juu nchini Kenya.
Anasema anachokikumbuka katika mazungumzo hayo ya kutafuata amani ya Burundi, mjadala ulikuwa mkali kwenye makubaliano ya kuunda jeshi la nchi.
Baada ya vita kumalizika mwaka 2005, Balozi Leontine Nzeyimana ni mmoja ya Warundi wengi walioweza kurejea nchini mwao, ambako huko aliendeleza harakati zake za siasa na hata kufanikiwa kuchaguliwa ubunge katika mkoa aliotoka wa Makamba mwaka 2010.
Anasema kushiriki kwake katika mazungumzo ya kuleta amani ya Burundi kulifanya viongozi wa chama chake, ambacho baadaye ndicho kilikuja kuongoza Burundi cha CNDD-FDD kutambua mchango wake.

Chanzo cha picha, Balozi Burundi
‘Chama tulichokitumikia hakikutusahau’’
Anasema aliporejea alikuta hali ya amani tofauti na alivyoiacha, kila mtu alikuwa anajisikia huru, wale waliokuwa wakihisi mwanzo kwamba hawana haki, wasiwasi huo uliondoka.
‘’Kulikuwa na mabadiliko, kwa sababu wakati nilipotoka Burundi kulikuwa na hofu sana, woga sana, jiji letu la Bujumbura lilikuwa limegawanyika kikabila, ilifikia wakati mtu wa kabila moja hawezi kwenda katika sehemu nyingine ya mji, hata ukienda unakwenda kwa hofu, watu walihama ilikuwa ni wakati wa hofu sana’’
Balozi Leontine Nzeyimana anasema makubaliano ya amani ya Arusha yamesaidia sana kuleta amani nchini Burundi.
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika, hali ya usalama nchini Burundi ilirejea na wakimbizi wengi wa Burundi walirudi nyumbani.
Changamoto ya wakimbizi waliorejea nyumbani Burundi

Hali hiyo ilisababisha changamoto ya ardhi, hususan katika eneo lililo mpakani mwa Tanzania katika jimbo la Makamba.
Balozi Leontine Nzeyimana anasema mwaka 1972 pamoja na 1993 kulitokea machafuko nchini Burundi na raia wengi waliokimbia nchi walitoka katika mkoa huo wa Makamba unaopakana na Tanzania, ambako ndiko anakotokea.
Baada ya kurejea, wengi walijikuta bila ya nyumba wala mashamba kutokana na kwamba walivyoondoka mali zao na ardhi zilichukuliwa na watu waliobaki, yakiwemo mashamba na nyumba.
Kutokana na hali hiyo iliundwa Tume ya maridhiano ambayo ilikuwa na kazi ya kurudisha mali za watu, walioondoka, lakini bila ya kuathiri wengine.
‘’ Ilikuwa ni kazi kubwa sana na mambo mengi yalitendeka na wengi walipata mali zao, licha ya kwamba bado matatizo madogo madogi bado yapo.
‘’..Tulijikuta tuko na kesi nyingi sana kwa sababu mtu tangu mwaka 1972 ndiyo amerejea sasa, anataka haki yake, na serikali ikasema iwapo kuna ushahidi kila mtu apewe haki yake. Hivyo ukafanyika utaratibu wa kuwarudishia watu mali zao bila ya kuwafukuza wale waliokuwa pale. Kwa sababu wengine wazazi wao walikuwa wamezaliwa hapo na hawajui pengine.
Hivyo ikawa kama kugawa mali hizo, yule mwenye mali na yule aliyejikuta hapo, ikabidi wafanye maridhiano na kukubaliana jinsi ya kugawana mali.’’
Athari za jamii kubaguana

Chanzo cha picha, Ubalozi Burundi
‘’Kitu ambacho naweza kuelezea jamii ni kwamba tukubali jinsi Mungu alivyotuumba mnaweza kuwa mko makabila tofauti lakini Mungu amewaweka katika ardhi moja, hivyo wote tushirikiane tu ili kwa pamoja tujenga taifa kwa vile hakuna kabila linaloweza kuondoa kabila lingine, sijawahi kusikia kama kuna kabila lililoweza kufutika.’’
Wito wake pia ni kwa wanawake kuendelea kusomesha watoto wa kike akiamini kuwa mama akiweza, taifa limeweza.
Imehaririwa na Florian Kaijage