Neymar aanza na sare Santos

São Paulo, Brazil. Staa wa Brazil Neymar, jana alicheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya nchi hiyo akiwa na Santos na kuisaidia timu yake kupata sare ya bao 1-1kwenye mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Albano Caldeira.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza tangu Neymar ajiunge Santos ambayo ni timu yake ya utotoni ikiwa ni mara ya kwanza anarudi kwenye timu hiyo baada ya kupita miaka 12.

Staa huyo mwenye miaka 33, alitambulishwa kwenye timu hiyo baada ya kuvunjiwa mkataba uliokuwa na thamani ya pauni 130 milioni kwa mwaka na klabu yake ya Al-Hilal inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

Neymar anayeongoza kwa kufunga mabao kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Brazil alianza kuichezea Santos mwaka 2009, ambapo alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Copa Libertadores mwaka 2011, baada ya kufunga bao muhimu kwenye mchezo wa mwisho.

Katika kipindi chake cha miaka minne kwenye timu hiyo alifanikiwa kucheza michezo 225 kwenye mashindano yote na kufunga mabao 136 huku akitoa pasi 64 za mabao.

Pamoja na kwamba alisumbuliwa na majeraha akiwa Saudi Arabia, Neymar aliingia akitokea kwenye benchi kwenye sare hiyo ya bao 1-1 dhidi ya Botafogo, hata hivyo aliumia dakika mbili tu tangu alipoingia uwanjani baada ya kujigonga na mpira kwenye nyonga lakini akaendelea kucheza.

“Naipenda Santos,’ alisema Neymar. “Sina neno lingine ambalo naweza kulitumia kusema haya, ninafuraha sana kuona usiku huu nimepata tena nafasi ya kuichezea timu hii.

“Bado nahitaji muda wa kucheza. Sipo fiti kwa asilimia 100, sikuwa nataka kukimbia wala kukokota mpira kwa muda mrefu, nafikiri nitakuwa fiti zaidi baada ya michezo minne au mitano.”

Mara baada ya kuondoka Santos, Neymar alijiunga na Barcelona na baadaye akaondoka na kwenda PSG kwa usajili uliovunja rekodi.

Hata hivyo, anatakiwa kuhakikisha anafanya kazi ya ziada kwenye timu hiyo ambayo msimu uliopita ilikuwa kwenye hatihati ya kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2023.

Akiwa na Santos ambayo sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi Kundi B ikiwa na pointi 8 baada ya kucheza michezo saba, Neymar amechukua jezi namba 10 ambayo ilitumiwa na gwiji wa zamani wa Brazil na Santos, Pele.