
Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeeleza matokeo ya utafiti wake kwamba asilimia 40 hadi 45 ya wanaume nchini wana dalili za upungufu wa nguvu za kiume.
Utafiti uliofanywa na BMH umeelezwa kwa waandishi wa habari leo Jumanne Machi 4, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Profesa Abel Makubi wakati akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita na mwelekeo wa hospitali hiyo.
Profesa Makubi ametoa takwimu hizo kuelezea ukubwa wa tatizo la nguvu za kiume linavyolikabili Taifa na kwamba, waliofanyiwa utafiti wameonyesha dalili hizo kwa viwango tofauti ambavyo ni hatua ya kwanza, ya pili na ya tatu ambayo ni tatizo kubwa.
“Tatizo ni kubwa na tafiti zetu zinaonyesha takribani ya wanaume asilimia 40 hadi 45 wana-some point (wanadalili) ya matatizo hayo,”amesema.
Huduma upandikizaji kwenye hospitali hiyo ilianzishwa Juni 2023, gharama yake ikiwa ni kati ya Sh6 milioni hadi Sh10 milioni, tofauti na nje ya nchi, inatozwa hadi Sh50 milioni; na hadi sasa wamepandikiza wanaume watano.
Kuanza kwa huduma hiyo BMH, kuliamsha hisia za watu wengi wenye tatizo la nguvu za kiume kutaka kufanyiwa upandikizaji, hata hivyo si wote wenye tatizo hilo wanahitaji upandikizaji.
Gazeti hili liliwahi kumnukuu Dk Anna Sarra wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akisema miongoni mwa maradhi yanayosababisha changamoto ya kupungua kwa nguvu za kiume ni kisukari, shinikizo la damu, uti wa mgongo na kuharibika kwa mishipa kutokana na upasuaji.
Pia, gazeti hili kwa mara kadhaa limewahi kuripoti kuongezeka kwa mahitaji ya dawa za kuongeza nguvu za kiume zikiwamo za kienyeji hasa kwa vijana.
Akizungumza leo Jumanne Machi 4, 2025 Profesa Makubi amesema, pia utafiti wao mbali na kubaini ukubwa wa tatizo, wengi wenye tatizo hilo ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 45 na miongoni mwa sababu ni magonjwa ya kuambukizwa na yasiyoambukizwa.
Utafiti wa BMH umekuja ikiwa imepita miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipowaagiza watafiti nchini kufanya utafiti wa kina kubaini chanzo cha tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume linalotesa vijana ambao ni nguvu ya Taifa.
Akizungumza Oktoba 3, 2022, Rais Samia amesema msingi wa tatizo hilo unaanzia kwenye lishe, huku akiwapa kazi watafiti wafanye kazi kuwasaidia vijana wawe mashababi ili wazae watoto wenye afya kwa ajili ya kulitumikia Taifa lao.
Hata hivyo, Profesa Makubi ameelezea namna wanavyofanya kutibu tatizo hilo akisema wanatumia vipandikizi maalumu kwenye uume kwa wanaume watano wenye changamoto za nguvu za kiume, tangu waanze kutoa huduma hiyo.
“BMH imefanikiwa kuweka vipandikizi kwa wanaume watano ambao walikuwa changamoto za upungufu wa nguvu za kiume, BMH ikiwa ni hospitali ya kwanza kutoa hii huduma hapa nchini,” amesema Profesa Makubi.
Amesema watu wote waliopatiwa huduma hiyo wanaendelea vizuri na hawajapata wenye changamoto yoyote.
Hata hivyo, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka BMH, Remigius Rugakingira amesema miongoni mwa sababu za upungufu wa nguvu za kiume ni msongo wa mawazo.
“Mara nyingi mtu akiwa na msongo wa mawazo anaweza kusababisha kupoteza nguvu za kiume. Mambo ya familia ya kila siku yanaweza kusababisha. Kwa hiyo tunaweza kusema mambo ya nje na ndani ya mwili. Homoni za kiume zikipungua zinaweza kusababisha nguvu za kiume kupungua,” amesema Dk Rugakingira.
Amesema chanzo kingine cha kupungua kwa nguvu za kiume ni mfumo wa maisha unaotokana na vyakula visivyo na virutubisho kamili, ukosefu wa mazoezi na kadri umri unavyoongezeka.
Dk Rugakingira anazitaja nyingine ni kuzidi kwa majukumu, magonjwa sugu ikiwamo kisukari, shinikizo la damu lisilodhibitiwa na unywaji wa dawa kiholela.
Amesema matibabu ya nguvu za kiume yanategemea kisababishi, kwa mgonjwa hufanyiwa vipimo kufahamu chanzo na kisha kufanyiwa matibabu.
“Kupandikizwa vipandikizi katika uume ni stage ya tatu, mtu ameshindwa kusimamisha kabisa, hivyo tutakuwekea vipandikizi katika uume ambavyo vitakusaidia kuufanya kuwa imara na kuweze kufurahia na kupata mtoto,” amesema Dk Rugangira.
Amesema wanaopandikizwa vipandikizi ni wale waliovunjika uume, walioumia mgongo na kukata mishipa ya fahamu na waliougua kisukari na kusababisha uume kushindwa kufanya kazi.
Amesema kati ya watu 20, wanane wanakuwa wazi kwa kueleza kuwa wakifanya tendo la ndoa mara moja hawawezi kuendelea lakini wakishafanyiwa wanaweza kwenda watakavyo.
Gharama za kupandikiza
Profesa Makubi amesema kulingana ukubwa, wangetamani kuwafanyia upandikizaji vipandikizi maalumu kwenye uume (Penile Implantation), lakini shida inakuwa ni gharama kubwa na wananchi wengi wanashindwa kuzimudu.
Hata hivyo, Profesa Makubi amesema Serikali inachofanya sasa ni kuona jinsi ya kupunguza gharama kwa kuhudumia vifaa, hivyo mgonjwa kugharamia kiasi kidogo cha fedha.
Vijana ‘kujibusti’
Uchunguzi wa siku kadhaa uliowahi kufanywa na Mwananchi, ulibaini matumizi ya dawa zinazotibu magonjwa mbalimbali kutumika kwa wenye matatizo ya nguvu za kiume kwa kile wanachokieleza ‘kujibusti.’
Mwananchi imefanya uchunguzi kuzunguka maduka mbalimbali ya dawa jijini Dar es Salaam na kubaini uwepo wa dawa hizo, huku wauzaji wakieleza biashara hiyo kwa sasa imechangamka.
Wataalamu wa dawa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamekiri dawa hizo zinatumika kuongeza nguvu za kiume, ingawa kusudio la awali la kutengenezwa kwake, lilikuwa kutibu watu wenye presha ya mapafu na wanaopanda milima mirefu lakini hawajajiandaa.
Wamesema hata dawa hizo zinapohitajika kutumika kwa ajili ya kuongeza nguvu, hilo linapaswa kufanywa kwa mujibu wa maelekezo ya daktari na sio kiholela kama wanavyofanya vijana hao.
Muuzaji wa dawa hizo katika duka moja lililopo Tabata Shule, Joyce Helina amesema watumiaji wa dawa hizo ni vijana, ingawa hata wazee wenye matatizo kama ya kisukari na presha nao wanatumia kwa kiasi.
“Katika duka langu hili kwa siku naweza kuwauzia vijana kuanzia saba hadi 10 na wengi unakuta ni wageni wa hapa, huwezi kuwajua lakini kusema ukweli dawa hizi zinanunuliwa zaidi,” amesema Helina.
Muuzaji mwingine, Juma Mustafa amesema ubora wa dawa wanazouza, inategemeana na aina ya kampuni.
“Tunauza ingawa Viagra inanunuliwa zaidi kutokana na bei yake kuwa chini, wateja ni wengi unajua kipindi cha nyuma tulizoea kupata wazee wenye matatizo ya presha, kisukari lakini kwa sasa vijana ni wengi,”amesema Mustafa.
Amesema vijana wanapokwenda dukani huwa wanapewa ushauri wa namna nzuri ya kuzitumia dawa hizo, huku akieleza kwa kawaida kwa mwezi wanatakiwa kutumia mara moja.
“Changamoto kijana akifika kununua dawa hii haji tena anakwenda sehemu nyingine anaogopa kujulikana, kesho anakwenda kununua duka lingine,” amesema Mustafa.