
Leo naanza na mfano hai. Msafiri na ngamia wake walisafiri jangwani kuanzia mapema alfajiri, wakati wa adhuhuri jua lilipokuwa kali, hawakuwa na budi kupumzika. Msafiri akamfungia ngamia wake na kupiga hema dogo, kisha akapumzika. Jua liliendelea kupanda utosini wakati fukuto likiendelea kuchukua nafasi. Ngamia akahisi ubongo wake ukichemshwa jikoni. Ilimbidi amwombe bosi asogee kando kidogo naye apate kupoza kichwa.
Bosi akaridhia na kujisogeza ili ngamia atulize kichwa hemani. Ngamia akafanya hivyo na maisha yakaendelea. Lakini dakika chache baadaye ngamia akadai kwa kuwa alihisi mishipa ya koo ikielekea kupasuka. Hivyo akamwomba tena bosi asogee zaidi ili apate ahueni. Bosi akaridhia na kujibana kwenye ukingo wa hema.
Ngamia akafurahia, lakini vipi kuhusu magega yake? Na tumbo? Je, miguu? Akawaza: “hapa nikitoa ombi jingine sitaeleweka, ni bora nifanye uamuzi halafu tutaeleweshana”. Akaingia mzima hemani, hema likaporomoka na wote wakabaki juani.
Simulizi hii haitofautiani na ya wapangaji wa maeneo ya biashara wa huku uswahilini. Mtu anapata uwezo wa kuendesha huduma za kifedha, anahitaji kajieneo kadogo kadiri ya hatua mbili kwa mbili tu kwa marefu na mapana. Wateja wake watakuwa ni wapita njia, hivyo hawatahitaji mambo mengi kama choo na sehemu ya kutupa taka. Dalali atamtafutia eneo la namna hiyo na kupiga hela yake.
Kesho mpangaji ataona kule ng’ambo ya barabara kuna akina mama wanauza mboga, kila mchana huwa wamemaliza mzigo na kwenda kujiandaa kwa kesho. Anaanza kuiona huduma yake ikimchelewesha. Akiangalia mtaani anaona biashara ya fasta ni kujaza wateja kwa kupima “visungura”. Bila kuwaza sana, anaamua kujiongeza.
Huku kwetu usitishike na karatasi ya bei, hata ikikuelekeza ununue kwa laki we toa Sh10,000. Daladala imeandikwa Tegeta Nyuki lakini ukiuliza unaambiwa inaenda Buza. Hivyo, hata ukiona kibanda cha miamala ya fedha ukiuliza utakutana na taarifa zisizo kwenye matangazo. Utaambiwa “cha kupima kinaanzia jero”. Mambo haya yananikumbusha enzi zile unakutana na muuza viatu kumbe anauza sigara; pafu Sh50.
Wanasema biashara ni kujiongeza. Lakini haiwezekani kujiongeza zaidi ya biashara yenyewe. Haijalishi ukubwa wa eneo, aina ya biashara ndiyo inayoamua mahitaji ya mteja wako. Mahala palipo na biashara ya wapita njia hapawezi kufanana na penye biashara ya walaji au walalaji. Ukiuza chakula na vinywaji lazima uwe na choo.
Hii si hiari bali ni faradhi. Mtu akinywa funda la kwanza la pombe, ni lazima figo ishtuke, kwani itahisi ugeni wa sumu mwilini. Haraka figo itakopa maji kutoka sehemu za mwili ili kuisukuma nje sumu hiyo. Mnywaji atalazimika kwenda maliwato kupata haja ndogo, hapo ndipo sumu inapunguzwa. Hatujasahau kuwa mwili unaingiza vingi lakini unatoa visivyohitajika ili mambo yaende.
Kariakoo inaingiza bila kutoa. Kitongoji kizima cha Kariakoo kimekuwa cha kibiashara kutokana na soko kuu. Kwa muda mrefu kitongoji hiki kilizidiwa na wafanyabiashara baada ya wadau kuchangamkia fursa zinazozunguka soko. Wafanyabiashara kutoka Zambia, Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda ni miongoni mwa wanaolitumia soko hili.
Kariakoo ilikuwa ikipumulia mdomo kutokana na kuelemewa. Na kwa vile kitongoji hakikuwa kimeandaliwa kibiashara ikawa shida. Wakongo na wingi wao walipogundua kuwa mzigo wao upo Kariakoo halafu dalali wa Kizaramo hajajiandaa ipasavyo, walivamia wenyewe na kutupeleka mpelampela.
Hivi karibuni Serikali iliamua kufanya marekebisho ya miundombinu na kuipa Kariakoo hadhi ya kuhudumia kimataifa. Hili ni jambo lililosubiriwa na wengi kwani wafanyabiashara walisumbuana na mamlaka kutokana na kanuni. Kama nilivyosema, hatukuwa tumejiweka tayari kwa mchakamchaka wanaokwenda nao wenzetu.
Lakini bado hatujatafakari. Jengo la ghorofa 16 liliporomoka hapohapo Kariakoo na kuua watu 36. Kampuni ya DPA ikatumwa kukagua ubora wa majengo kitongojini hapo. Ikagundua kuwa katika majengo 90 iliyoyatathmini, majengo 67 yalikuwa yamejengwa holela. Hatukuzingatia ushauri wake, na hata ule wa Tume ya Mheshimiwa Lowassa baada ya kuanguka kwa Hoteli ya Chang’ombe Village Inn mwaka 2006 pale Keko. Kwa mujibu wa Tume, kati ya ghorofa 505 zilizokaguliwa, 147 zilikutwa hazina nyaraka za ujenzi.
Kwa mujibu wa Mwananchi Digital, fundi mmoja anakiri kwamba yeye na wenzake wawili walipewa kazi kwenye jengo hilo lililobomoka. Kazi ilikuwa kubomoa kuta za ndani ili kuongeza maeneo ya upangishaji. Waliianza Novemba 14 mwaka huu, lakini wakati wakibomoa waliona udongo ukishuka kutoka juu. Siku ya ajali ilikuwa ni siku yao ya kumalizia kazi. Fundi alishtuka baada ya kuona zege likikatika na kelele chini ya jengo. Akawashtua wenzake na kwa pamoja wakasepa.
Majengo ya Kariakoo yamechoka. Kwa akili ya kawaida mtu mzima akivunjika nyonga tatizo huwa kubwa. Wakati jengo limezidiwa, mtu anapiga ukuta nyundo kwa lengo la kuongeza mzigo mwingine! Kwa lugha nyingine tunasema “shimo ndani ya shimo”.
Mimi ningepewa kipaza sauti ningesema Kariakoo ifungwe na ijengwe upya ili ikutane na hadhi ya soko la kimataifa. Ila nawamaindi kinoma wapangishaji wanaotuumiza kwa tamaa ya faida ya tele kwa tele!