Ni dabi ya kwanza kwa Hamisa na Jux

Dar es Salaam. Hatimaye ile siku imefika na haina kipengele ambapo wababe wa soka la Tanzania, Yanga SC na Simba SC wanakutana katika dabi ya Kariakoo itakayopigwa Dimba la Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara 2024/25.  

Dabi hii inavuta hisia za mashabiki wengi Afrika na kuacha kumbukumbu nyingi lakini itakuwa ya kwanza kwa baadhi ya mastaa wa muziki, mitindo na filamu Bongo wanaoshabikia soka tangu kutokea tukio muhimu maishani mwao kama ifuatavyo.

Hamisa Mobetto & Aziz Ki

Akiwa maarufu katika mitindo na muziki, Hamisa Mobetto alihamia Yanga kama shabiki akitokea Simba, huko alimfuta mpenzi wake, Stephane Aziz Ki ambaye Februari 16 walifunga ndoa na kufuatiwa na sherehe kubwa na ya aina yake.

Hii itakuwa ni dabi ya kwanza tangu wawili hao kufunga ndoa, bila shaka kiu ya Aziz Ki itakuwa ni kuisaidia timu yake kupata ushindi ambao utakuwa pia zawadi kwa mkewe ambaye amekuwa akimuunga mkono katika kazi yake hiyo tangu wamejuana.

Vilevile itakuwa ni dabi ya kwanza tangu Hamisa alipohamia Yanga rasmi hapo Agosti 4, 2024 na kupokelewa na Aziz Ki kwa kuvalishwa jezi ya timu katika tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi, kitendo kilichoacha mijadala mingi.

Kabla ya hapo, Hamisa, Miss XXL After School Bash 2010 alikuwa shabiki wa kutupwa wa Simba, utakumbukwa kwa kuleta kombe uwanjani katika fainali ya Simba Super Cup 2021, shindano liloshirikisha timu kama Al Hilal na TP Mazembe.

Iwapo Hamisa atajitokeza uwanjani katika dabi hii, hii ndio itakuwa mara ya kwanza kufanya hivyo akiwa kama shabiki wa Yanga, timu ambayo inasaka taji lake la 31 la Ligi Kuu Bara ili kuzidi kuikoleza rekodi yake ya kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi kwa muda wote.  

Kama Hamisa aliweza kumsindikiza Aziz Ki katika tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)  2023/24, basi pia anaweza kuja katika dabi kumshangilia mumewe kama ilivyokuwa katika tuzo hizo ambapo alishinda tatu.

Jux & Priscilla

Hii ni mara ya kwanza Jux anashuhudia Yanga yake katika dabi ya Kariakoo akiwa na mwali ndani baada ya hapo Februari 8 kufunga ndoa na mpenzi wake kutokea Nigeria, Priscilla ambaye waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024.

Utakumbuka Jux alishatoa wimbo, Shugga Daddy Yanga (2023) kwa ajili ya timu yake hiyo huku mwaka juzi akitumbuiza katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, tamasha linaloandaliwa na Yanga kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wa msimu mpya.

Kwa vile mastaa wengi wa muziki na hata filamu huenda uwanjani katika mechi kubwa kama hii dabi, huenda naye Jux akaongozana na mkewe kushuhudia chama lake ambapo itakuwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo.

Hata hivyo, bado haijafahamika ikiwa Priscilla naye anaishabikia timu ya mumewe maana hajawahi kuonekana akiwa amevalia jezi ya Yanga au kuhudhuria mechi zake.

Priscilla, binti wa mkongwe wa Nollywood, Iyabo Ojo, tangu amekuwa na uhusiano na Jux ukurasa wake wa Instagram amezidi kupata mashabiki wengi kutoka Tanzania na ikiwa atajihusisha moja kwa moja na Yanga, basi ni wazi atazidi kupata wafuasi wengi.

Utakumbuka katika wimbo wa Jux, Ololufe Mi (2024) ambao katika video yake kaonekana Priscilla, katika vesi ya pili ambayo ameimba Diamond Platnumz ameitaja Yanga, timu ambayo anaishabiki baada ya kuondoka Simba kama shabiki.