Nigeria inayoathiriwa na mafuriko yatafuta suluhisho la kudumu kwa ukosefu wa maji

Ahmad Elnafaty alichimba visima vitano karibu na nyumba yake katika jimbo la Kano kwa kipindi cha miaka minne. Hakuna hata kimoja kilichotoa maji ndani ya muda wa wiki moja. Hatimaye, alikata tamaa.

Kama familia nyingi katika jiji la kibiashara, jamii ya Elnafaty sasa inanunua bidhaa hiyo maji kutoka kwa wafanyabiaswa. Ni gharama inayokawabili kila mwezi ya naira 200,000 (sawa na dola za Marekani 125) ambayo imekuwa kawaida kwa familia nyingi za Nigeria.

“Bahati mbaya sana,” Elnafaty ameiambia TRT Afrika, akimaanisha juhudi zake zilizoshindikana za kupata maji ya kisima.

Kinachomshangaza ni mazingira ya nchi ambapo mito yake hujaa maji kila mara. Mamilioni ya raia kama yeye wanakosa maji kutokana na mifumo mibovu ya usambazaji ambayo ni kama haifanyi kazi.

Matatizo ya maji yamefanya baadhi ya watu kuimarika kiuchumi. Utafiti wa mwaka 2021 uliofanywa na UNICEF na Wizara ya Maji ya Nigeria ulionyesha kuwa kati ya vituo vya usambazaji maji milioni 2.31 kote nchini, asilimia 75 vilikuwa vinamilikiwa na watu binafsi, na asilimia 43 ya vituo hivyo vilikuwa ni visima ilivyochimbwa.

Faida za kuchimba visima

Uhaba wa maji katika nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika umefanya kuwepo kwa wafanyabishara wengi wa uchimbaji visima, wauzaji wa mashine za kuvuta maji na mafundi, na wakati mwingine kufanya watoto kukosa shule.

“Katika jimbo la Kano, visima vya kuchimba kawaida huhitaji kufikia kina cha mita 30 hadi 60 ili kuwa na uhakika wa kupata maji, huku vingine vikifikia hadi mita 250 au zaidi,” mchimbaji Lamir Safiyanu Madugu ameiambia TRT Afrika.

“Kina cha wastani cha visima ni chini ya mita 20, huku kiwango cha juu mara chache kikizidi mita 60.”

Kuchimba visima hugharimu takriban naira 1,050,000 (sawa na dola 658), bila kujumuisha gharama ya mafuta ya pampu ya maji. Wakati wa msimu wa kiangazi, ambapo viwango vya maji hushuka zaidi, Madugu huchimba visima vitano hadi kumi kwa wiki.

Wataalamu na Wanigeria mashuhuri mara kwa mara wameonya kuhusu matatizo kwa mazingira yanayotokana na uchimbaji wa visima bila mpango maalum. Rais mstaafu wa nchi hiyo Olusegun Obasanjo anahofia kuwa kuna janga kubwa linakaribia, akizungumzia kuhusu uchimbaji wa visima kiholela katika mji wake wa Abeokuta, kusini magharibi mwa Nigeria, hivi karibuni.

Kushindwa kwa mfumo

Mbali na wizara ya maji ya taifa, Nigeria ina wizara za maji tofauti katika majimbo yake 36 na mji mkuu Abuja, pamoja na mashirika ya maji ya serikali yanayohusika na kuunda na kuimarisha mifumo ya maji ya umma.

Wizara ya Maji na Usafi wa Mazingira ya ilisema mwezi Mei kuwa serikali ya Nigeria, kwa kushirikiana na baadhi ya mashirika ya kimataifa, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, imekamilisha jumla ya miradi 565 ya maji katika kipindi cha miaka miwili, ikinufaisha zaidi ya Wanigeria 451,000.

Dkt. Zaharaddeen Garba, profesa wa kemia ya mazingira katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello huko Zaria, anasema kuna mengi zaidi yanayohitajika kufanywa na anahusisha tatizo hilo na mchanganyiko wa ukosefu wa miundombinu, ukarabati duni na ukuaji wa haraka wa miji.

“Mabomba yamechakaa, mifumo ya usambazaji haiko thabiti, na uwezo mdogo wa kutbi maji,” ameiambia TRT Afrika. “Sababu nyingine ni ukuaji wa miji na ongezeko la idadi ya watu, ambalo linaweka shinikizo kubwa kwenye mifumo ya usambazaji wa maji iliyopo na kusababisha uhaba na kutokuwepo kwa usawa.”

Mabadiliko ya hali ya hewa yamezidisha changamoto hizi. Uhaba wa mvua husababisha joto jingi, ambalo pia huathiri upatikanaji wa maji.

Uvunaji wa maji ya mafuriko

Wataalamu wanaamini Nigeria inaweza kubadilisha tatizo la mafuriko na kuelekea kupata maji ya kutosha.

“Kutumia mifumo ya kuhifadhi maji ya mafuriko ni njia moja ambayo Nigeria inaweza kutumia uwezo wa vyanzo vya maji vinavyokumbwa na mafuriko ili kuunda vyanzo vya maji safi,” anasema Dkt. Garba.

“Hii inahusisha ujenzi wa mabwawa, madaraja na miundombinu mingine ya kuhifadhi maji ya mafuriko, ambayo yanaweza kutibiwa na kusambazwa. Nigeria pia inaweza kuangazia teknolojia za ubunifu, kama vile mitambo ya matibabu ya maji inayozunguka, ili kutibu na kutumia maji ya mafuriko.”

Kwa kusimamia maji ya mafuriko kwa njia ya busara, Nigeria inaweza kubadilisha tatizo kuwa jambo linalofaa, hivyo kuimarisha upatikanaji wa maji na kusaidia maendeleo ya kiuchumi. Lakini hili linahitaji mipango makini, uwekezaji wa miundombinu, na ushirikiano wa wadau.

“Njia nyingi zinahitajika ili kuhakikisha usambazaji wa maji endelevu. Njia ya kwanza inatakiwa kuwa kuwekeza katika maboresho na upanuzi wa miundombinu, ambayo ni pamoja na ya kisasa, mabomba na mifumo ya usambazaji,” anaeleza Dkt. Garba.

Serikali pia inahitaji kuimarisha usimamizi wa bodi za maji za serikali kupitia ujenzi wa uwezo, matumizi ya teknolojia na uwazi.

“Kukuza mazoea ya uhifadhi wa maji na mikakati ya usimamizi wa mahitaji kunaweza kusaidia kupunguza upotevu na kuimarisha matumizi,” Dkt. Garba anaiambia TRT Afrika.

Uwezekano wa ubinafsishaji

Tangu ubinafsishaji wa mawasiliano ya simu mwaka 1999 ulipochochea ukuaji wa uchumi, wadau wamekuwa wakipendekeza ubinafsishaji kama suluhisho kwa sekta zingine zinazosimamiwa vibaya na serikali.

Lakini wataalamu wanaonya dhidi ya kuchukulia hili kama suluhisho la moja kwa moja.

“Ni kweli kwamba ubinafsishaji wa sekta ya mawasiliano ya simu nchini Nigeria ulileta ustawi mkubwa katika sekta hiyo. Hata hivyo, kutumia mfano huo kwa bodi za maji za serikali si rahisi kama inavyoweza kuonekana. Hili ni jambo tata zaidi,” anasema Dkt. Garba.

Anaamini kuwa ubinafsishaji wa bodi za maji za serikali unaweza kuleta ufanisi, lakini gharama inaweza kuwa kikwazo, hasa kwa kaya zenye kipato cha chini.

Dkt. Garba anapendekeza kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu na utoaji wa huduma, huku taasisi za umma zikibaki na jukumu la usimamizi “ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa njia ya haki na gharama nafuu.”

Watumiaji kama Elnafaty, ambao tayari wananunua maji safi kutoka kwa wauzaji, huenda wasiwe na tatizo kulipia mfumo wa kuaminika zaidi unaohakikisha usambazaji wa mara kwa mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *