
Katika mkutano wenu hapa nchini, viongozi wa nchi wanachama wa SADC na EAC mmetaka kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo pamoja na kurejeshwa kwa huduma muhimu kama vile maji, chakula, matibabu, elimu na kadhalika. Lakini kama lilivyo sikio la kufa, dalili za kurejea kwa amani zimebaki kuwa kitendawili kisicho na mteguzi hasa ukizingatia jitihada za kundi la M23 kutaka kuitawala Kongo. Hali inazidi kuwa tete kadiri masaa yanavyoyoyoma.
Pamoja na kutajwa na makundi yanayojigamba kwa uharibifu huo kama M23, lakini huwezi kuzungumzia M23 bila kuangazia historia ya jamii ya Watutsi katika eneo la mashairiki mwa Kongo, na ambao pia wako nchini Rwanda. Makundi mbalimbali yalibuniwa ili kutetea maslahi ya jamii ya watutsi katika eneo hilo. Mwaka 2006 CNDP (National Congress for the Defence of the People) iliundwa na viongozi wa Watutsi wa Congo mashariki.
Lakini pia pamoja na hayo, kwa upande wangu bado nawashushia lawama mabeberu wa Kimagharibi hasa nikitazama uwezo mkubwa wa waasi wa Kiafrika.
M23 inamiliki silaha na silaha nzito ailizotumika katika mashambulizi ya hivi majuzi. Vile vile pamoja na idadi yao kuwa kubwa, wapigaji wake wanavalia sare rasmi za kijeshi wakionesha kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha.
Uwezo huu umewezesha M23 kuleta changamoto kubwa kwa Wanajeshi wa DRC na kudhibiti maeneo ya kimkakati ndani ya eneo hilo.
Tangu enzi na enzi mabeberu wa Kimagharibi walikuwa wakimezea mate utajiri wa Afrika na kuitawala kinguvu. Mtindo wao wa kuigawanya na kuitawala Afrika (divide and rule) ulisababisha kuvijenga vikundi vya waasi na kuvifadhili kwa fedha na silaha kali.
Naamini hao ndio chanzo kikubwa cha migogoro barani humu hasa nchini Kongo kwa sasa kwa vile nchi hiyo inamiliki utajiri wa madini.
Mwalimu Nyerere alipata kutahadharisha juu ya migawanyiko ya aina hii na fujo zilizokuwa zikijitokeza. Alisema kuwa Wanyamulenga sio wahamiaji waliokuja Zaire.
Ufalme wa Rwanda uliganywa kati ya Ubelgiji na Ujerumani. Na Ubelgiji ulichukua theluthi mbili ya ufalme wa Rwanda. Tunaposema heshimu mpaka uliowekwa na Ujerumani na Ubelgiji, pia tunapaswa kuwaheshimu watu uliowapokea chini ya mgawanyo.
Nyerere aliongezaongeza kuwa huwezi kugeuka na kusema hawa si raia wa nchi hii. Je utawarejesha peke yao au utawarudisha na kipande chao cha ardhi? Tena huwezi kuwaambia nendeni nyumbani, nyumbani wapi? Katika kujenga hoja yake, Nyerere alitoa mfano wa kabila la Wamasai wa Tanzania na Wamasai wa Kenya na kusema hawawezi kuambiwa warudi Kenya ama Tanzania kwa kuwa nchi yao ya asili iligawanywa katika makoloni mawili ya Waingereza na Wajerumani na baada ya uhuru wamejikuta wapo katika nchi mbili tofauti.
Baadhi ya Mataifa ya Kiafrika kama Kongo, Liberia na mengineyo yalikuwa yakiumizwa na Mataifa makubwa ili kuwatawala kiuchumi. Ile kanuni ya “wagawanye uwatawale” ilitumika na kuwafanya wapoteze utajiri wao.
Ndio unakuta mtu anatoka zake huko, anatumia tofauti zenu kuwakosanisha, kisha anakuja kuwasaidia kumaliza vita. Anaimalizaje vita hiyo na hali ameshapata chimbo la kuiba dhahabu na soko la kuuzia silaha?
Lakini pia vibaraka wa ndani nao ni ishu kubwa. Waswahili tunasema “Mchawi ndugu” kwani ndugu yako ndiye anayejua madhaifu yako.
Hataona dhambi kukuuza kwa watu wabaya naye apate chake. Kwa mfano kukishakuwa na Kongo hii na Kongo ile, basi tegemeeni lolote. Lakini kama zingeshikana na kuwa kitu kimoja kungekuwa na ugumu kuzihujumu.
Mara nyingi tumezoea kuona jinsi Mataifa makubwa ya Ulimwengu wa Kwanza yakifaidika na chumi za Mataifa ya Ulimwengu wa Tatu. Yanaanza na lugha tamu inayoitwa “misaada”, lakini misaada hiyo huwekewa masharti yanayolenga kuwarutubisha.
Moja ya masharti inaweza kuwa ni kupatiwa vitalu nchini mwenu. Lakini pamoja na kufaidika, Mataifa hayo makubwa yamekuwa yakibuni hujuma mbalimbali kama kuwagombanisha wenyeji, kisha kudai kusimamia amani huku yakichota rasilimali.
Bila shaka waasi hawajifunzi kwa yaliyotokea kwa akina Savimbi na Doe. Mabwana wao hawakuwa na rafiki wala adui wa kudumu. Ukiwapelekea mchongo waje kuiba madini nchini kwako watakukumbatia, lakini utamu ukikolea watakuua ili kukunguza matumizi yao.
Hali tete inayoendelea na migogoro iliyopo nchini Kongo, inasababisha madhara makubwa sio kwa Kongo tu bali hata katika nchi za Jumuiya ya Afika ya Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika.
Katina kipindi hiki kigumu Afrika inatakiwa kushikamana kama ilivyoshikamana wakati wa kutafuta uhuru kutoka kwa wakoloni.