
Dar es Salaam. Ingawa uamuzi wa Marekani kusitisha misaada ya nje ni maumivu kwa mataifa mbalimbali, hatua hiyo pia inatazamwa kama hatma ya nafasi ya taifa hilo la Magharibi katika kuitawala dunia.
Tangu aapishwe kuwa Rais wa Marekani Januari mwaka huu, Donald Trump ameshasaini nyaraka takribani 79 zikiwamo za kusitisha misaada katika mataifa mbalimbali duniani, kadhalika michango yake katika mashirika ya kimataifa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi na sera yake ya kuirejesha hadhi ya Marekani ‘Make America Geat Again’ ambayo kwa mujibu wa wanazuoni wa siasa za kimataifa, inahatarisha nafasi ya taifa hilo katika kuitawala dunia.
Lakini wapo wanaoona kinachofanywa na Marekani ni mbinu ya kuuthibitishia ulimwengu ukubwa wake, ili hatimaye mataifa yakaipigie magoti.
Wachambuzi wengine wa masuala ya siasa, wamekwenda mbali zaidi na kueleza tangu kitambo Marekani ilishapoteza nafasi ya kuwa kiranja wa dunia, hasa kwa sababu imeshindwa kudhibiti machafuko mashariki ya kati na imebaki kuhubiri maslahi binafsi.
Inapoteza heshima yake
Akizungumzia hilo, Mwanazuoni wa Siasa za Afrika, Ezekiel Kamwaga anasema ukubwa na utawala wa Marekani katika Dunia ulitegemea nguvu za aina mbili ilizonazo.
Nguvu hizo kwa mujibu wa Kamwaga, ni za kijeshi zilizoliwezesha taifa hilo kutuma vikosi vyake kwa ajili ya kutuliza ghasia katika mataifa mbalimbali.
Kwa upande mwingine, anasema taifa hilo lina nguvu ya uchumi iliyoliwezesha kuwa na mashirika lukuki yanayotoa misaada kwenye mataifa na jumuiya mbalimbali duniani.
Yote hayo, Kamwaga anasema ndiyo yaliyoitambulisha, kuiheshimisha na hata kuifanya Marekani iwe rafiki wa wengi, kadhalika mtawala wa dunia.
Hatua zinazofanywa sasa na taifa hilo, anasema zinaiondolea Marekani sifa, nguvu na heshima iliyonayo kwa mataifa mengi na kwamba inabaki na hadhi ya utajiri.
Hilo linatokana na kile alichoeleza, waliokuwa washirika wa taifa hilo hawatashawishika tena kuiheshimu Marekani, kwa sababu hawana wanachokipata kutoka kwake.
“Unapoondoa Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) unaondoa nguvu iliyokuwa inakusaidia kuendelea kuaminika na kupendwa,” anaeleza Kamwaga.
Anakwenda mbali zaidi na kueleza ililazimika mataifa mbalimbali kuiamini Marekani kwa kuwa ilikuwa msaada kwa matibabu ya mamilioni ya wagonjwa waliosumbuliwa na maradhi mbalimbali.
“Kwa sasa Marekani hataaminika tena. Kwa sehemu kubwa anaharibu asili na utawala wake aliokuwa nao kwa zaidi ya miaka 80,” anaeleza.
Marekani haiepukiki
Hata hivyo, mtazamo wa Kamwaga unatofauti na wa Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo aliyesema kuna umuhimu wa kujua Marekani ilikuwaje kinara wa dunia.
Anasema hadhi iliyonayo Marekani sasa, ilijengwa kwa namna ilivyoshiriki mwishoni mwa vita ya kwanza na ya pili ya dunia.
Nguvu nyingine, anasema inatokana na uimara wake katika masuala ya kiulinzi na kijeshi na sio kutoa misaada kama wengi wanavyodhani.
Ili Marekani ikome kuwa kiongozi wa dunia, Dk Masabo anasema lazima iache kutegemewa na nchi nyingine katika masuala ya ulinzi kwa maana ya kutuma vikosi vyake na vifaa.
“Hadi sasa tunavyoongea ni nchi tatu pekee ndizo zilizotengeneza ndege za kivita, ambazo ni Marekani Urusi na China,” anasema mwanazuoni huyo.
Kwa sababu ya uhalisia huo, anafafanua nchi za Ulaya hazina namna zinayoweza kufanya, ili kuacha kuwa tegemezi kwa Marekani, hasa kwa masuala ya kiulinzi.
Dk Masabo anakwenda mbali zaidi na kusema ni nchi zinazoendelea pekee ndizo zinazotegemea misaada ya kuishi leo na kesho kwa Marekani, wengine wanategemea ulinzi.
Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, mashirika makubwa ya kifedha na kiraia ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), yalianzishwa kwa falsafa za kimarekani na yanalitegemea taifa hilo kwa michango.
Anaeleza China kwa sera zake, haiku tayari kubeba jukumu lililokuwa linabebwa na Marekani kwa sababu taifa hilo halitaki kuwekeza kwenye vita.
