Niger: Mazungumzo ya kitaifa kufanyika kuanzia Februari 15 hadi 19

Miezi kumi na minane baada ya kuingia madarakani, Jenerali Tiani alitia saini agizo mwishoni mwa juma hili la kutaka kuitishwe mazungumzo ya kitaifa kuanzia Februari 15 hadi 19 nchini Niger. Wajumbe wasiopungua 674 waliochaguliwa na wanajeshi watagawanywa katika tume tano ili kufafanua kinachohitajika kufanyika. Watakaokosekana ni wawakilishi wa vyama vya siasa ambao bado wamesimamishwa.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Agizo hilo lililotiwa saini siku ya Jumamosi, Februari 8 na Jenerali Tiani, ambapo anaitisha mikutano ya kitaifa kati ya Februari 15 na 19 nchini Niger, pia inatoa fursa ya kuundwa kwa tume ya kuisimamia zoezi hilo. Hii itaongozwa na chifu wa kimila, Mamoudou Harouna Djingarey, ambaye atakuwa na kibarua kigumu cha kuongoza mijadala hiyo. Ataandamana na makamu wa rais ambaye ni Kanali-Meja Maman Souley, Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Ulinzi. Atakuwa mwanajeshi pekee katika ofisi hiyo, ambayo pia inajumuisha watu binafsi na wanachama wa mashirika ya kiraia wanaounga mkono utawala wa kijeshi ulio madarakani huko Niamey.

Hii ndiyo kesi, kwa mfano, ya Ibrahim Assane Mayaki, Waziri Mkuu chini ya utawala wa Rais Ibrahim Baré Mainassara, mwishoni mwa miaka ya 1990, au ya Abdoulaye Seyni, mwanachama wa Umoja wa Kulinda Ukuu na Utu wa Watu, muungano wa mashirika ya kiraia yanayojulikana zaidi chini ya jina la M62.

Kuweka muda wa Mpito

Wakati watu kadhaa wanasema walishangazwa kujua kuhusu uteuzi wao kwenye televisheni bila kushauriwa kabla, hakuna hata mmoja wao aliye katika mojawapo ya vyama 172 vya kisiasa vilivyoorodheshwa nchini Niger. Kwa vile vyama hivi bado wamesimamishwa na utawala wa kijeshi, hakuna wawakilishi wao hata mmoja aliyealikwa kwenye vikao hivi, ambavyo shughuli zao zitafanyika ndani ya kamati ndogo tano zinazoitwa “Uchumi na Maendeleo Endelevu”, “Mageuzi ya Kisiasa na kitaasisi” au “Haki na Haki za Binadamu”.

Wajumbe hao watakuwa na kazi ya kutoa rasimu ya awali ya Mkataba wa Mpito ambapo watalazimika kutunga mapendekezo. Hati inaweza hasa kuwezesha kujifunza zaidi kuhusu muda wa Mpito. Alipochukua mamlaka mwezi Julai 2023, Jenerali Tiani – ambaye anatarajia ripoti ya mwisho ya mkutano huu mkuu kuwa imefika ofisini mwake mwanzoni mwa mwezi Machi – alidokeza kwamba muda wa Mpito unaweza kudumu kwa miaka mitatu. Bunge pia litalazimika kuamua kama ataweza kuwania au la katika chaguzi zijazo.