Ni madudu, ufanisi ripoti za CAG, Takukuru

Dar es Salaam. Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mwaka 2023/24 zimeonyesha mafanikio katika baadhi ya sekta, lakini pia zimebaini changamoto kadhaa, zikiwemo kasoro katika usimamizi wa fedha za umma.

Ripoti hizo, zilizowasilishwa leo Machi 27, 2025, kwa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam, zimeangazia ufanisi pamoja na mapungufu katika taasisi na mashirika ya umma, miradi ya maendeleo, serikali za mitaa na Serikali Kuu.

CAG Charles Kichere amewasilisha ripoti mbalimbali za ukaguzi ya mwaka 2023/24 kuhusu hesabu za fedha, ukaguzi wa ufanisi, ukaguzi maalumu na wa kiuchunguzi, mifumo ya Tehama na kaguzi za kiufundi.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila kwa upande wake amewasilisha ripoti ya utendaji kazi wa taasisi yake kwa mwaka 2023/24, akiangazia kazi ilizofanya na kufanikisha kuokoa mabilioni ya shilingi ambayo yangepotea.

Mbali na Rais Samia, hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu na Profesa Ibrahim Juma.

Ufanisi waongezeka

Akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi, CAG Kichere amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, asilimia 99.5 ya hati alizozitoa ni safi na hivyo akieleza mwenendo wa hati hizo ukiridhisha.

“Mwenendo wa hati za ukaguzi katika mwaka wa fedha 2023/2024, nimetoa jumla ya hati 1,301, ikiwa ni ongezeko la hati 92 ikilinganishwa na hati 1,209 zilizotolewa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Kati ya hizo, hati zinazoridhisha ni 1,295 (asilimia 99.5), hati zenye shaka ni tano (asilimia 0.4), hati mbaya ni moja, sawa na asilimia 0.1 na hakukuwa hati iliyoshindwa kutolewa maoni.

“Kwa ujumla hati za ukaguzi wa hesabu zinaonyesha kuwa utayarishaji wa hesabu unaridhisha na unaimarika. Na kwa kiasi kikubwa unazingatia taratibu na kanuni za uandaaji za hesabu za kimataifa,” amesema Kichere.

Kwa upande wake Chalamila, amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Transparency, Tanzania ni nchi ya pili kuwa na kiwango cha chini zaidi cha vitendo vya rushwa kati nchi 10 wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Amesema Transparency kupitia kiashiria cha CPI ilitoa taarifa hiyo Februari 11, 2025 ambapo kwa mwaka 2024, Tanzania ilipata alama 41 kwa 100 na kushika nafasi ya 82 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti.

“Kwa mujibu wa kipimo hicho, Tanzania imeendelea kuimarika katika kupunguza rushwa kwa wastani mzuri. Tanzania imepanda na miongoni mwa nchi nne za Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye kuimarika katika kupambana na vitendo vya rushwa.

Hatua zimechukuliwa

Mara baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Rais Samia amesema ukaguzi uliofanyika unatoa taswira ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuziimarisha taasisi za umma ili ziweze kutumia rasilimali za umma vizuri.

“Faraja tuliyoipata ni kwamba kumekuwa na kuongezeka kwa ufanisi katika matumizi ya rasilimali za Serikali. Pamoja na upungufu uliotajwa hapa, kumekuwa na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za Serikali.

“Hiyo ni faraja yetu kama Serikali, kwamba tumeweza kukuza uwazi na uwajibikaji na hatimaye kuleta utawala bora, tunaendelea kuleta utawala bora ndani ya Serikali,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wa Takukuru, amesema taarifa imeashiria kuongezeka kwa ufanisi wa aina mbili; kwanza, ufanisi ndani ya taasisi yenyewe hasa kwa kuboresha taarifa zake na kuongezeka kwa ufanisi katika taasisi za umma.

“Ufanisi katika matumizi ya mifumo na Tehama, kwamba kwa kiasi fulani sasa Tehama inatumika ndani ya Serikali na taasisi zetu, lakini na mifumo iliyowekwa nayo inafuatwa na kwa kiasi kikubwa kupunguza zile kasoro zilizokuwa zikijitokea huko nyuma,” amesema.

Rais Samia amesema Serikali itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti za Takukuru na CAG na kwamba watafuatilia maoni ya wabunge wakijadili ripoti hizo ili wayafanyie kazi.

“Sisi upande wa Serikali tuko tayari kuendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizi mbili, tutasikiliza vizuri, tutafuatilia vizuri mjadala wa Bunge kwenye taarifa ya CAG na Takukuru.

“Tutakwenda kufanyia kazi vizuri yale yote ambayo yameelezwa, ili hatimaye tuweze kujenga utawala bora ndani ya nchi yetu,” amesisitiza Rais Samia.

Hasara TRC, ATCL, TTCL

Pamoja na mafanikio ya upande mmoja, , CAG Kichere amebainisha kasoro kwenye mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2023/24, kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imepata hasara ya Sh91.8 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka hasara ya Sh56.6 bilioni mwaka uliotangulia.

CAG Kichere amesema hasara hiyo inatokana na gharama kubwa za matengenezo ya ndege na hitilafu za injini, hasa ndege za Airbus zilizokaa muda mrefu bila kufanya kazi zikisubiri injini.

“Pia kampuni ilitumia Sh99.8 bilioni ikiwa ni ruzuku kutoka serikalini, endapo isingekuwa ruzuku hiyo, kampuni ingepata hasara halisi ya Sh191.6 bilioni,” amesema.

Amependekeza ATCL ishirikiane na Serikali katika kufanya utafiti wa njia bora zaidi za uendeshaji wa ndege kwa kuzingatia masuala ya kifedha na kiuchumi ili kuongeza ufanisi wa uendeshaji.

Kwa upande wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kichere amesema lilipata hasara ya Sh27.7 bilioni mwaka wa fedha wa 2023/2024. Ongezeko hili ni kutoka Sh4.32 bilioni ya hasara kwa mwaka uliopita.

Hasara hii ya mwaka huu inachangiwa na ongezeko la gharama baada ya kuhamishiwa Mkongo wa Taifa na Kituo cha Taifa cha Data.

“Licha ya kukusanya mapato Sh24 bilioni kutoka kwenye mkongo, fedha hizo hazikuhesabiwa kama mapato ya TTCL bali zilitumika kulipia deni la mkongo, hivyo shirika limeendelea kupata hasara,” amesema.

Amependekeza deni la mkongo wa taifa lilipwe na taifa na mapato yanayopatikana yatumike kuendesha shirika kiufanisi.

Aidha, amesema Shirika la Posta Tanzania lilipata hasara ya Sh23.6 bilioni ambayo ilichangiwa na kushuka mapato kwa asilimia 20.

Kwa upande wa shirika la Reli Tanzania (TRC), Kichere amesema mwaka wa fedha 2023/2024, shirika hilo lilipata ongezeko la asilimia 100 la hasara hadi Sh224 bilioni ikilinganishwa na Sh102 bilioni mwaka uliopita.

CAG Kichere amesema hasara hiyo imechangiwa na kupungua kwa mapato ya usafirishaji kutokana na uhaba wa vichwa vya treni na mabehewa pamoja na mvua kubwa iliyosababishwa kufungwa kwa njia kwa miezi minne.

“Shirika lilitumia Sh29 bilioni ikiwa ni ruzuku kutoka serikalini, kama ruzuku hilo isingetolewa shirika lingepata hasara ya Sh253 bilioni,” amesema CAG.

Kichere amesema taarifa hiyo haihusu mapato ya SGR kwa sababu taarifa inaishia Juni 30, 2024 ambapo treni ilikuwa haijaanza kufanya kazi.

Amependekeza shirika lijikite katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wake pamoja na kutekeleza hatua za kupunguza gharama na mpango wa kina kupata injini na mabehewa, ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.

IPTL yaidai Tanesco

CAG Kichere amebainisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linadaiwa Sh238.7 bilioni na kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Amesema deni hilo linajumuisha deni halisi Sh111.4 bilioni na riba ya Sh127.2 bilioni.

