NIKWAMBIE MAMA: Wagombea wasaidiwe kujaza fomu zao vizuri

Pale Nyumba ya Sanaa kulikuwa na watu wenye vipaji vya ajabu sana. Kaka yetu mmoja alikuta mti umeangukia njiani, wakati wapishi wakiona kuni zinawasubiri, yeye aliona taswira ya mamba kwenye gogo. Alilichukua na kuingia nalo karakarani. Akalichonga kuwa kinyago cha mamba aliyebeba vyura, kenge na mijusi. Akaiita kazi yake “Mamba wa Upendo”. Punde tu kazi hiyo ikauzwa kwa mamilioni ya shilingi kwa mtalii wa kizungu.

Msanii huona matokeo ya kile anachokifikiria kabla ya kuanza kazi yake. Kule “Mwisho wa Reli” wapo mabingwa wenye uraibu wa kubishana. Wanausanifu ubishi kabla hawajauanza, na wakiuanzisha ni lazima watashinda. Ni kwa sababu walishaufanyia michoro kabla. Mtu anadiriki kumlipa mwenzake ili amshikie ubishi wake pale anapopatwa na dharura.

Lakini msaidizi akishindwa au kutouendeleza ubishi huo, atalipa fidia!

Namkumbuka mwalimu wetu mmoja aliyeigeuza taaluma yake kuwa sanaa. Yeye aliweka lengo la ufaulu wa darasa lake zima, akawaza kuwaondoa woga wale wanaofeli wawafikie wanaopasi.

Sijui kama alikuwa sawa, kwani alikuwa radhi kupunguza alama za mwanafunzi aliyepata alama 100 ili asiwatishe wenzake, na kumwongezea aliyepata 10 ili aone kuwa inawezekana kupata 100.

Lakini mwishowe yeye ndiye aliyefeli baada ya wazazi kukagua mitihani yake kwa kina. Waligundua kuwa alitumia lugha tata na kuwapa tiki aliowakusudia, lakini akawapa mkasi wengine kwa jibu lilelile. Kwa mfano alitoa swali la kutafsiri sentensi “Mamba anaogelea ziwani”. Wote walimtafsiri mamba kama crocodile, lakini akawakosesha baadhi na kuwasahihisha kuwa Mamba ni jina la mtoto, huku akiwapasisha wengine kuwa mamba ni crocodile.

Hii inafanana na vituko vinavyoendelea kwenye vituo vya kuandikisha wapigakura kwenye serikali za mitaa. Wagombea wa chama “A” hawakuenguliwa baada ya kukosea kujaza fomu, lakini wale wa kuanzia chama “B” na kuendelea walienguliwa kwa makosa yaleyale. Kwa nini wasisaidiwe kuzijaza fomu hizo kama wenzao? Ieleweke kuwa kama makosa yalikuwamo kwenye mtihani, basi watahiniwa hawakuwa na makosa.

Yupo mtu aliyejihakikishia kuwa na ubovu wa meno kutokana na kuumwa meno kila wakati. Aling’oa jino moja baada ya jingine bila kupata nafuu. Alipomalizia kung’oa gego la mwisho, akalalamikia tena maumivu yaleyale. Wataalamu wakashtuka na kuunda jopo la uchunguzi. Masikini kumbe jamaa hakuwa na matatizo ya meno, bali fizi zake ndizo zilimsumbua! Hii ni kama ile ya mgonjwa wa kichwa kupasuliwa mguu.

Makosa mengine ni aghalabu kurekebishika. Kijana mwenzetu aliyeteswa na mapenzi alikunywa vidonge vingi kwa nia ya kujiua. Pamoja na kuvibwia kwa siri, joto la kifo lilipomkabili alijitokeza mwenyewe hadharani na kuomba kunusuriwa. Ni mfano wa mtu aliyekusudia kujinyonga; akishaitegua stuli aliyosimamia wakati akijitundika kitanzini, ataomba malaika ashuke kuja kumshikilia.

Ndivyo ninavyowaona viongozi wetu wanaosimamia zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wanajisahaulisha kuwa kuna maisha baada ya uandikishaji. Wao huchukulia ndio wamemaliza kila kitu, wakati bado hawajaandika hadithi zao vizuri (kama alivyosema mzee Mwinyi). Zoezi likifanyika kwa weledi, hadithi ya mtumishi husimuliwa na kusikika vizuri na waja hapo baadaye. Lakini akivurunda inakuwa kinyume chake.
Mifano ya viongozi walioadhirika baada ya kwenda kinyume na haki ipo mingi sana. Wengine hawakutoboa; walikamatwa au kuuawa, wengine walizikimbia kasri zao na kwenda kufia ugenini, tena kwa aibu. Wengine hawakusikika tena baada ya kukimbia. Baadhi yao walikataliwa hata kufagia barabara huko ugenini. Inasemekana yule aliyekusudia kuifanya dunia nzima kuwa himaya yake alikimbilia mtaroni, akajitumbukiza kwenye pipa la kemikali.

Ndugu zetu huku mtaani wafikirie kwa makini; Mifano ya hapo juu ni ya waliokuwa wakuu katika himaya zao. Meza ilipogeuka wakashindwa hadi kupanga chumba cha giza uswahilini, na wengine kutokubalika ugenini kwa madhila waliyoyazua. Sasa sembuse hawa wadogo ambao wanapostaafu wanawarudia walewale waliowatesa huku mtaani. Ni vema kuamua mapema: kama maji yanakushinda usiingize mguu.

Wakati mwingine tunawalaumu wakuu wasio na makosa. Lakini hatuachi kuwashauri kwamba wadogo wao hufanya maamuzi bila kutumwa. Juzi kati Mkuu wa Mkoa alitoa siri kwamba dereva wake alikuwa akienda kudai fedha kwa wafanyabiashara kwa madai kwamba alitumwa na Mkuu. Walishindwa kumkatalia kwa kudhani kuwa dereva alikuwa “chawa” wa Mkuu wa Mkoa.

Hivyo hawa wanaotimbanga huku mtaani hujikinga na makoti ya wakubwa wao. Si ajabu tunawalaumu wakubwa wakati wadogo wanafanya “uchawa” kwa faida yao. Kwamba mambo yatakapotiki wataonekana kuwa ni wapambanaji. Hawa si watu wazuri kwani wanamchonganisha bosi wao na wananchi. Mmesikia wenyewe jinsi wapigakura huku mtaani wanavyoapa kukipiga chini chama chao.

Sitaacha kuwaasa viongozi wangu, hawa machawa hawana jipya. Kwenye suala la uchaguzi kuna kukubaliwa au kukataliwa. Ikitokea ngome kubwa kuanguka, wananchi watasema “kumbe inawezekana!” Itakuwa kama Zambia ambako tangu kutetereka kwa chama tawala mwaka 1991, kambi ya upinzani inabadilishana Ikulu wakati chama tawala kipo kama kilichokwisha kujinyonga.