
Wanasema umdhaniaye ndiye kumbe siye. Unaweza ukamwona mtu mnadhifu ukadhani kuwa yupo sawa, lakini kumbe mtu huyo akawa ndiye chenga kulikoni mwingine unayemwona kuwa waluwalu.
Mara zote mtu hapimwi kwa suti wala vinjenga alivyovalia, bali kwa mwenendo wake wa maisha. Siku hizi hata vibaka nao wanavaa suti, chawa ndio usiseme maana hao ndio hutinga viwalo vikali kuliko mabosi wao.
Pia kuna neno kuwa mchafu hujificha kwenye usafi. Wengine wanasema utanashati huficha umasikini. Ndivyo ilivyo; ukiona mtu anayenyuka pamba kali asubuhi na jioni huku uswahilini anza kuwa na wasiwasi naye.
Wengi wao hawana mageto au wanaishi kwenye mazingira duni mno. Bila shaka hili ni zaidi ya tatizo kwani mhusika anaweza kuwa na upungufu wa afya ya akili (kama kuku anayepigana na kioo). Badala ya kuwa vile anavyotamani kuwa, mtu wa aina hii hutamani kuonekana mbele za watu vile anavyotamani kuonekana.
Siku si nyingi zilizopita niliongea sana kuhusu mikopo batili inayokwenda kwa majina chungu nzima kama mikopo umiza, kausha damu na majina mengine mabaya zaidi.
Nilisema iwapo mamlaka zitakaa kimya bila kuidhibiti, mambo mabaya sana yatarajiwe kuibuka. Niliyasema hayo kwa kuwa niliona wazi jinsi maisha ya Mtanzania wa kawaida yanavyotegemea mikopo, lakini kinyume na matarajio yao mikopo hiyo inageuka kuwa vitanzi badala ya ngazi.
Sikuacha kuwagusa walimu kama sekta mojawapo inayoathiriwa sana na mikopo hiyo. Walimu kama dira ya viongozi wa Taifa la kesho, wanajaribu kujiweka kwenye nafasi ya kutodharaulika kuficha hali zao duni.
Hapa ndipo wanapojikuta wakilazimika “kujitengeneza” ili waweze kubeba taswira isiyotia shaka. Kwa sababu ya uwezo wao mdogo, wamekuwa ndio wadau wakubwa wa mikopo ya kausha damu. Matokeo yake huwa ni mvurugiko wa afya ya akili unaotishia kukiingiza kizazi kwenye mtaro.
Janga la marejesho ya mikopo liliwapelekea walimu kuyakimbia madarasa na kwenda kupiga deiwaka kwenye vijiwe vya bodaboda ukizingatia lengo la wakopeshaji ni kupata faida kubwa kutoka kwa wakopeshwaji.
Walimu wakathibitisha kuwa kausha damu hailipiki kwa mshahara. Iliwabidi wapige kwata za miguu na mikono kutafuta ahuweni, lakini hali ilizidi kuwa mbaya.
Kausha damu wana jeuri ya kubeba kitanda alicholalia mgonjwa mahututi mwenye deni lao.
Kuvurugwa kwa afya ya akili hakuna tofauti na kuingiwa na uchizi.
Hivi majuzi tumesikitika sana baada ya binti yetu mmoja huko Simiyu kupigwa bakora zilizopelekea umauti wake.
Hata kama binti huyu angelimuua mwenzie, adhabu yake haikupaswa kuwa ya “sheria mkononi”. Mashuhuda wanaelezea jinsi alivyopigwa fimbo za mgongoni hadi kichwani.
Kama tungejua wenetu wanatandikwa bakora za vichwa, hakuna ambaye angethubutu kumpeleka mtoto shuleni.
Hii kadhia ni wazi kabisa kuwa inatokana na kuharibika kwa afya ya akili ya mwalimu. Yeye kama mzazi, hakupaswa kuadhibu kwa lengo la kuumiza. Hakuna mzazi anayeweza kukata mkono wa mwanaye aliyedokoa nyama jikoni.
Ni jukumu lake kumuondoa kwenye tabia hiyo kwa njia ya mafunzo, kama ingebidi basi ni adhabu ndogo tu. Wakati mwingine adhabu inapozidi, mtoto huwa sugu na kutosikia la muadhini wala mnadi swala.
Walimu wa zamani wanajulikana kwa uadilifu wao. Lakini wa sasa (japo si wote) wanasifika kwa vituko vyao. Ni kawida sana kusikia kwenye habari: “Mwalimu kampa ujauzito yatima”, “Mwalimu kalawiti wavulana wawili”, mwalimu kwenye kesi za unyang’anyi, fumanizi na kadhalika.
Pamoja na wao kuwa washauri bora kwenye jamii, hivi sasa ni miongoni mwa makundi yanayoongoza kwa kujinyonga.
Kwa kawaida ualimu ni fani inayobeba hadhi kubwa sana. Enzi zetu kule kijijini ukutanapo na muungwana aliyevaa mavazi nadhifu yaliyonyoshwa vizuri, viatu vilivyong’arishwa na anayeongea lugha nyofu, hutakosea ukibahatisha kuwa huyo ni mwalimu.
Hata watoto wao walijitanabaisha kwenye jamii kiasi cha kuwaongezea heshima wazazi wao. Japo hauna kipato cha kutisha, lakini ualimu uliongoza kwa heshima.
Katika maisha yetu sote tunajua heshima ya mwalimu. Licha ya kuwa wao ni watu muhimu sana waliotufumbua hadi tukajitambua, lakini pia mwalimu ni kiongozi asiyeyumbishwa na mambo ya mpito.
Kwenye awamu za viongozi wakuu hapa nchini, walimu wanaongoza kwa idadi na weledi. Ni kada yenye nguvu duniani kote kwani mwalimu wa kweli humpokea mzazi na kumsongesha mbele kijana wake.
Iwapo mwalimu asingefanya jukumu lake sawasawa, basi ajali ambazo zingesababishwa na mainjinia, marubani na manahodha zisingekuwa na idadi. Nashauri walimu wawe wakitazamwa kwa ukaribu, na ufanyike mpango maalum wa kuwaondoa kwenye majanga ya mikopo ya hatari haraka iwezekanavyo.
Bila kusahau, narudia kuomba waendesha mikopo inayovuruga afya ya akili wasitishwe mara moja kufanya hivyo wasiweze kuvuruga na kada zingine.
Dereva anayeelekea kuwasha gari hupima kwanza oil ili asijisahau na kuikaanga injini ya gari hilo.
Nasi hatuna budi kuwapima walimu wetu kila mara ili kuhakikisha wapo sawa kiakili.
Vinginevyo watatukaangia wenetu kabla hawajatimiza ndoto zao za kuliongoza Taifa lao la kesho. Na tusije kustaajabu tukija kupata viongozi wa “kimtindo” iwapo tutalichukulia poa suala kubwa kama hili.