Amesema pamoja na mgogoro kuhusu kutohuishwa kwa leseni ya IPTL kati ya mwaka 2017 hadi 2022, kampuni hiyo imewasilisha madai mengine mengi ya fidia, gharama za uzalishaji na ada za kisheria huku Tanesco ikidai mgogoro huo ulishatatuliwa kupitia kesi namba 200 ya mwaka 2015

“Kwa upande mwingine hadi Juni 2024, IPTL ilikuwa haijarejesha Dola za Marekani 148 milioni, sawa na Sh389.8 bilioni zinazodaiwa na Serikali tangu Februari 2022 zilizotokana na makubaliano kuhusu fedha za Tegeta Escrow,” amesema.

“Napendekeza Serikali ifanye tathmini kamili ya madai yote ya madeni yanayohusiana na kampuni ya IPTL ili kubaini uhalali wake, usahihi wake na utekekelezaji wa makubaliano ya kisheria, pia Serikali irejeshe pesa inazodai IPTL Dola za Marekani 148 milioni, kwa kuzingatia mkataba wa makubaliano wa mwaka 2021 kuhusu fedha za Tegeta Escrow.”

Makusanyo serikali za mitaa

Akizungumzia ukaguzi kwenye mamlaka za serikali za mitaa, Kichere amesema mamlaka 14 zilitarajiwa kukusanya Sh45.6 bilioni kutoka kwa wakala wa mapato lakini zimekusanya Sh19.4 bilioni zikiwa ni upungufu wa Sh26.1 bilioni.

Amesema upungufu mkubwa ulionekana kwenye halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lililopanga kukusanya Sh15 bilioni lakini likakusanya Sh3.4 bilioni. Kinondoni ilipanga kukusanya Sh10.2 lakini ikakusanya Sh5 bilioni.

“Halmashauri ya Ubungo ilipanga kukusanya Sh3.1 bilioni lakini ikakusanya Sh909 milioni. Mwanza ilipanga kukusanya Sh3.6 bilioni lakini ikakusanya Sh1.6 bilioni.

Amesema Halmashauri ya Kibondo ilipanga kukusanya Sh2.1 bilioni lakini ikakusanya Sh635 milioni huku Halmashauri ya Babati iliyopanga kukusanya Sh2.5 bilioni ikikusanya Sh1.4 bilioni.

‘Kampuni ya nguzo ivunjwe’

Katika hatua nyingine, CAG Kichere ameshauri kampuni ya kutengeneza nguzo za zege nchini Tanzania ivunjwe baada ya kushindwa kufanikisha majukumu yake tangu kuanzishwa kwake.

Amependekeza kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ivunjwe na badala yake, shughuli zake zifanywe na idara ndani ya Tanesco.

Kichere amesema fedha nyingi zinatumika kulipa gharama za kawaida na kwa wazabuni wa nje wanaotengeneza nguzo, badala ya kampuni hiyo kutekeleza jukumu lake.

“Kwa zaidi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, bado haijaanzisha uzalishaji wa nguzo wala kuwa na maabara yake ya ndani, hali inayoiweka katika utegemezi wa huduma kutoka nje,” amesema.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuzalisha na kupima ubora wa nguzo za umeme huku katika mwaka wa fedha 2023/2024, ilipokea Sh6 bilioni kutoka Tanesco, ambapo Sh4 bilioni zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda na maabara ya kupima ubora wa nguzo.

“Sh2 bilioni zilielekezwa kwenye gharama za uendeshaji. Licha ya hivyo, fedha nyingi zilitumika kulipa gharama za kawaida na wazabuni wa nje wanaotengeneza nguzo badala ya kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake,” amesema Kichere.

Watumishi wadai mabilioni

Ripoti hiyo imebainisha watumishi wa umma wanadai Sh311.9 bilioni katika taasisi 269 za Serikali. Amesema fedha hizo zinahusisha mishahara, gharama za usafirishaji kwa wastaafu na marupurupu ya kisheria.

“Serikali Kuu inadaiwa Sh274.8 bilioni, mamlaka ya serikali za mitaa Sh24.5 bilioni na mashirika ya umma Sh12.6 bilioni,” amesema.

Kichere amependekeza Serikali kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Hazina kuhakikisha fedha zinatengwa kwa wakati kulipa madeni hayo kuepuka malimbikizo.

