Kufuatia uamuzi wa Netflix wa kutoonyesha tena filamu zake zenye anuani ya “Hadithi za Palestina”, kufuatia mashinikizo ya Wazayuni, shirika hilo utiririshaji limekosolewa kimataifa.
Ingawa Netflix, yenye makao yake makuu ya California inadai kuwa uamuzi huo ulikuwa sehemu ya “sera za kawaida kuhusiana na leseni,” wanaharakati wanaounga mkono Palestina bado hawajashawishika na wamejiunga na vuguvugu linalokua la kutaka shirika hilo libatilishe uamuzi huo wa kufuta filamu kuhusiana na Palestina.
Wanaharakati wanasema kuondolewa kwa uchache filamu 24 kuhusu maisha ya Wapalestina katika huduma ya utiririshaji ya Netflix ni sawa na kufuta uwakilishi wa Wapalestina kwenye jukwaa hilo.
Idadi kubwa ya watumiaji wa Netflix wameacha kutumia huduma hiyo kuonyesha mshikamano na Wapalestina wakati wa vita vya mauaji ya kimbari ambavyo vinaendelezwa na utawala katili wa Israel kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Wanaamini kuwa kulipia huduma za Netflix ni sawa na kusaidia kifedha “kufutwa Palestina.”

Watumiaji wengi wa zamani wa Netflix wanasema jukwaa linaendeleza dhana mbaya, kukuza simulizi zenye upendeleo na kuchangia kutengwa Wapalestina ambao tayari wanakandamizwa.
Shirika la Netflix sasa linatuhumiwa kwa kuhusika katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa kwa pamoja na Israel na Marekani huko Gaza.
Barua ya kutaka kurejeshwa filamu hizo imeandikwa na mashirika 30 yanayounga mkono Palestina, ikiwa ni pamoja na Freedom Forward.