NIKWAMBIE MAMA: Taka ni fursa itumike

Kuna baadhi ya tungo za muziki zinafikirisha sana. Vijana wawili wa zamani waliuliza kwenye utunzi wao: “Ingekuwa vipi kama pumzi ingeuzwa buku?” Ni swali fupi lakini tafakuri yake inaishi tangu wakati huo na itaendelea kudumu mpaka vizazi vijavyo. Inaakisi maisha ya uhalisia, na ina majibu tofauti kulingana na kina cha tafakari ya mtu anayejibu.

Vijana hao walijibu kwamba masikini wote tungekufa, kwani kulipia elfu moja kwa kila pumzi si jambo dogo. Ukigawanya siku moja moja kwenye umri tulionao sasa, na ukizidisha elfu moja kwa siku hizo ni fedha nyingi sana. Hivi leo kuna watu wanaoshindwa kupata mlo mmoja kwa siku nzima, sasa fikiria wangewezaje kulipia pumzi kila baada ya sekunde? Kuna sekunde ngapi kwenye siku?

Lakini mimi niliona kuna kitu za ziada; hakika asingelibaki mtu. Umeme unapoisha nyumbani na ukajikuta huna uwezo wa kuununua, unaahirisha baadhi ya mambo wakati unatafuta namna ya kutatua tatizo hilo. Utaachana na TV na pengine ukashindwa hata kufanya kazi zako kwenye muda huo. Lakini cha kufurahisha ni kwamba utabaki hai ukitafuta namna nyingine.

Lakini pumzi inapokata kiumbe hai hukosa muda wa ziada. Hawezi kuahirisha kupumua ili akatafute vocha ya kujazia pumzi nyingine. Ndio maana vijana wale wa zamani wakasema masikini tungelikufa. Ila mimi nawaongezea kuwa masikini tungetangulia kufa tukifuatiwa na matajiri. Yaani sote tungekufa. Hakuna tajiri bila masikini kwa sababu hawa wawili wanategemeana kama nzi na kidonda.

Wakulima wawili walioanza kilimo cha jembe la mkono watatofautiana baada ya mmoja kujiongeza.

Hapo kabla wote walilima ili kukidhi mahitaji ya chakula majumbani mwao. Waliitwa masikini kwa sababu upo wakati ambao mazao yalikataa. Pengine ni kwa sababu za kawaida za kimazingira kama ukosefu wa mvua.

Hivyo kuhemea chakula au kulala njaa kwenye familia za wakulima hawa halikuwa jambo la ajabu.

Mmoja wa wakulima hao anaweza kujiongeza na kufanya kilimo cha umwagiliaji kisichotegemea sana misimu.

Atapata mavuno mengi kiasi cha kuwa na ziada ya kuwauzia wenzake waliokosa. Pia atakuwa na ziada ya kununua mbolea na pembejeo zilizo bora. Akili ikimkaa sawa, atajiongeza kwa kilimo cha mazao ya biashara.

Atanunua matrekta, magari ya kusafirisha mazao yake kwenda sokoni, na ataajiri wafanyakazi.

Huyu sasa ni tajiri. Lakini msingi wake ni wanunuzi wa bidhaa zake, wengi wao wakiwa ni masikini kama alivyokuwa yeye.

Kama masikini wasingenunua mazao yake, asingelikuwa na ukwasi alionao sasa. Ndio maana nasema iwapo tungelipia kila pumzi tunayovuta, masikini wangekufa na tajiri angekosa mtu wa kumuuzia. Naye angefilisika na kukosa buku ya kulipia pumzi ya sekunde.

Watu wanaoishi mijini watakubaliana nami nikisema matumizi ya nishati safi yalianza zamani sana.

Huku nje tuna mitaa ya uswahilini na ile ya ushuani. Katika nyakati za sikukuu, watoto wa uswazi walialikwa kwa anko kusherehekea na wenzao ushuani.

Huko walikuta mizinga ya Johnnie Walker, Grants, VAT 69 na mingine tofauti na mizinga ya gongo, mdafu na komoni waliyoizoea. Walikunywa maziwa kwa mayai badala ya chai mkandaa kwa vitumbua.

Pia watoto wa kishua waliwafunza wenzao namna ya kupika kwa nishati za gesi na umeme. Hakuna mtoto wa uswahilini ambaye hakuyapenda maisha ya ‘makochini’.

Kwa muda mfupi walisahau maisha ya kukatiza usingizi kwa safari za kwenda kutafuta maji, kuni na kufukuzana na visiesie na tongwa wanaomaliza mpunga shambani.

Pale ushuani kwa kubonyeza kitufe cha jikoni unawasha jiko, kitufe cha bafuni unaoga, cha sebuleni unapunga upepo baridiiii…

Tofauti ya uswahilini na uzunguni ni uwezo wa kimaisha. Wazee wa ushuani ni mabosi na wafanyabiashara wakubwa, wakati uswahilini kuna makapuku wa hali ya chini na wachache wenye uwezo wa kati. Hizo ni takwimu ingawaje hata kule Masaki kuna “Mwembe Sindimba”, migoma na mapombe ya kiswahili kama kawaida. Pia hata uswazi ukisikia nahau ya “Mzungu Mweusi” ujue kuna bosi hapo kitaa.

Mmoja ni Mzaramo aliyefanikiwa sana kwenye biashara ya utalii.

Mzee huyu japo alikuwa na uwezo wa kutumia nishati safi tangu enzi hizo, utamaduni wake ulipelekea matumizi ya nishati chafu pale kwake.

Alidai kuwa hakuna wali bila ukoko, alihamasisha mapishi ya kuku kwenye chungu na jiko la mkaa, na kuku aokwe kwa moshi wa kuni.

Aliwahi kusikika, akisema ladha ya maji ya kwenye jokofu haifikii maji ya mtungini kwenye kombe la bati!

Watu wa aina hii wanahitaji sana mkaa safi unaozalishwa na kutumika bila kuathiri mazingira.

Hawa na wale wenye hali ngumu sana wawe wa kwanza kufundishwa uzalishaji wa mkaa safi kwa kutumia malighafi rahisi kama taka.

Tuache kukariri kuwa taka ni hatari, na tuchukulie taka kuwa fursa. Kwa mfano hivi sasa huku uswahilini ukikutwa unazika taka ili kutengeneza mboji unakamatwa. Ati ni kwa sababu “unakwepa” ada ya usafi.

Tuachane na fikra hizi.

Mkaa unaozalishwa na taka utadumisha utamaduni wa wazee wa ukoko, utaongeza kipato na utahifadhi mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *