Niger yasaini makubaliano ya ushirikiano wa satelaiti 3 na kampuni moja ya Russia

Serikali ya Niger, ikiwakilishwa na Waziri wa Mawasiliano, Sidi Mohamed Raliou, imetia saini makubaliano ya kushirikiana na shirika moja la Russia katika kuendesha satelaiti tatu.

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo imefanyika Niamey mjini mkuu wa Niger ambapo shirika la Glavkosmos ambayo ni kampuni tanzu ya shirika la anga za juu la Russia liitwalo Roscosmos, litaipa Niger satelaiti tatu kwa ajili ya kuimarisha usalama na uwezo wa ulinzi wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Waziri Sidi Muhamed Raliou ametangaza habari hiyo na kusisitiza kuwa, makubaliano hayo yanajumuisha ushirikiano katika uendeshaji wa satelaiti ya mawasiliano, satelaiti ya kutambua vitu kwa mbali na satelaiti ya rada kwa madhumuni ya ulinzi na usalama. Uzalishaji wa satelaiti hizo unatarajiwa kufanyika nchini Russia katika kipindi cha miaka minne ijayo.

“Tumejitolea kuwa huru na kujichukulia wenyewe maamuzi yetu katika uwanja huu,” amesema Waziri Raliou akibainisha kuwa, mradi huo utahusisha pia timu za mafunzo kwa wananchi na raia wa Niger ili waweze kusimamia vizuri vifaa.

Waziri wa Mawasiliano wa Niger ameongeza kuwa, kwa hivi sasa Russia imekubali kuikodisha vifaa kama hivyo Niger hadi satelaiti hizo zitakapokuwa tayari. 

Baada ya mapinduzi ya mwaka jana, Niger imezidi kujitenga na Ufaransa ambaye ni mkoloni wake wa zamani na inaimarisha uhusiano na washirika wengine wa kimataifa kama vile Russia.

Mwezi Septemba mwaka huu pia, Burkina Faso, Mali na Niger zilikubaliana na Russia kupata mawasiliano ya simu na satelaiti za uchunguzi kwa ajili ya maendeleo na ustawi mpana zaidi barani Afrika.