NIKWAMBIE MAMA: Elimu ya ujuzi ni suluhisho

Karne sita kabla ya kuzaliwa Kristo aliishi mwanafilosofia na mshairi maarufu wa Kichina, Lao Tzu (Laozi au Masta wa kale). Mwanafilosofia huyu alikuwa bingwa wa misemo inayoishi, ukiwemo wa “usinifundishe kula samaki bali nifundishe kuwavua.”

Aliiona dhana ya kujifunza na kutenda mwenyewe ndiyo suluhisho la utumwa. Mtu anayekupa chakula cha leo anakuwa msaidizi wako wa leo tu, usipoangalia kesho utalazimika kumfanyia lolote ili akuwezeshe tena.

Tangu enzi hizo Wachina waliifuata filosofia hiyo hadi wakati wa akina Mwenyekiti Mao walioijenga kama sera ya Kitaifa.

Wachina wote wakakulia kwenye utamaduni wa kujifunza na kutenda kwa tija ya Taifa lao. Tena wengine (kama wa-Tao) waliitukuza kama imani ambapo badala ya watoto kuswagwa kwenda mashuleni au wazazi mashambani, wao walichukulia kwenda shuleni na kazini ni sehemu ya ibada.

Kaulimbiu hii unaweza kuitafsiri kirahisi katika maisha “yetu” pale unapokutana na rafiki anayekulisha “tungi” kila siku bila kukupa siri ya namna anavyozichanga. Usipokuwa makini utajikuta ukimpigia simu asubuhi kumwomba hela ya supu badala ya kujitafutia mahitaji yako mwenyewe.

Mara nyingi wahisani wa aina hii huwa tayari kutoa fedha kwa mabadilishano na kitu muhimu na cha thamani zaidi kwao.

“Usinifundishe kula samaki” ulikuwa ni mwanzo wa siasa ya “Ujamaa na Kujitegemea,” ambayo baba wa Taifa aliizindua hapa nchini mwanzoni mwa miaka ya sitini. Wengi hawakumwelewa, wakadhani ni mbinu yake kujifunika dhidi ya mabavu ya mabepari wa Kimagharibi.

Ile jeuri ya kukataa masharti ya mabeberu na Benki ya Dunia ikaonekana kama iliyopikwa na manguli wajamaa, wakiwemo Warusi na Wachina.

Lakini kumbe hata baadhi ya nchi tajiri zilianzia kwenye ujamaa (kama inavyoonekana China kwa sasa).

Hii inadhihirisha kwamba ujamaa haumaanishi umasikini wala ubepari si utajiri, ni mifumo ya maisha ya kila siku ya mwanadamu. Si kila aishiye pwani ni mvuvi, ndiyo maana masikini wapo hata Ulaya wakati Asia kuna matajiri wanaonunua timu zinazoongoza kwenye ligi pendwa zaidi duniani.

Wengi walishindwa kuona tofauti kati ya ujamaa na umasikini.

Ndiyo maana baadhi ya watu waliposikia kaulimbiu ya “Siasa ni Kilimo” wakala kona. Hata baadhi ya viongozi wenzake wakadhani kuwa kuwapeleka wananchi kwenye vijiji vya ujamaa ni kuwaadabisha wazururaji.

Wakajikuta wakitumia mabavu bila kujua kuwa hapa duniani matajiri wakubwa wa uhakika ni wakulima. Wapo wanaojipiga makonzi kwa majuto leo wanapoziangalia Gezaulole, Mwanalugati na Kibugumo.

Hiyo ndiyo sehemu ya sera ya Ujamaa na Kujitegemea tuliyojifunza kutoka kwa Wachina. Pamoja na kaulimbiu za awamu mbalimbali za uongozi kutofautiana, nchi yetu ingeweza kusimama kwenye Ujamaa na Kujitegemea.

“Uhuru na Kazi” ungetupatia “Ruksa” ya kujiachia na “Maisha Bora” chini ya “Ukweli na Uwazi” ukizingatia “Hapa Kazi tu” na kudumisha “Kazi Iendelee” daima dawamu.

Utaona ya kuwa kilichokuwa tofauti ni jinsi kila awamu ilivyochagua vipaumbele katika uongozi wake, lakini sera mama ya Ujamaa na Kujitegemea ilisimama kama msingi.

Tunaona mfano wa wajasiriamali wa Kichina walivyosambaa duniani wakifanya kazi ambazo hapa kwetu zilishindikana hata viwandani. Hayo ndiyo matunda yao ya kujitegemea baada ya kujifunza, siyo kujifunza kutafuta ajira.

Taifa lolote haliwezi kujua kila kitu. Ili kuepusha kuendelea kuajiri wataalamu wa kigeni mwaka hadi mwaka, mpango wa kubadilishana taaluma na rafiki zetu ungetiliwa mkazo.

Mataifa wanayotoka wataalamu hawa yanahitaji ujuzi wa taaluma zetu, hivyo badala ya kuwalipa mahela mengi tunaweza kubadilishana wataalamu wetu na wao mambo yakaenda kwa wepesi.

Haina haja ya kuibiana taaluma wala kutorosheana wataalamu, ni kuimakinisha sera yetu ya kujitegemea.

Hivi sasa tunao marafiki wengi wataalamu kama India na China kwenye masuala ya afya, teknolojia, ujenzi, uchapaji, usindikaji na kadhalika. Tunaweza kubadilishana wataalamu kwa muda fulani kisha tungeurithi ujuzi tulioupata kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo.

Ingawa hivi sasa tuko vizuri sana kwenye tiba za macho na moyo, lakini vizuri hiyo tunaviongelea Mijini tu. Tungepeleka Hospitali za Rufaa vijijini ambako wananchi ni wengi zaidi.

Elimu haina mipaka wala mwisho. Sisi kama binadamu tumeumbwa tujifunze mpaka siku za miisho yetu, maana hakuna hata mmoja aliyekufa akijua kila kitu.

Nina uhakika hivi leo ukimtaka Mchina wa Kariakoo akutengenezee mbege atakutengenezea kwa mikono yake baada ya muda mfupi tu. Mbona “gongo” wanatengeneza humuhumu uswahilini mwetu, wanaipa majina mazuri na vifungashio vya kupendeza kisha kuitia sokoni!

Maboresho yaliyofanywa kwenye mtalaa wa elimu yaelekezwe kuzalisha wataalamu wazalendo ili kuipandisha nchi kiuchumi. Itakumbukwa kuwa hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na elimu ya ujuzi.

Katika vipindi vilivyopita tulikuwa na elimu kwa vitendo iliyozalisha mafundi, wasanii na wajasiriamali. Lakini kwa sababu zisizoelezeka elimu hii haikudumishwa.

Wakati huu mabadiliko ya kiteknolojia yanafuatana na tatizo la ajira ulimwenguni kote. Ni muhimu kuwaandaa watoto wetu kupitia mtalaa mpya ili wawe tayari kujiajiri.

Inashangaza watu walioishia darasa la nne la mkoloni na la saba baada ya uhuru wakiweza kujiajiri, lakini wa vyuo vikuu vya sasa wakishindwa.