
Nikikumbuka stori ya mtego wa panya huwa napata woga sana. Katika stori hii, panya anauona mnofu wa samaki aliotegewa. Anamwomba jogoo autegue ili apate riziki yake, lakini pia anatahadharisha kuwa mtego wa panya una hatari kubwa. Haumchagui panya pekee bali hunasa waliomo na wasiokuwamo. Jogoo anampuuza na kwenda na hamsini zake. Panya anamwendea mbuzi, lakini pia mbuzi hampi ushirikiano. Bila kuchoka, panya anamfuata ng’ombe na kumtaka msaada uleule. Ng’ombe anacheka na kumjibu kuwa balaa lile hajaandaliwa ng’ombe mtoa maziwa, bali ni la panya mdokozi.
Usiku mwenye nyumba anastushwa na mfyatuko wa mtego. Anapapasa kizani, lakini ghafla anapiga uyowe baada ya kung’atwa mkononi. Mkewe anabeba taa na kuja haraka kwenye eneo la tukio. Anamkuta mumewe akigaragara kando ya mtego uliomnasa nyoka. Mama anagundua kuwa si panya aliyemgonga mumewe. Anapiga mayowe kuwaamsha majirani, lakini mzee anakata moto kabla hawajampakia kwenye bajaji. Inasemekana stori hii haikutungwa ila ilitokana na kilichotokea siku zilizopita. Tuendelee…
Asubuhi majirani wanakusanyika kusikiliza masaibu yale. Kwa sababu bado watu ni wachache, mchana wanapikiwa ugali, na jogoo anapendekezwa kuwa kitoweo. Habari ya msiba inasambaa haraka hivyo siku inayofuata mipango ya mazishi inafanywa. Wahudhuriaji wanapikiwa wali na siku hiyo mbuzi anachinjwa. Siku ya tatu marehemu anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Kwa kuwa kinachofuata baada ya mazishi ni kuanua tanga, ng’ombe naye anachinjwa kuhitimisha shughuli. Neno la panya linatimia: Mtego wa panya hunasa waliomo na wasikuwamo.
Uchaguzi Mkuu wa 2025 unaanza kuchukua sura ya mtego wa panya. Wakati Tume Huru ya Uchaguzi ikisisitiza kuwa kila kitu kipo sawa, baadhi ya washiriki wa uchaguzi huo wanaipinga kauli ya Tume. Wanadai bado majibu ya maswali ya msingi hayajatolewa. Wakati ule wa mchakato wa ama tuendelee na mfumo wa utawala wa chama kimoja au tuingie kwenye demokrasia ya vyama vingi, Watanzania wengi walipiga kura kutaka kuendelea na mfumo wa chama kimoja.
Iwapo Mwalimu Nyerere angezingatia filosofia ya “wengi wape”, leo tusingelikuwa miongoni mwa mataifa yenye tawala za kidemokrasia. Pengine tusingedumu na amani tunayojivunia tangu enzi na enzi.
Kuelekea uchaguzi ujao, nchi yetu imeanza kuingia kwenye kurasa za vurugu za kisiasa.
Wanasiasa na wasio wanasiasa wamekuwa wakikabiliana na mashitaka na vichapo kutoka kwa vyombo vya dola.
Hii inatokea kila mara pale Jeshi la Polisi linapopambana na makundi ya watu kwenye maandamano, mikutano ya hadhara, na mikusanyiko katika sehemu tofauti, ikiwemo Mahakamani.
Lakini imeshuhudiwa mara kadhaa Jeshi la Polisi likiharibiwa sifa na watu wahuni. Matukio ya raia wema kutekwa na “watu wasiojulikana” yamekuwa yakipamba vichwa vya habari kila baada ya muda mfupi. Mara zote watu hawa wamekuwa wakijitambulisha kama wanausalama, hivyo kulitia doa Jeshi. Ingelikuwa busara kwa Jeshi la Polisi kujisafisha kwa kuwashughulikia wenzao wenye tabia hizi ili kuepusha migongano katika jamii. Tabia ya baadhi ya Polisi kukamata raia kama wanakamata kumbikumbi itafsiriwe kuwa jinai na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Ni kwa muda mrefu sasa Watanzania wamekuwa mashakani kutokana na kadhia ya utekaji. Wanasiasa, wasanii na hata wanafunzi wasio na hatia wamekuwa wakitekwa na kupotezwa. Suala hili linaleta utata, kwani mara kadhaa Polisi wamekuwa wakikamata huku wakiwa wamevalia kiraia, hivyo kuwapa urahisi watekaji au watu wasiojulikana (kama wanavyojulikana) kutumia mwanya huo. Watu wasiojulikana wanatumia nguvu kubwa sana wakati wakimkamata raia asiye hata na bakora. Ndo maana nawataka Polisi wabadili mtindo kwani naamini wanaweza.
Polisi wamefunzwa ukamataji wa nguvu ndogo, ya kati na ya juu kulingana na hali iliyopo kwenye tukio. Wanaweza kufanya ukamataji mwepesi usiohusisha nguvu kubwa wala silaha. Wanasimama mbele ya mkamatwaji mtarajiwa, wanajitambulisha na kumwomba mtu huyo kuongozana nao kituoni. Lakini watamwomba baada ya kumtajia tuhuma au sababu za kutakiwa kuongozana nao.
Wale wenzangu na mie kwanza hawavai sare za Jeshi la Polisi. Lakini huwa na kawaida ya kubeba silaha nzito, ikiwezekana za kivita.
Wao hawana namna ya kujitambulisha; unafikiri wataanzaje kukwambia “sisi ni watekaji, ingia garini tukupeleke msituni”? Ni lazima watasingizia kuwa wao ni Polisi.
Sasa hapa ndipo Polisi wanapotakiwa kuonesha tofauti baina yao na watekaji. Polisi ni mtu aliyekwenda chuo kusomea namna ya kumlinda raia na kukabiliana na uhalifu. Hivyo huweza kusoma hisia za mtu mwovu kabla hajamkamata.
Watekaji huwa hawajiamini, kwani hawana elimu wala mbinu za kumdhibiti mtuhumiwa.
Kimbilio lao ni kipigo na kuburuzana. Iwapo hatutabadilika katika kipindi hiki, tutashuhudia kukithiri kwa vurugu kiasi cha kuuharibu uchaguzi mzima.
Baadhi ya vyama vya siasa vinaweza kufanya kila viwezavyo kuwaharibia wapinzani wao, lakini pia kuiangushia Serikali mzigo wa lawama.
Tuwe makini na mtego wa panya. Vurugu za kisiasa zinatuhusu sote tuliomo na tusiokuwamo.
Tusije tukadhani fujo za upande mmoja zitaubakiza upande mwingine salama. Hoja za watawala na wapinzani zisikilizwe kwa usawa na kutolewa majibu. Haina maana kumwomba Mungu huku tukiwachapa virungu watumishi wake!