Ngumi taifa wanawake kambini

MABONDIA 16 wa timu ya Taifa ya ngumi, wameingia kambini jana Jumapili tayari kwa maandalizi ya ushiriki wa mashindano ya Ubingwa wa Dunia kwa Wanawake yatakayofanyika katika Jiji la Nis, Serbia Machi 8-16 mwaka huu.

Kambi ya timu hiyo iliyoanza jana saa 3 asubuhi na itakayokuwa chini ya makocha watatu, daktari mmoja na mwamuzi mmoja imewekwa katika Apartment zilizopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga makocha watakaokinoa kikosi hicho ni; Samwel Kapungu ambaye ndiye kocha mkuu, akisaidiwa na Kassim Hussein na Fatuma Manzi, huku mwamuzi akiwa ni Baraka Lusato kwa nia ya kufundisha sheria za mchezo wa ngumi na Dk Mussa Maira ndiye daktari wa timu.

Makore aliwataja mabondia wanaounda timu hiyo, uzito na klabu wanazotoka katika mabano ni; Veronika Thomas (Kg 48, MMJKT), Latifa Said (Kg 50, JKT), Sarafina Fusi (Kg 50, Ngome), Zulfa Macho (Kg 52, Ngome), Tatiana Ezekiel (Kg 54, Zugo) na Martha Patrick (Kg 54, Ngome).

Wengine ni mabondia wa uzito wa Kg 57 ambao ni, Vumilia Kalinga (Ngome), Zawadi Amos (MMJKT) na Halima Vunjabei (Nakozi), Doricas Daudi (Kg 60, Kamwe), Zulfa Iddi (Kg 60, Zogo) na Najma Isike (Kg 63, Taifa).

Pia wamo Consolata Laizer (Kg 66, Polisi Arusha), Salma Michael (Kg 75, Mwanza na mabondia wa uzito wa juu wa Kg 81, Rachel Msingo kutoka Dodoma na Mariam Msabila wa Klabu ya Kinyogoli.

Kwa mujibu wa Makore, mabondia 12 ndio watakaoteuliwa kwa ajili ya safari ya kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya ubingwa wa dunia.