NIKWAMBIE MAMA: Uchaguzi Mkuu asibebwe mtu

Inatia moyo kuona vyama vyote vya siasa, kuanzia chama tawala hadi vile vya kambi ya upinzani vikijiimarisha kufanya uchaguzi wa huru na haki.

Nasema hivi kutokana na kauli za vyama hivi kuwakemea wagombea wake wenye tabia za rushwa na kubebwa.

Tofauti na chaguzi nyingi zilizopita, kauli za viongozi wa vyama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu zinatoa nuru ya kutendeka kwa haki.

Zamani zile tulisikia malalamiko mengi kutoka kambi ya upinzani. Wagombea wao waliwalalamikia wenzao wa chama tawala kuwa walikuwa wakiwatambia kuwa hawatawaachia nafasi hadi kiyama.

Lakini mbaya zaidi chama hicho tawala kilisikika kupitia kwa baadhi ya watu wake kwamba hata kingesimamisha jiwe badala ya mtu, chama chao kingeshinda uchaguzi. Na kwa vile matokeo mengi yalikuwa chanya kwao, kauli hizo zilionesha kumaanisha.

Hali hii ilichangia sana kutokujiamini kwa kambi ya upinzani. Tulizoea kuona viongozi wa kambi ya upinzani wakihama vyama vyao kwa kile kilichoaminika kuwa ni “kurubuniwa” na chama tawala, hivyo kuachia majimbo na kupunguza idadi ya wawakilishi wa upinzani.

Pia tuliona waumini waadilifu wa upinzani wakivikwepa vyama vyao na kukimbilia kwenye chama tawala ili kupata uhakika wa kushinda majimboni.

Hii ilitokana na wagombea hao kujihakikishia kuwa ndani ya mbeleko isiyochanika.

Lakini kauli zinazoendelea kutolewa na viongozi wakubwa wa chama tawala zinatoa nuru ya uchaguzi kuwa huru na wa haki.

Viongozi hawa wamekemea rushwa kwenye uchaguzi, na wamewataka wagombea kutotegemea “kubebwa” na chama bali wajibebe kwa utumishi wao.

Kwamba wajiimarishe wenyewe ndani ya jamii kiasi cha kuwapa tumaini wapiga kura. Pengine huu ni ukurasa mpya kwenye kitabu cha uchaguzi wa kidemokrasia.

Lakini tayari kuna sintofahamu zinazoendelea katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu.

Baada ya kupigwa stop kwenye rushwa pamoja na kubebwa, viongozi wanaotarajia kugombea wanaanza kuchangamkia fursa ya kukusanya fedha kinguvu kutoka kwa wananchi.

Tayari kuna michango ya lazima inayopitishwa kwenye vikundi vya wajasiriamali na vijiwe vya bodaboda kwa lengo la kuwafanyia wepesi wagombea hao. Hii ni sawa na rushwa ingawaje mtoaji hajui kwamba anaishiriki.

Hatukatai kuwa ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni jambo la lazima. Hii ni pamoja na kuvunja vijiwe vinavyoashiria uvunjifu wa amani huku mitaani, na kuwapeleka wahusika mbele ya sheria.

Lakini sasa zoezi hilo linabeba sura ya ukusanyaji haramu wa fedha kutoka kwa raia. Watu wanakamatwa na kufikishwa kwenye ofisi ya Mtaa na Kata wakitishiwa kufungwa iwapo hawatatoa chochote.

Mambo haya yanaashiria uwepo wa viongozi wachache wanaojisafishia njia za kushika hatamu kwa kutumia mchezo mchafu.

Tuliposikia kuwa viongozi watajibeba, tulipata faraja ya kuwepo kwa uwiano baina ya wagombea. Tuliamini kuwa muomba kura ataonekana katika rangi yake halisi.

Hii ingemfanya mpiga kura kumtathmini mgombea kwa uwezo wake bila kudanganyika na rangi ya fedha za chama.

Hivyo hawa wanaolazimisha michango huku mtaani ni wazi kuwa wanajificha kwenye kivuli cha Serikali kuchangisha fedha isivyo haalali.

Tatizo kubwa la watu wasio na karama ya uongozi ni mabavu. Wanaamini kuwa kama vile pesa inavyoweza kusambaratisha milima na mabonde, basi nao wataweza kufanya lolote kwa kutumia pesa.

Rushwa imenata kwenye fikra zao, na wengi wao hivi sasa wanashindwa kujenga hoja za msingi mbele ya wapiga kura.

Kiongozi yeyote mwenye mapungufu ya fikra haamini kabisa kupata kiti bila kuhonga.

Hii ni kwa sababu anajijua kuwa hana ushawishi mwingine kama uchapa kazi, utimizaji wa ahadi na hata historia nzuri inayoweza kumshawishi mpiga kura.

Hata kwenye maongezi, kuna tofauti kubwa kati ya huyu anayepiga ngonjera za mafanikio na yule anayechanganua mifumo ya maendeleo.

Ni lazima Serikali ijihadhari na mbinu za watu hawa wanaoichukulia Serikali kama chombo cha kuwaburuza wananchi ili wafanikishe malengo yao.

Na mwisho wa siku Serikali ndiyo itakayolalamikiwa kwa vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na sheria.

Ni uhalifu kama uhalifu mwingine wowote unaofanyika mitaani, na hatua zake zisitofautiane katika kuukabili.

Kwa mfano katika kamata kamata inayoishia mtaani, wahusika watawakamua fedha wakamatwaji ambao wataamini kuwa huo ni mpango wa Serikali.

Jeshi la Polisi nalo litaingizwa kawamani kwa kuvunja sheria na kukiuka katiba. Wakati huo hawa waliotenda dhambi hiyo watakuwa wamejificha salama kwenye ngao ya Serikali. Iwapo Serikali itawaonea haya watenda maovu ya aina hii, itajiweka kwenye hatari ya kukosa uaminifu wa wananchi wake. Madhara makubwa yanaweza kutokea baada ya kuasisiwa na watu wachache tu kama tunavyoona yanayoendelea kutokea huko nje. Hapa sisi hatuhitaji migogoro, kwani hayo ya majirani zetu yanatukosesha usingizi.

Tunachohitaji ni kushiba ugali wetu na kumshukuru Mungu. Hayo mengine tuwaachie wazoefu.

Chonde chonde waomba kura, mjibebe kwa sifa zenu na wala si kwa fahari ya vyama. Mjifunze kujitegemea kwani hivyo ndivyo tunavyoishi kutoka siku hadi siku huku mtaani.

Mbeleko ya mama inaishia pale unapotembea, hivyo kazeni kamba za viatu vyenu muende!