Ngoma nzito viti maalumu CCM

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuripotiwa sintofahamu kwenye mchakato wa kuwapata wabunge na madiwani wa viti maalumu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kumeibuka mjadala mpya kuhusu ukomo wa viti hivyo.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Sophia Simba ameibuka akisema ifike mahali uwepo ukomo wa viti maalumu ili wengine wakalie nafasi hizo.

Awali, ilidaiwa jumuiya za chama hicho (Umoja wa Vijana-UVCCM) na Wazazi nazo zinataka kupata nafasi sawa za uwakilishi bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani kama ilivyo kwa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT).

Kutokana na uwepo wa taarifa hizo, inaelezwa huenda nafasi za uwakilishi kupitia UWT bungeni zitapungua ili kutoa nafasi kwa wawakilishi kutoka Wazazi na UVCCM.

Kwa sasa CCM ina wabunge wa viti maalumu 94 waliotokana na makundi mbalimbali kupitia uwakilishi UWT na Vijana.

Hata hivyo, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akizungumza na Mwananchi Februari 21, 2025 alisema nafasi ya viti maalumu ni mali ya chama cha siasa na kuwa watalifanyia kazi.

Makalla aliyetembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam alisema:

“Viti maalumu ni mali ya chama cha siasa, sasa kwa kuwa CCM ina UWT, basi inapewa dhamana ya kuwapata wabunge wa viti maalumu. Inawezekana mjadala ukawepo kwamba wapo kinamama walioko Jumuiya ya Wazazi, wapo kinadada walioko UVCCM wanasema hii keki yote ya kwetu basi tuongezewe…

“Niseme tunalifanyia kazi, tutakapokaa vikao kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi, CCM itatoa utararibu.

Hata hivyo, Makalla alisema CCM bado inaamini UWT ndiyo yenye jukumu la kuratibu kwa kina mchakato huo, huku akiweka wazi kuwa suala la mgawanyo sawa kwenye nafasi hizo halitakuwepo.

Hoja ya ukomo

Simba akizungumza leo Ijumaa Februari 28, 2025 katika maadhimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo) jijini Dar es Salaam sambamba na kuadhimisha miaka 30 ya Beijing, amesema UWT katika mikutano yake ilishapitisha viti maalumu viwe na ukomo wa miaka 10 lakini utekelezaji umekuwa mgumu.

“Imefika mahali watu wakishatimiza miaka 10 tunaangaliana sura, yule naye tumwambie aende jimboni, ataweza kwenda jimboni kweli? Tumuache aende, kwa nini asiweze kwani hilo la miaka 10 tulishalijadili ndani ya CCM na lipo kwenye makabrasha yetu,” amesema Simba aliyewahi pia kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM.

Amesema lengo la uwepo wa viti maalumu ni kuwawezesha wanawake kupata nguvu, ujuzi na pengine hata pesa za kwenda kugombea majimboni.

“Kwa hiyo, natarajia kwa mwaka huu kina mama wengi ambao wameshahudumu kwa zaidi ya miaka 10, wawaachie vijana sababu zile nafasi ni za kuwawezesha.

“Kama umeshakaa bungeni mpaka miaka 20 kwenye viti maalumu bado unashindwa kuingia kwenye jimbo, basi hauwezesheki na umeshindwa kujiwezesha. Kukataa kuondoka ni kama choyo,” amesema.

Ametoa mfano wa Zakhia Meghji na Anna Abdallah akisema ilifika mahali waliachana na viti maalumu wakaenda kugombea majimboni.

Amesema kwa upande wa Zanzibar, Tereza Omar na Asha Simba walikuwa mashujaa wa kuomba uwepo wa viti maalumu, lakini ilifika mahali mahali wakaondoka.

Ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kuwania majimboni ili idadi ya wanawake bungeni iwe kubwa, akiwashauri vijana kuanza siasa wakiwa wadogo badala ya kusubiri kuteuliwa.

Kufuatia hoja hiyo, Mwanasiasa mkongwe na mbunge za zamani CCM, Kate Kamba akizungumza na Mwananchi amesema lengo la kuanzishwa viti maalumu lilikuwa kama shule ya mafunzo ya siasa kwa wanawake kabla hawajiangia kwenye mchakato wa kuwania majimbo.

Kamba ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, amesema shule hiyo inapaswa kuwa na muda maalumu ili kutoa nafasi kwa wanawake wengine kujifunza na kuwa na ushiriki mkubwa katika siasa na uongozi.

“Watu wanapaswa kujua mambo ya siasa ni magumu, lazima uwe imara, ukubali kuna kushinda na kushindwa, usihofie wala kuweka kinyongo ukipata matokeo usiyoyataka.

“Ni vyema ukawepo muda maalumu, vikao vya chama ndivyo vinaweza kuamua muda gani unatosha kwa mtu kuwa kwenye viti maalumu kabla ya kutoka kwenda kupambania jimbo na kuruhusu wengine waingie kujifunza,” amesema Kate ambaye ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa mbunge.

Kwa upande wake, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Husna Sekiboko amesema hakuna shida kuweka ukomo ubunge wa viti maalumu kwani ni sawa na chuo cha mafunzo.

Sekiboko amesema kikubwa ni kutazama muda gani ambao wanawake wanatakiwa kuwa majimboni kutokana na mahitaji.

“Kama tunataka kutoa fursa kwa wanawake wengi, basi tuweke miaka mitano ili wanawake wengi zaidi wapate nafasi, lakini kama ni kuwajengea uwezo wanawake ili wahitimu, naamini vipindi viwili (miaka 10) vinaweza kututosha kisha tukapambane huko,” amesema.

Amesema kama Taifa linataka kupata viongozi wazuri ipo haja kuwaandaa kuanzia vijana, hivyo miaka 10 inawatosha kuwapata wanawake wazuri na wenye uwezo.

Amesema viti maalumu si fursa, akishauri wanawake wengine wasifikirie hivyo, badala yake washindane, ingawa anakiri wenye nguvu bado ni wachache, wengi bado wana hofu kwenye majukwaa, hivyo anashauri wasiwekewe ukomo bali wajengewe uwezo.

Mmoja wa wabunge wa viti maalumu ambaye hakutaka kutajwa jina, pia amesema nafasi za viti maalumu zinapaswa kuwekewa utaratibu wa ukomo ili kusaidia wasichana kupata ujuzi kwenye nafasi hizo.

“Si kwa upande wa viti maalumu tu hata majimboni kuna watu wako jimboni kwa zaidi ya miaka 20 wanataka kushindana na wale waliotoka vyuoni. Hapa kushinda kwa yule anayeanza inakuwa ni vigumu kwa kuwa kampeni zinahitaji fedha,” amesema.

Kuhusu Ulingo

Akizungumzia kuhusu miaka 15 ya Ulingo na miaka 30 ya Beijing, Sophia Simba amesema kuna mabadiliko makubwa yametokea, ikiwemo kuongezeka kwa nafasi za uteuzi za wanawake, viongozi wa kuchaguliwa na kuwepo kwa mwamko wa wanawake kuingia kwenye siasa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Awali, mratibu wa Ulingo, Dk Ave-Maria Semakafu amesema katika miaka 15 moja ya mambo wanayojivunia ni kuibua taswira ya mwanamke katika ngazi ya uamuzi na michakato ya kidemokrasia.

Amesema walipoanzisha umoja huo ilikuwa ngumu, ikizingatiwa kuliibuka kelele za mafisadi lakini walihakikisha wanasimama imara kufanikisha hilo.

Dk Semakafu amesema katika harakati hizo mwaka 2015 walikuwa waangalizi wa uchaguzi wakaibua namna wanawake wanavyonyanyasika kwenye harakati za uchaguzi.

“Kubwa tunalolikumbuka ni katika kutaka 50 kwa 50 katika Bunge la Katiba, ikiwemo mwenyekiti akiwa mwanaume basi makamu awe mwanamke na tunafurahi aliyekuwa makamu wa Bunge hilo wakati huo, ndiye Rais wa nchi hii leo, ambaye ni Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Amesema wameweza kuwaunganisha wanawake wa itikadi mbalimbali.

Mjumbe wa Ulingo Zanzibar na mkurugenzi wa Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Sitti Abbas Ali amewasihi wasichana kujitokeza kuchukua fomu kugombea kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Mwenyekiti wa Shirika la Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu (Sawuta), Stela Jairosi amesema Ulingo imewasaidia kuwapa elimu na kuwezesha kupata wabunge watano wenye ulemavu na madiwani 13 hadi sasa.

Akimwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Msajili Msadizi, Hollo Kazi amesema kwa kuwa vyama vipo katika uandaaji sera ya jinsia ni vyema wakatumia nafasi hiyo kuweka mambo yanayowahusu wanawake.

Imeandikwa na Nasra Abdallah, Elizabeth Edward, Habel Chidawali na Sharon Sauwa