Deni Machinga Complex

CAG Kichere amebainisha pia kwamba mkopo wa Sh15.9 bilioni uliotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka 2007 kwa ajili ya ujenzi wa Machinga Complex iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam umelipwa Sh80 milioni.

Aidha, amesema mkopo huo haukufuata masharti ya mkataba ikiwemo upatikanaji dhamana ya Serikali na hatimiliki ya ardhi.

Mkaguzi huyo amesema hadi kufikia Juni 2024, mkopo na riba umefikia Sh27.6 bilioni lakini tangu mwaka 2009 halmashauri imerejesha Sh80 milioni.

Hati mbaya, zenye shaka

Kichere ameyataja mashirika manne ya umma yaliyopata hati zenye shaka na hati mbaya katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2023/24.

Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na kiwanda cha dawa cha Keko Pharmacetical kinachozalisha dawa na vifaatiba mbalimbali, zikiwemo barakoa.

“Taasisi zilizopata hati zenye shaka na hati mbaya ni pamoja na Kiwanda cha Dawa Keko, Bodi ya Chai Tanzania, Chuo cha Sukari cha Taifa na Shirika la Posta Tanzania, haya ni mashirika ya umma,” amesema Kichere.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, amezitaja Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, Mfuko wa Afya kuwa zimepata hati mbaya.

Vivuko 32 si salama

CAG Kichere katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2023/24, amesema imebaini vivuko 32 vinavyomilikiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) havikidhi matakwa ya kiusalama majini.

Amesema vivuko hivyo havikukidhi matakwa ikiwemo kutokuwa na vyeti vya usalama majini na baadhi havikusajiliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).

“Kutokuwa na vyeti vya usalama majini maana yake havijakidhi vigezo vya kiusalama vinavyotakiwa kwa vyombo vya majini ili viweze kusafiri bila matatizo,” amesema Kichere.

Katika ripoti maalumu ya uchunguzi ya Mei 2024, Mwananchi lilifichua kwamba usalama wa zaidi ya watu 60,000 wanaotumia vivuko vya Kigamboni-Magogoni uko shakani kutokana na ubovu na ukosefu wa matengenezo ya kisheria na kitaalamu kwa vivuko hivyo.

Hata hivyo, Januari 23, 2025, Azam Marine Limited ilizindua vivuko viwili vya mwendokasi vitakavyotoa huduma katika eneo la Magogoni-Kivukoni, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano kati yake na Temesa.

Takukuru yaokoa mabilioni

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Takukuru, Chalamila amesema kwa mwaka 2023/24 taasisi iliokoa Sh30.1 bilioni kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi.

“Baadhi ya chunguzi zilizofanikisha uokoaji huo, mosi ni mikopo isiyorejeshwa kwenye Benki ya Maendeleo (TIB) ya Sh6.6 bilion,i iliyotolewa bila kuzingatia utaratibu na vigezo kwa kampuni ya Amboni Sisal Properties Ltd ya Tanga fedha hii tayari imerudishwa TIB.

“Pili, ushuru uliokusanywa kwenye maeneo ya minada masoko na maeneo mengine Halmashauri ya Ilala kiasi cha Sh6.8 bilioni, wakusanyaji hawakuwasilisha fedha hizo benki na sasa zimerudishwa kwenye akaunti ya mfuko mkuu wa halmashauri ya jiji.

Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri, Sh3.1 bilioni kati ya fedha hizo, Sh1.1 bilioni (fedha taslimu) zilirejeshwa kwenye akaunti za halmashari na Sh2 bilioni zilidhibitiwa sambamba na vifaa kurejeshwa kwenye miradi husika.

“Nne ni ukwepaji wa kodi Sh2.4 bilioni, kati ya fedha hiyo Sh281.4 milioni zilikuwa za kodi iliyokwepwa kulipwa na wafanyabiashra mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma.

Amesema pia taasisi imeokoa Sh2.1 bilioni zilizotokana na ukwepwaji wa kodi ya zuio.

Imeandikwa na Peter Elias, Sute Kamwelwe na Harieth Makwett

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *