Nicolás Maduro: Kiongozi ambaye ameapa kushinda uchaguzi ‘kwa njia yoyote ile’

Venezuela's President and presidential candidate Nicolas Maduro attends presidential election rally ahead of upcoming election in Caracas, Venezuela on July 18, 2024

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Author, Vanessa Buschschlüter
  • Nafasi, Mhariri wa Latin America na Caribbean , BBC News Online

Rais Nicolás Maduro alipopanda jukwaani tarehe 4 Februari mwaka huu kuadhimisha kumbukumbu ya mapinduzi yaliyoshindwa ya mtangulizi wake, Hugo Chávez, matamshi yake yalikuwa na makali sana.

Tarehe nne ya Februari ni siku ambayo wafuasi wa Chavismo, vuguvugu la kisiasa lililoundwa na marehemu Chávez, wanasherehekea mwanzo wake mnamo 1992.

Akizungumza na umati wa watu waaminifu wa Chavista waliovalia fulana zao nyekundu za kitamaduni, aliwataka waonyeshe “mishipa ya chuma” kabla ya uchaguzi wa rais wa Julai.

Venezuelan President Nicolás Maduro speaks with government supporters during an event commemorating the anniversary of the failed 1992 coup d'état led by late President Hugo Chavez, at the Miraflores presidential palace in Caracas , Venezuela, on Sunday. February 4, 2024

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo tarehe 4 Februari, Nicolas Maduro alisema chama chake kitashinda “kwa hali yoyote”

Alikuwa na sababu nzuri ya kufanya hivyo. Oktoba iliyopita, Wavenezuela milioni 2.4 walipiga kura zao katika mchujo ulioandaliwa na muungano wa vyama vya upinzani.

María Corina Machado alishinda kwa 93% ya kura.

Bi Machado tangu wakati huo amekuwa mpinzani mkubwa wa Bw Maduro, akiyafanya yale ambayo watu wengine hawakuyapata kabla yake – kuunganisha upinzani wa Venezuela uliogawanyika nyuma ya kiongozi mmoja.

Katika kipindi cha miaka 11 madarakani, Bw Maduro ameweza kuupiku upinzani mara kwa mara, akisaidiwa na ukweli kwamba mara nyingi viongozi wa upinzani walionekana kutumia muda mwingi kushambuliana badala ya kuzingatia kumpiga.

Na labda ni woga huo ambao ulimfanya Bw Maduro asitabiri tu ushindi katika uchaguzi ujao – jambo ambalo wagombea wengi hufanya – lakini kuongeza kwamba angeshinda “hata kwa hila”.

Kwa wanaharakati wa upinzani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kuwa wahanga wa unyanyasaji wa serikali, matamshi ya rais hayakuwa ya kushangaza.

Lakini hata hivyo ni kuteleza ulimi kutoka kwa kiongozi wa vuguvugu ambalo linapenda kujionyesha kuwa linawakilisha Wavenezuela wengi , ambao unadai kuwa uungwaji mkono wao wa dhati, umeipatia ushindi katika chaguzi nyingi na kuiweka madarakani bila usumbufu tangu wakati huo 1999.

Si mara ya kwanza kwa maneno ya Bw Maduro kuibua hisia.

Wapinzani wa Bw Maduro kwa muda mrefu wamemdhihaki kwa matusi yake na mwanzo wake ‘wa chini’ kama dereva wa basi.

Lakini kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 ametumia maisha yake ya zamani kujinufaisha, akikuza sura yake kama “mtu wa watu”, akicheza salsa na mkewe wakati wa vipindi vyake vya runinga na hajawahi kukosa hafla ya kupiga besiboli, kurusha mpira wa vikapu au kuigiza pigano katika mchezo wa ndondi

Venezuelan President Nicolas Maduro (R) dances with his wife Cilia Flores during a demonstration against the United States' decision to renew sanctions on several top Venezuelan officials, in Caracas on March 12, 2016.

Chanzo cha picha, Getty

Na ingawa hakuwahi kupata umaarufu miongoni mwa Wachavista ambao mtangulizi wake Hugo Chávez alikuwa nao, hadi sasa ameweza kubaki kiongozi asiyepingwa wa vuguvugu hilo.