“Ukiondoa vita dhidi ya Vietnum, wenyewe kwa wenyewe na dhidi ya Japan, China haikuwahi kupigana vita nyingine yoyote, kwa hiyo haipendi vita,” anasema.
Lakini kwa Marekani, Dk Masabo anasema inapenda vita kwa sababu inajenga uchumi kupitia hali hiyo, kwa kuuza silaha.
“Kwenye vita, Marekani ananufaika kwa kuuza silaha, kwa hiyo anajiona ana faida kwenye hilo. Leo hii watu wakitishika watanunua silaha kujiimarisha,” anasema.
Kama ilivyo kwa China, anasema Urusi nayo haina nia ya kuwa mtawala wa dunia na hata mashambulizi yake dhidi ya Ukraine yanalenga kuifanya nchi hiyo isitawalike.
Anasema Marekani itaondoka katika nguvu ya kuitawala dunia kwa muktadha wa kidiplomasia na haki za kibinadamu, lakini inaendelea kuwa na nguvu kwa sababu ya jeshi, hivyo itabaki kuwa mtawala.
Inathibitisha ukubwa, itaumia baadaye
Mwanahabari mkongwe anayeishi nje ya Tanzania, Ansbert Ngurumo anasema kinachofanywa na Rais wa Marekani, Donald Trump kinalenga kuthibitisha kuwa taifa hilo lina sauti na uwezo wa kufanya na kuharibu inachotaka.
Kila mbinu zinazofanywa na Trump kwa sasa, Ngurumo anasema zinaweka msisitizo wa kuonyesha ukubwa wa Marekani na kwamba ndilo taifa kiranja.
“Hapa anawathibitishia wapiga kura wake kwamba Marekani ina sauti kubwa na uwezo wa kufanya na kuharibu inachotaka na kwamba, inathibitisha yenyewe ni kiranja na ndio maana inapofanya hivyo watu wanalia,” anasema.
Ingawa uamuzi uliochukuliwa ni mgumu, Ngurumo anasema unawafurahisha na kuwanufaisha Wamarekani kwa kuwa unaokoa fedha nyingi za walipakodi zilizokuwa zikienda kufanya kazi nyingine katika miradi ya watu wengine.
“Kwa kuwa Trump ni mfanyabiashara, tafsiri ya maisha kwake ni fedha, kwa hiyo kila kitu zikiwamo siasa zake anazifanya kifedha fedha,” anasema Ngurumo.
Anasema kinachofanywa sasa na Marekani, ndiyo kinaliongezea nguvu zaidi taifa hilo ya kuheshimika na kujenga ushawishi kwa wapiga kura na ulimwenguni kwa ujumla.
“Anayatikisa mataifa mengine ili yampigie magoti, anataka wakubaliane ili atoe kidogo kuliko anachotoa sasa kama mchango wake na mataifa mengine, yaongeze kiwango cha kutoa kwa sababu anaona taifa lake linanyonywa,” anasema.
Hata hivyo, Ngurumo anasema kinachofanywa na Trump kinaitengenezea Marekani maadui wengi wa baadaye, jambo litakaloliathiri taifa hilo.
“Walioijenga Marekani kuwa taifa linalotoa misaada walilenga kuihusisha na siasa za Dunia. Anachokifanya Trump ni kinyume na dhamira hiyo, kweli kwa sasa kitainufaisha Marekani na yeye binafsi atajenga ushawishi kwa Wamarekani, lakini anajenga uadui na dunia na athari zake zitaonekana baadaye,” anasema Ngurumo.
Marekani imepoteza sifa
Hoja ya Ngurumo ni tofauti na iliyotolewa na Mchambuzi wa Siasa za Kimataifa, Ibrahim Rabhi anayesema Marekani ikishajiondoa kitambo kwenye nafasi ya kuiongoza dunia.
Kilichobaki katika taifa hilo kwa mujibu wa Rabhi, ni nguvu ya mabavu inayoiamanisha dunia tangu muda mrefu.
Anasema taifa hilo limeondoka katika nafasi hiyo kwa sababu limekosa sifa ya kuwa kiongozi, kutokana na mizozo inayoendelea mashariki ya kati, hatua yake ya kuweka vikwazo vya mara kwa mara, mambo ambayo hayatarajiwi kwa kiongozi.
Mchambuzi huyo anaeleza kwa sasa Marekani imeamua kuvua ngozi iliyokuwa inajificha nayo muda mrefu ya kunadi demokrasia, uhuru na haki, badala yake inanadi maslahi yake binafsi.
“Kwa kufanya hiki inachoendelea kufanya inatoa nafasi kubwa kwa mataifa mengine yanayotafuta nafasi ya kuiongoza dunia yapenye kuwa na nafasi hiyo,” anasema.
Hata hivyo, anasema hatua hiyo itaiathiri na Marekani pia kwa kukosa washirika muhimu iliyokuwa nao awali.
“Mfano kwa sasa Umoja wa Ulaya inawaza usalama wao kwa ajili yao na sio kufikiria usalama wao juu ya mgongo wa Marekani, yote haya ni kwa sababu tayari Marekani si kiranja tena,” anasema.