
Kwenye mchezo wa ndondi bondia anaweza kufanya kama aliyejisahau, akakuletea uso usiokingwa na mikono yake.
Mbinu hii wenyewe wanaiita “kuuza sura.” Ukiamini kuwa kajisahau, utaingia kichwa kichwa, lakini ghafla atakuwahi na kukumaliza.
Mabondia wengi wameshaumizwa kwa mtindo huu, lakini mabondia wajanja hupuuza chambo hicho na kuendelea na pambano kwa kuzingatia kanuni za mchezo.
Wakati mwingine bondia huyo anaweza kukurushia matusi ya nguoni ili kukupandisha hasira na kukupoteza umakini.
Anafanya hivyo kwa umakini mkubwa asisikiwe na mwamuzi ili asiadhibiwe. Usipokuwa makini utagadhabika na kuamua kumtwanga kwa hasira. Kwa kuwa yeye alikwishakujiandaa na hilo, atakuwa akikukwepa kwa urahisi na kukumaliza kwa urahisi mithili ya mvuvi anavyompata mkisi mwenye hasira.
Kwenye mpira wa miguu pia zipo mbinu kemkem zinazoyafanya mataifa fulani kung’ara kwenye medani hiyo. Mbinu niliyoipenda zaidi ni ile ambayo timu “A” inacheza golini kwao ili kuwavuta mahasimu wao wawafuate kujaribu kupata goli. Timu nzima ya mahasimu inadanganyika na kuvutika upande wao.
Timu “A” inapoona hivyo, inatoka mbio nyingi na kufanya shambulizi la ghafla hata kupata goli.
Inafanana pia na mbinu ya kivita iliyobuniwa na Mfalme Chaka wa Afrika ya Kusini.
Yeye alilipanga jeshi lake kwa mtindo wa “V”. Kutokana na miti na mawe yaliyopo kwenye uwanja wa vita, adui aliweza kuona askari wachache kule mwishoni bila kuwaona wengi walio kando.
Hivyo madui hao waliingia katikati ya “V” bila kutambua, ndipo jeshi la Chaka lilipojifunga mithili ya duara na kuwashambulia.
Mapambano yote yana mbinu za ushindi, na wenye uzoefu na mbinu nyingi ndio wenye nafasi kubwa ya kushinda.
Tumeshuhudia timu zetu zikiwa na ubora wa kuzipita timu za mataifa mengine, lakini mara tunapokutana nao uwanjani tunashindwa kupata matokeo mazuri.
Sababu ni kwamba wanatuzidi kwa mbinu za kimichezo. Hii inatokana na uzoefu wetu mdogo kwenye mashindano ya kimataifa.
Mbinu hizi zote na za ziada, utazikuta kwenye siasa.
Kambi moja inaweza kuiuzia sura kambi nyingine kuipotezea dira.
Kama vile bondia anavyomtusi mpinzani wake bila kusikiwa na mwamuzi, ndivyo chama kimoja kinavyoweza kukiingiza mkenge chama pinzani. Kwa kuwa anayeanza huwa haonekani, yule anayejibu mwishoni ndiye mwenye hatari kubwa ya kufanya makosa.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unaanza na vurugu baina ya chama cha upinzani na vyombo viwili muhimu; Tume ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi. Katika mfumo wetu wa utawala, Serikali huundwa na chama kimoja kinachoshinda uchaguzi huo.
Hiki ndicho kinachoteua wasimamizi wa uchaguzi ambao chenyewe pia hushiriki. Hivyo malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi na Tume ya Uchaguzi ni malalamiko dhidi ya Serikali.
Serikali kama msimamizi na mlezi wa vyama vyote vya siasa haipaswi kuegemea upande wowote. Ni sawa na mwamuzi katika pambano la mahasimu. Mwamuzi anatakiwa kuwa makini sana na mchezo, kwani lolote laweza kutokea.
Anaweza kudanganywa na mbinu za kimichezo akadhani hayo ni madhambi na akayachukulia hatua, au pengine akadanganywa na figisu na kujikuta akitoa haki upande usiostahili.
Katika mchezo wa robo fainali za Kombe la Dunia mnamo mwaka 1986, mchezaji Diego Maradona alitumia ufundi mkubwa kuipatia ushindi Argentina dhidi ya Uingereza.
Alimdanganya mwamuzi kuwa anapiga mpira kwa kichwa, kumbe akatumia mkono. Nawaza kile ambacho kingetokea iwapo mwamuzi huyo angelikuwa ni raia wa Argentina; bila shaka angeuawa na mashabiki kabla ya kutoka uwanjani.
Kwa mfano huo tungependa Tume ya Uchaguzi na Serikali kwa ujumla kuwa makini sana kabla ya kutoa maamuzi.
Mambo makubwa huanza na madogo, kama hatutaongeza umakini tunaweza kuingia kwenye orodha ya mataifa yasiyozingatia chaguzi za kidemokrasia.
Ni doa kubwa sana kwa nchi kama Tanzania ambayo haitegemewi kuingiwa na mzimu kama huo. Ni kawaida ya mtu muadilifu kuwa zaidi ya shetani mara anapopigwa mhuri wa dhambi.
Tanzania ni nchi iliyolelewa katika maadili, upendo na amani, ikiwa na zaidi ya miaka sitini ya muungano. Tumevumiliana na kusahihishana kwenye tofauti zetu bila kukwaruzana.
Basi tusitegemee kupata utulivu wa mapema mara tutakapoanza kupigana wenyewe kwa wenyewe baada ya kutofautiana kisiasa, kiimani, kiuchumi na kadhalika.
Natoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuwa mfano mwema wa kudumisha amani nchini.
Kama nilivyosema, makubwa huanza na madogo. Nimpongeze Katibu Mkuu wa CCM kwa mfano mzuri aliotuonesha hivi majuzi.
Alipokelewa na wimbo uliotungwa na wafuasi wa chama chake, lakini baada ya kuusikiliza aligundua kuwa wimbo huo ulikuwa na maneno ya kibaguzi. Aliupinga kwa kusema chama chake hakina nia ya kuchochea ubaguzi.
Vyama vingine viichukue falsafa hii na kuwaelimisha wafuasi wao kurekebishana kwa maelewano.
Uchaguzi ufanyike kwa haki na usawa bila dhuluma. Pasiwepo magoli ya mikono hata kama wasimamizi hawatayaona. Mwisho wa siku sote tumuunge mkono mshindi tukijifunza mazuri yake na kurekebisha mapungufu yake. Tumwombe Mungu aubariki Uchaguzi Mkuu wa 2025 uwe wa amani na ukweli.