
Dar es Salaam. Mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 20, Ivory Coast imejivua uenyeji wa mashindano hayo.
Nchi hiyo imefanya uamuzi huo mgumu kwa kile ilichokisema ni kutokuwa na uwezekano wa kumudu gharama za kuyaandaa mashindano hayo.
“Serikali imelipa taarifa Shirikisho la Soka Ivory Coast kuhusu kujiondoa kama mwenyeji wa AFCON U20. Rais anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa kila mtu kwa kujitolea kwake,” imesema taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Ivory Coast (FIF).
Kwa mujibu wa ibara ya 77 ya kanuni za mashindano hayo, nchi mwenyeji ikijitoa kwa muda usiozidi miezi sita, inatozwa faini ya Dola 250,000 (Sh665 milioni).
Kitendo cha Ivory Coast kujitoa kunamaanisha kuwa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ inalazimika kusubiri uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wa wapi mashindano hayo yatafanyika.
Ngorongoro Heroes ni miongoni mwa timu 13 zitakazoshiriki mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili.