
Ripoti ya Umoja wa Mataifa, inaonesha kuwa Mohamed Bazoum aliyekuwa rais wa Niger, aliyeondolewa madarakani na wanajeshi mwaka 2023, ameendelea kuzuiwa pamoja na mke wake.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Imebainika kuwa, tangu kuondolewa kwake madarakani, Bazoum na mkewe Hadiza wameendelea kuzuiwa katika makaazi ya rais jijini Niamey bila sababu muhimu.
Watalaam wa Umoja wa Mataifa wanasema kuendelea kuzuiwa kwa Bazoum, ni kukiuka haki zake za msingi, na anapaswa kuachiwa huru haraka na mkewe.
Mawakili wa Bazoum nao wamesema, rais huyo wa zamani na mkewe hawana mawasiliano yoyote na watu wa nje wakiwemo watoto wao na ndugu zao wa karibu, baada ya kupokonywa simu zao Oktoba mwaka 2023, baada ya kudaiwa kuwasiliana na maadui wa serikali ya kijeshi.
Bazoum ambaye alichaguliwa mwaka 2021, alipinduliwa na Jenerali Abdourahamane Tiani Julai mwaka 2023, ambaye wakati huo alikuwa ni mkuu wa kikosi maalum cha kumlinda rais, akimtuhumu kiongozi kwa kushindwa kuilinda nchi dhidi ya mashambulio dhidi ya makundi ya kijihadi.