Neymar avunjiwa mkataba Saudia

Riyadh, Saudia Arabia. Staa raia wa Brazil Neymar amezifikisha mwisho zama zake kwenye soka la Saudi Arabia baada ya mkataba wake Al Hilal kusitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.

Mshambuliaji huyo  alihamia kwenye Saudi Pro League akitokea Paris Saint-Germain mwaka 2023 na alisaini mkataba aliokuwa akilipwa Pauni 2.5 milioni kwa wiki katika klabu hiyo ya Al Hilal.

Hata hivyo, Mbrazili huyo amekuwa akiandamwa na majeraha mengi, ikiwamo tatizo la goti lililomfanya awe nje kwa msimu mzima wa 2023-24.

Neymar, 32, amefunga bao moja na asisti tatu katika mechi saba alizocheza kwa kipindi cha miaka miwili huko Kingdom Arena. Jambo hilo limemfanya staa huyo wa zamani wa Barcelona kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake Al Hilal, ambayo ilitangaza kuachana naye.

Al Hilal ilitangaza hivi: “Al Hilal na Neymar wamekubaliana kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande mbili. Klabu inamshukuru sana Neymar kwa kile alichokifanya kwa kipindi chake alichokuwa Al Hilal na tunamtakia mafanikio mema kwenye maisha yake ya mpira.”

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, Neymar atarudi zake Santos timu aliyoanzia soka.

Fowadi huyo mwenye uwezo wa kucheza namba tofauti kwenye safu ya ushambuliaji aliibukia kwenye klabu hiyo ya Brazil, ambapo amefunga mabao 136 na asisti 64 katika mechi 225. Alihamia Barcelona mwaka 2013, ambako alifunga mabao 105 na asisti 76 katika mechi 186 alizocheza kwa kipindi cha miaka minne kwenye timu hiyo na kushinda La Liga mara mbili, Copa del Rey mara tatu na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja