Neymar nje tena kwa jeraha

Nyota wa Brazili anayekipiga Ligi Kuu nchini Saudi Arabia maarufu kama ‘Saudi Pro League’ Neymar jr imeripotiwa amepata tena jeraha hapo jana kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Barani Asia kati ya Al Hilal dhidi ya Esteghal.

Neymar aliingia uwanjani dakika ya 58 akitokea benchi ikiwa ni mchezo wake wa pili baada ya ule wa Al-Ain tangu apone majeraha ambayo yaliyomweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.

Dakika ya 87, alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kupata maumivu ya msuli wa paja wakati aliposhindwa kupokea pasi na kuanguka chini akionekana kuwa na maumivu makali huku akishikilia mguu wake.

Neymar alijiunga na Al Hilal akitokea PSG ya Ufaransa kwa dau la paundi 75 milioni huku akiwa amecheza mechi saba na kufunga bao moja.

Kwenye mchezo wa jana, Al Hilal walipata ushindi wa mabao 3-0 wakiichapa Klabu ya Esteghal ya Iran kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Asia ambapo mabao yote yalifungwa na Aleksandr Mitrovic.

Neymar amekuwa na majeraha ya mara kwa mara akiwa amezitumikia timu kadhaa kubwa duniani ikiwemo Barcelona na PSG ya Ufaransa.