Dar es Salaam. Katikati ya wiki hii liliibuka sakata la Miss Tanzania 2023, Tracy Nabukeera kutangaza hatoshiriki Miss World 2025.
Ujumbe wa kujitoa aliuchapisha kupitia ukurasa wake wa Instagram, akidai hatoshiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa kampuni inayosimamia mashindano ya urembo nchini.

Hata hivyo jumbe za watu juu ya taarifa hiyo zilionesha kuibua hisia mbalimbali kwa wapenzi na urembo nchini, huku kila mmoja akiongea lake. Na wengine wakidai huenda waandaaji wa mashindano hayo wanaelekea kushindwa.
Kutokana na hisia hizo mchanganyiko za watu ni ishara tosha kuwa bado Watanzania wana kiu kubwa ya kuona warembo wa Tanzania wanafika mbali katika upande wa sanaa hiyo licha ya kuwa vinaibuka vikwazo kila kukicha.
Ikumbukwe mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 huku Theresia Shayo akiwa mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo, kisha yalisimama kwa muda mrefu na kurejea 1994 ambapo mshindi alikuwa Aina Maeda.
Hata hivyo wapo waliofuatia kama vile Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basilla Mwanukuzi (1998) ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Look inayoendesha mashindano ya Miss Tanzania na akafuatia Hoyce Temu (1999) ambaye kwa sasa ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Mashirika ya Kimataifa Geneva Uswisi.

Baada ya kupita warembo hao walifuata wengine kama vile Jacqueline Ntuyabaliwe (2000), Millen Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumari (2005), Wema Sepetu (2006), Richa Adhia (2007), Nasreen Karim (2008), Miriam Gerald (2009), Genevieve Emmanuel (2010), Salha Israel (2011), Brigette Alfred (2012), Happiness Watimanywa (2013).
Haikuishia hapo, wengine waliofuata ni Lilian Kamazima (2014), Diana Edward (2016), Queen Elizabeth Makune (2018), Silvia Sebastian (2019), Rose Manfere (2020), Halima Kopwe (2022) na Tracy Nabukeera (2023).
Katika orodha ya warembo hao inaonesha ipo miaka ambayo shindano hilo halikufanyika na hapo ndipo linapozalishwa swali na baadhi ya wadau kuwa huenda unakaribia mwisho wa Miss Tanzania kwani hata kasi yake na ukubwa wa majina ya washindi wake hayasikiki na kufanya vizuri kama ilivyokuwa zamani.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Look inayoendesha mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, Basilla Mwanukuzi ameeleza sababu ya shindano hilo kutofanyika katika baadhi ya miaka.
“Miss Tanzania ni tamasha ambalo linapangwa kufanyika kila mwaka, lakini pia inategemea na majira na nyakati. Pia Miss Tanzania tunapeleka mshindi Miss World kwa hiyo wanaporukaruka na sisi huwa inatuathiri. Miss World waliruka karibia miaka mitatu.

“Sisi ratiba yetu tunashiriki kwa lengo la kwenda kwenye mshindano ya dunia huwa tunaangalia lini tufanye mashindano ya Miss Tanzania. Kwahiyo ilibidi tusogeze mbele, kwa mwaka jana yalifanyika mashindano lakini fainali tunaifanya mwaka huu,” anasema Basilla.
Licha ya mpangilio wa ratiba hizo za kampuni inayosimamia mashindano hayo ni wazi kuwa nguvu kubwa na ya ziada inahitajika ili kuiinua Miss Tanzania ili ijijengee heshima kama ilivyo katika sanaa nyingine nchini.
Serikali ni wakati sasa wa kuishika mkono na kutia nguvu kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika aina nyingine za sanaa nchini. Dunia nzima inatambua sanaa ni ajira hivyo hata urembo ni ajira kubwa kwa mabinti ikizingatiwa wengi wao baada ya kutoka kwenye mashindao hayo hujikita katika kurudisha kwa jamii.
Mashindano hayo kubaki kwa kampuni bado ni donda ndugu. Serikali ni wakati wa kuweka mipango mikakati ya kulibeba jambo hili liwe la Kitaifa kwani ni njia moja wapo ya kutoa fursa ya kipekee kwa nchi yetu kujulikana kimataifa.
Washindi wanawakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa kama Miss World, wanapata nafasi ya kuonyesha utamaduni, vivutio vya utalii, na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Mfano mzuri ni Nancy Sumari, ambaye alishinda taji la Miss Tanzania mwaka 2005 na kisha kushika nafasi ya sita bora katika Miss World, akifahamika kama Miss World Africa.
Hata hivyo nguvu kubwa katika mashindano haitaishia tu kuwa fursa bali ni sehemu ya kuhamasisha wanawake kuwa wajasiri hasa katika kushiriki kuonesha vipaji walivyonavyo.
Mbali na hayo, washindi wa Miss Tanzania mara nyingi hutumika kama mabalozi wa kampeni za kijamii, wakishiriki katika shughuli za kijamii kama vile kupambana na umasikini, lishe bora, na usawa wa kijinsia. Hii inasaidia kuhamasisha jamii kuhusu masuala muhimu na kuchangia katika maendeleo ya kijamii.
Hivyo basi umakini wa hali ya juu unatakiwa katika kulilinda shindano hili ili lisipotee au kuanguka kabisa kwa uzembe wa watu wachache.