Marekani. Kutana na Nick Cannon ambaye ni Rapa na DJ nchini Marekani, mwamba ni baba wa watoto 12 akiwa amezaa na wanawake sita tofauti kwa kipindi cha miaka 12 tangu alipojaliwa watoto wake wa kwanza pacha na aliyekuwa mkewe, Mariah Carey.
Cannon, 44, aliliambia jarida la People kuwa watoto ndio furaha ya maisha yake, anafurahishwa sana na watoto wake kwa kila wanachofanya na kila siku kuamka tu akiwa baba, hiyo ni furaha tosha.
Akizungumza katika Podcast ya The Language of Love na Dk. Laura Berman, Cannon alisema kila mwanamke ambaye ana mtoto naye, hakika kulikuwa na mazungumzo ya mshangao ni jinsi gani ujauzito ulipatikana na namna mtoto atakavyokuwa.

“Ninahisi kila mwanamke niliyezaa naye ni mama wa ajabu ama wa kipekee, kila mwanaume anatakiwa kuwa na mama wa aina hiyo ambaye anatamani watoto na kuwa mama wa mfano,” alisema Cannon.
Na hawa ni wanawake sita na watoto wao waliojaliwa na Nick Cannon ambaye jicho lake halichoki kuangazia warembo kutoka kiwanda cha muziki, milamu na mitindo kwa miaka zaidi 10 sasa.
1. Mariah Carey (2)
Mwimbaji Mariah Carey ni mama watoto wao pacha, Monroe na Morocco Scott waliozaliwa Apili 2011, Mariah na Cannon walifunga ndoa mwaka 2008 na kudumu hadi mwaka 2016 walipoachana kwa talaka.
Katika mahojiano na jarida la Us Weekly, Februari 2018, Cannon alisema mtoto wao, Morocco ni mtundu sana wa teknolojia kiasi kwamba amebadilisha nywila (password) za barua pepe zake zote.
Julai 2022 kwenye kipindi, Hot Tee Talk Show, Cannon alieleza ingawa hayupo na Mariah wanashirikiana vizuri kulea watoto na bado ana upendo kwake na kila wakati ataendelea kumpenda mwimbaji huyo wa kibao maarufu, We Belong Together (2005).
2. Brittany Bell (3)
Huyu ni Mwanamitindo na aliwahi kuwa Miss Arizona U.S.A, Brittany Bell amejaliwa watoto watatu na Cannon, Golden Sagon aliyezaliwa Februari 2017, Powerful Queen aliyezaliwa Desemba 2020 na Rise Messiah aliyezaliwa September 2022.
“Bell amekuwa mwamba na msingi wa safari yangu ya Ubaba. Amenifundisha mengi kuhusu uzazi, saikolojia, kiroho, upendo na maisha ya haki kwa ujumla,” alisema Cannon.
Mwaka mmoja baada ya kuzaliwa mtoto wao, Powerful Queen, Cannon alisema ni mtoto mzuri na akatania kwamba jina lake lingine analoweza kumpa lilikuwa “Genius Empress”.

3. LaNisha Cole (1)
Mrembo huyu ni Mpiga Picha, LaNisha Cole amezaa mtoto mmoja wa kike na Nick Cannon, Onxy Ice Cole ambaye alizaliwa Septemba 2022 na Cannon kutumia Instagram kutoa ujumbe kumuhusu.
“Ninaahidi kumpenda msichana huyu mdogo kwa moyo wangu wote, bila kujali mtu yeyote anasema nini. Nimeacha kujaribu kujieleza kwa ulimwengu au jamii na badala yake ninafanya kazi na kumtumainia Mungu asiye na mwisho,” alisema Cannon.

4. Abby De La Rosa (3)
Ni DJ na Mtangazaji maarufu wa Redio. Abby De La Rosa na Nick Cannon wana watoto pacha, Zion Mixolydian na Zillion Heir waliozaliwa Juni 2021, pia kuna Zeppelin Cannon aliyezaliwa Novemba 2022.
Kwenye siku ya kuzaliwa pacha hao, De La Rosa aliwapa heshima kwenye Instagram, aliandika kwamba walimpa kusudi la kuishi na ni moyo wake katika umbo la kibinadamu.
Pia alitumia ujumbe kwa Cannon akisema; “Ulimwengu unaweza kusema kile wanachotaka lakini wewe una upendo wa juu na zaidi kwa ajili yetu na kwa hilo tunakushukuru milele”.
5. Alyssa Scott (2)
Huyu ni Mwanamitindo, Alyssa Scott na Cannon walijaliwa mtoto wa kiume, Zen hapo Juni 2021 lakini alifariki baada ya miezi mitano baada ya kugunduliwa na saratani ya ubongo.
Siku ambayo ingekuwa ni ya kuzaliwa kwa Zen, Alyssa Scott aliandika ujumbe Instagram akimtakia heri ya kuzaliwa manaye.
“Heri ya siku ya kuzaliwa Zen, katika hisia zote nilizonazo leo kuna upendo usioweza kushindwa. Mimi hujaribu kila niwezavyo kubaki na mtazamo chanya ila kwa sasa siwezi kujizuia kulia, haifai kuwa hivi” alisema.
“Akilini mwangu naweza kukuona ukikata keki, ukivuta miguu yangu, lakini ukweli ni kwamba mimi ndiye nitazima mshumaa wako wa kwanza, natamani angekuwa hapa” alieleza Scott.
Novemba 2022 wawili hao walitangaza wanatarajia mtoto mwingine ambaye ndiye wa 12 kwa Cannon, na Desemba 2022 wakaweka wazi kujaliwa mtoto wa kike waliyempa jina la Halo Marie Cannon.

6. Bre Tiesi (1)
Mrembo huyu ni wakala wa mali isiyohamishika na Mwanamitindo, aliigiza msimu wa sita wa ‘Selling Sunset’, Bre Tiesi na Cannon wana mtoto mmoja, Legendary Love aliyezaliwa Juni 2022.
Januari 2022 ndipo Cannon alifichua kwamba alikuwa anatarajia mtoto na Bre Tiesi, aliliambia gazeti la E! Daily Pop kwamba yeye na mwigizaji huyo wa ‘Wild ‘N Out’ wamekuwa wapenzi kwa miaka.
Bre Tiesi aliweka video YouTube yenye urefu wa dakika 11 ukionyesha kuzaliwa kwa Legendary Love ambapo Cannon anaonekana akiwa amemshika mtoto wake mchanga. “Hey, Legendary,” baba huyu alitamka kabla ya kubadilisha nepi ya mtoto huyo.