Hili lilikuwa tofauti na hapo awali alipochaguliwa na Hugo Chávez mnamo 2012 kama mrithi wake baada ya kugunduliwa na saratani.

Wengi walidhani Chávez angemchagua Diosdado Cabello, mwanajeshi mkali na mpambanaji, kwa nafasi ya kaimu rais wakati kiongozi huyo mgonjwa alipokuwa akipokea matibabu nchini Cuba.

Lakini badala yake Chávez alimteua Bw Maduro, ambaye alikuwa amemtaja kuwa makamu wa rais baada ya kuhudumu kwa miaka sita kama waziri wa mambo ya nje wa Chávez.

Kufuatia kifo cha Chávez mnamo Machi 2013, Bw Maduro alishinda uchaguzi ambao ulifuatia kifo cha rais , na kumshinda mgombea wa upinzani Henrique Capriles kwa asilimia 1.6 – matokeo ambayo Bw Capriles aliyapinga.

Mnamo 2018, Bw Maduro alishinda kwa kura nyingi katika uchaguzi ambao ulipuuzwa kuwa haukuwa huru na wa haki.

Muungano mkuu wa upinzani uliamua kususia uchaguzi baada ya kundi la wagombea kukamatwa au kutoroka nchini, na kuacha uwanja ukiwa tupu kwa Bw Maduro peke yake.

Yamkini, mojawapo ya mafanikio makuu ya Bw Maduro ni jinsi ambavyo ameweza kwa muda wa miaka 11 iliyopita sio tu kuzuia pingamizi zozote za utawala wake ndani ya chama chake cha PSUV, bali pia kuunda ushirikiano wenye nguvu na wale ambao wamemuunga mkono.

Waziri wake wa ulinzi, Vladimir Padrino, amekuwa katika wadhifa huo kwa takriban muongo mmoja, akihakikisha kwamba vikosi vya jeshi vinasalia nyuma yake.

Msaada wa vikosi vya jeshi ulikuwa muhimu wakati kiongozi wa Bunge la Kitaifa lililodhibitiwa na upinzani, Juan Guaidó, alijitangaza kuwa rais halali mnamo Januari 2019, akisema kwamba kuchaguliwa tena kwa Bw Maduro mnamo 2018 kulifanyika kwa udanganyifu.

Matumaini ya upinzani kwamba Bw Guaidó angechukua nafasi ya Bw Maduro katika ikulu ya rais yalikatizwa baadaye , huku taasisi zote kuu zikisalia chini ya udhibiti thabiti wa serikali.

Washirika wa Bw Maduro pia wanadhibiti shirika kuu la uchaguzi, Mahakama ya Juu na ofisi ya Mwanasheria Mkuu, miongoni mwa zingine.

Akiwa na shaka na watu wa nje, anajizunguka na kundi la wanasiasa wanaoaminika, ambao huwazungusha kupitia nyadhifa tofauti za juu.

Miongoni mwao ni Delcy Rodríguez, ambaye amewahi kuwa waziri wake wa mawasiliano, waziri wake wa mambo ya nje na hivi karibuni, kama makamu wake wa rais.

Nicolas Maduro, Venezuela's president, right, speaks to members of the media, next to First Lady Cilia Flores, center, and Delcy Rodriguez, Venezuela's vice president, left, after casting a ballot during a referendum vote in Caracas, Venezuela, on Sunday, Dec. 3, 2023.

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Delcy Rodríguez (kushoto) amekuwa mmoja wa washirika wa karibu wa Bw Maduro na mkewe Cilia Flores (katikati)

Kakake Jorge ni mshirika mwingine wa karibu wa Maduro, ambaye kwa sasa anaongoza Bunge la Kitaifa linalodhibitiwa na serikali.

Bw Maduro na baadhi ya watu wake wa ndani – akiwemo waziri wake wa ulinzi – wameunganishwa zaidi kwa kushtakiwa na mamlaka ya Marekani mwaka wa 2020 kwa “ugaidi wa mihadarati” na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Rais alitumia hati ya mashtaka kujionyesha kama mpiganaji dhidi ya “majeshi ya kibeberu ya Marekani”, ambayo anadai yanamlenga kwa sababu “anasimama kutetea haki ya watu wake”.

Pia analaumu vikwazo vya Marekani kwa mzozo mbaya wa kiuchumi ambao Venezuela imekumbwa nao chini ya uongozi wake.

Takriban Wavenezuela milioni nane wameondoka nchini humo katika muongo mmoja uliopita, wakisukumwa na mchanganyiko wa uhaba ulioenea wa bidhaa muhimu na kuongezeka kwa ukandamizaji wa kisiasa.

Ili kukomesha kudorora kwa uchumi, mnamo 2019 Bw Maduro alilegeza baadhi ya kanuni kali za fedha za kigeni zilizoletwa na Chávez.

Uhaba umepungua tangu wakati huo, lakini wale wasio na fedha za kigeni wanaendelea kuhangaika.

Kura za maoni zinaonyesha umaarufu wa Bw Maduro umeshuka kwa miaka mingi, kwa sehemu kubwa kwa sababu ya kuzorota kwa uchumi ambao amekuwa akisimamia.

Walakini, chama chake cha kisoshalisti cha PSUV bado kinaweza kutumia idadi kubwa ya wafuasi, pamoja na idadi kubwa ya watu ambao wamefaidika kifedha kutokana na utawala wake ili kusalia madarakani.

Supporters of President of Venezuela Nicolas Maduro attend a rally ahead of the presidential election on July 18, 2024 in Caracas, Venezuela.

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Chama cha Maduro cha PSUV kina wafuasi sugu waliojitolea

Hatua za serikali yake katika miezi ya hivi karibuni, hata hivyo, zinaonekana kusaliti wasiwasi wake kwamba chama chake chenye nguvu kinaweza kukosa kushinda uchaguzi ikiwa kura itakuwa huru na ya haki.

Kwanza, mtawala mkuu, mshirika wa serikali, alimpiga marufuku mpinzani wake mkuu, María Corina Machado, kugombea wadhifa huo – uamuzi ambao ulithibitishwa baadaye na Mahakama Kuu inayodhibitiwa na serikali.

Kisha, mwanamke ambaye muungano wa upinzani ulikuwa umemchagua kuchukua nafasi yake kwenye kura alizuiwa kujiandikisha.

Hatimaye, mwanadiplomasia wa zamani asiyejulikana, Edmundo González, alithibitishwa kuwa mgombea wa muungano wa upinzani mwezi Aprili.

Bw González amempita Bw Maduro katika kura za maoni katika muda mfupi, huku baadhi wakimpa kiongozi huyo wa miaka 74 uongozi wa 40% kuliko rais.

Kwa kujibu, matamshi ya Bw Maduro yamekuwa ya kivita zaidi, hata kuibua hatari ya “vita vya wenyewe kwa wenyewe” ikiwa atashindwa.

“Ikiwa hamtaki umwagaji damu nchini Venezuela, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoletwa na mafashisti, basi tujitahidi kupata mafanikio makubwa zaidi, ushindi mkubwa zaidi katika historia ya uchaguzi wa watu wetu,” aliwaambia wapiga kura chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi.

Kuchochea umwagaji damu kunaweza kuonekana kuwa mbaya, lakini Bw Maduro ana mengi ya kupoteza, iwapo atashindwa kwenye uchaguzi.

Sio tu kwamba Marekani imetoa zawadi ya $15m (£11.6m) kwa kukamatwa kwake kwa mashtaka ya “ugaidi wa mihadarati”, lakini pia anachunguzwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama wakati wa kukandamiza wimbi la maandamano dhidi ya serikali mwaka 2017.

Hakuna mtu anayepaswa kushangaa ikiwa, atashindwa katika uchaguzi, dereva huyo wa zamani wa basi atakataa kukubali na kwamba amefika mwisho .

Wengi wanaogopa hatakubali kuondoka kimya kimya.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah