London, England. Baada ya kuiondoa Tottenham Hotspur katika nusu fainali ya Kombe la Carabao sasa Liverpool itavaana na Newcastle katika fainali itakayochezwa Machi 16, 2025 kwenye uwanja wa Wembley.
Katika mchezo wa jana Liverpool ilipata ushindi wa mabao 4-0 ambao uliihakikishia kutinga fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 kwani katika mchezo wa kwanza Tottenham ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani.

Mabao ya Liverpool yalifungwa na Cody Gakpo ambaye aliunganisha pasi iliyopigwa na Mohamed Salah katika dakika ya 34 kisha Salah kufunga lingine kwa mkwaju wa penati dakika ya 51.
Dakika ya 75, Dominik Szoboszlai aliifungia Liverpool bao la tatu akipokea pasi ya Conor Bradley huku bao la nne likifungwa na beki, Virgil van Dijk ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Alexis Mac Allister.

Pasi ya bao aliyotoa Mohamed Salah kwa Cody Gakpo ilikuwa ya kwanza kwenye mashindano ya Carabao tangu alipofanya hivyo 2014 ambapo alimpasia Didier Drogba wakati alipokuwa Chelsea kwenye mchezo dhidi ya Shrewsbury Town.
Bao la penati lililofungwa na Mohamed Salah linamfanya kufikisha jumla ya mabao nane ambayo amefunga kwa mikwaju ya penati katika mashindano yote msimu huu huku Steven Gerrard akiwa anashikilia rekodi hiyo kwa England kwa kufunga mabao 11 ya penati msimu wa 2013-2014.
Bao alilofunga Virgil van Dijk linamfanya kuwa beki mwenye mabao mengi katika mashindano yote ya England akiwa amefikisha jumla ya mabao 26.

Liverpool inatinga fainali ya Kombe la Carabao kwa mara ya 15 ikiwa ni mara nyingi zaidi ya Klabu nyingine ya England huku ikiwa na rekodi ya kutwaa mataji 10 ikishika nafasi ya kwanza.
“Ni muhimu kwenda fainali, naelewa jinsi gani uwanja wa Wembley ulivyo wa kipekee, lakini tunatambua mchezo utakuwa mgumu kwani Newcastle ni timu yenye kiwango cha juu.
“Tumejitahidi sana kuboresha timu, wachezaji wanajitahidi sana kujiboresha, lakini tunahitaji kushinda mataji, natumaini tutafanya hivyo,” amesema Arne Slot meneja wa Livepool.