Newcastle waambiwa Isak asiuzwe kokote

Mabosi wa Newcastle United wameambiwa wagomee ofa yoyote inayomhusu straika Alexander Isak dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi Ulaya.

Fowadi huyo wa kimataifa wa Sweden amethibitisha kuwa silaha imara ya klabu hiyo baada ya kufunga mabao 23 msimu huu, ikiwamo bao la pili muhimu kwenye fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Liverpool, Jumapili iliyopita.

Sasa Mwenyekiti wa Newcastle, Yasir Al-Rumayyan amewaambia watendaji wengine wa klabu hiyo watafanya kila wanaloweza kuhakikisha wataendelea kubaki na wachezaji wao muhimu wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa mastaa.

Al-Rumayyan alisema anauhakika Isak atabaki kwenye timu hiyo huku wamiliki wa klabu Saudi Arabia’ Public Investment Fund ikiwa haina wasiwasi wowote kutokana na kuwa na mkwanja wa kutosha. Gavana wa PIF alikuwapo uwanjani Wembley, Jumapili iliyopita na kumshuhudia Isak akifunga bao muhimu lililoihakikishia timu hiyo inanyakua taji msimu huu.

Newcastle inafahamu wazi itakuwa kwenye presha kubwa ya kubaki na mchezaji huyo wakati dirisha lijalo la usajili litakapofunguliwa kutokana na Barcelona kuwa miongoni mwa timu zinazomtaka fowadi huyo na ilituma skauti wake wakamtazame kwenye mechi ya West Ham United.

Isak amekuwa akihusishwa sana na mpango wa kuachana na timu hiyo na bado hakuna ishu ya kuongezewa mkataba.

Kuna timu kibao zinamfukuzia mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Sociedad, ikiwa ni pamoja na Arsenal na Liverpool, huku mkataba wake kwenye kikosi hicho cha St James’ Park utafika tamati 2028.

Mazungumzo ya mkataba mpya yataanza mwishoni mwa msimu huu, kutokana na sasa miamba hiyo inapambana kuhakikisha inakamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Ushindi wa Kombe la Ligi imewapa tiketi ya kucheza Europa Conference League.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *