Niger: Raia 44 wauawa katika shambulio la wanajihadi kusini magharibi

Raia 44 waliuawa siku ya Ijumaa, Machi 21, katika shambulio jipya la wanajihadi kusini magharibi mwa Niger, Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya serikali, Télé Sahel.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani, washambuliaji wa Islamic State katika Sahara Kubwa waliwashambulia waumini katika msikiti wakati wa sala ya Ijumaa katika kijiji cha Fambita, katika eneo linaloitwa “mipaka mitatu”. Eneo ambalo limekuwa kimbilio la wanajihadi wa Saheli wanaoshirikiana na Islamic State na Al-Qaeda.

Niger, nchi kubwa ya Sahel inayotawaliwa na utawala wa kijeshi, kwa mara nyingine tena imekumbwa na mashambulizi makali ya wanajihadi, ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 44 kusini magharibi mwa nchi hiyo.

“Siku ya Ijumaa, Machi 21, kijiji cha Fambita, katika wilaya ya vijijini ya Kokorou, kililengwa na mashambulizi ya kikatili ya magaidi kutoka Islamic State katika Sahara (IS), ambao walilenga msikiti, kulingana na chanzo hicho. Wizara ya Mambo ya Ndani imesema shambulio hilo limeua “mashujaa 44, wote raia, 13 wamejeruhiwa, wanne kati yao wakiwa katika hali vibaya” na Setikali ya Niger inatangaza maombolezo ya kitaifa ya saa 72 kuanzia Jumamosi.

“Karibu saa 8 mchana, wakati waumini wa Kiislamu walipokuwa wakiswali swala ya Ijumaa, magaidi hao waliokuwa na silaha nzito waliuzingira msikiti huo kutekeleza mauaji yao ya kikatili,” wizara hiyo imesema, na kuongeza kuwa washambuliaji pia “walichoma moto soko na nyumba wakati walipokuwa wakirejea nyuma.”

“Idadi ya muda ni ya mashujaa 44, wote ni raia, 13 waliojeruhiwa, wanne kati yao wamejeruhiwa vibaya na wanatibiwa,” taarifa hiyo imeongeza. “Uhalifu huu wa kutisha utapaswa kuadhibiwa, wahalifu, wahusika wenza, wafadhili na washirika watasakwa na kufikishwa mbele ya mahakama zinazohusika ili kujibu makosa yao,” imebainisha wizara hiyo ambayo pia imetangaza maombolezo ya saa sabini na mbili kote nchini, kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu.

Mashambulizi yanaendelea licha ya ahadi za utawala wa kijeshi

Niger mara kwa mara inakabiliwa na mashambulizi kutoka kwa makundi ya wanajihadi kama vile Boko Haram na tawi lake lililojitenga, IS katika Afrika Magharibi, kusini mashariki mwa nchi. Fambita, kwa upande mwingine, iko kusini-magharibi, katika idara ya Téra ya eneo la Tillabéri, kwa upana zaidi katika eneo linaloitwa “mipaka mitatu”, kwenye mipaka ya Niger, Mali na Burkina Faso: eneo ambalo limekuwa kimbilio la wanajihadi wa Sahel wanaohusishwa na Islamic State na Al-Qaeda.

Niger inatawaliwa na utawala wa kijeshi ambao ulichukua mamlaka katika mapinduzi ya Julai 2023, na kumpindua Rais mteule Mohamed Bazoum, ambaye inamshikilia. Utawala wa kijeshi umeahidi kukabiliana na ukosefu wa usalama. Hata hivyo, mashambulizi yanaendelea: tangu mwezi 2023, angalau watu 2,400 wameuawa nchini humo, kulingana na shirikalisilo la kiserikali la Acled, ambalo linarekodi waathirika wa migogoro duniani kote.

Niger, kama majirani zake Mali na Burkina Faso, imekuwa ikikabiliwa na ghasia hizi kwa takriban miaka kumi. Baada ya kuvunja ushirikiano wao wa kijeshi na Ufaransa, nchi hizi tatu za Sahel zikiongozwa na tawala za kijeshi ziliungana ndani ya shirikisho la Muungano wa Nchi za Sahel (AES) Walitangaza kuunda kikosi kijacho cha wanajeshi 5,000 ili kupambana na wanajihadi, huku operesheni za pamoja zikiwa tayari zinatekelezwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *