Netanyahu aishukuru Marekani kwa kuisaidia kikamilifu Israel katika jinai zake

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ameishukuru Marekani kwa kuiunga mkono Israel katika jinai zake kwenye maeneo tofauti ya Asia Magharibi. Vile vile amekiri kuwa Israel inaendelea kupata hasara kubwa katika vita vinavyoendelea baina yake na Kambi ya Muqawama wa Kiislamu.

Benjamin Netanyahu amesema hayo baada ya walowezi 6 wa Kizayuni kuangamizwa na wengine 50 kujeruhiwa wengi wao wakiwa ni askari wa utawala wa Kizayuni bada ya lori moja kuvamia eneo moja lililoko karibu na kambi ya shirika la kijasusi la Israel Mossad mjini Tel Aviv. 

Televisheni ya al Alam imeripoti habari hiyo na kumnukuu Netanyahu akisema jana kwamba, anaishukuru Marekani kwa msaada wake mkubwa katika mashambulizi yanayofanywa na Israel tangu tarehe 7 Okbota 2023 na mauaji yake ya umati na ukatili wa kuchukupa mpaka unaofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza, Palestina.

Silaha za Marekani ndizo zinazotumika kufanya jinai za kutisha huko Palestina hasa Ghaza na hivi sasa Netanyahu anaishukuru Marekani kwa kushiriki kikamilifu kwenye jinai hizo

Jinai hizo za Israel ambazo hivi sasa Netanyahu anaishukuru Marekani kwa kushiriki kikamilifu ndani yake, zimeshapelekea zaidi ya Wapalestina laki moja na 43,500 kuuawa shahidi na kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. Zaidi ya Wapalestina 10,000 hawajulikani walipo na kuna uwezekano mkubwa nao wameuawa. Uharibifu uliofanywa na Israel katika maeneo ya Palestina na Lebanon hauna mfano na haujawahi kushuhudiwa katika historia ya zama hizi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba dereva wa lori aliyewavamia Wazayuni hao kwenye kituo cha basi ni mkazi wa mji wa Kiarabu wa Qalansawe na kuongeza kuwa devera huyo alitoka kwenye lori baada ya kugonga basi akiwa na kisu mikononi mwake. Duru nyingine za habari za utawala wa Kizayuni zimetangaza kuwa, wote waliojeruhiwa ni askari wa kikosi cha 8200 cha Glilot cha utawala wa Kizayuni.

Glilot iko karibu na eneo la Herzliya lenye makao makuu ya Shirika la Kijasusi la Israel Mossad pamoja na vitengo kadhaa vya kijasusi vya jeshi la utawala wa Kizayuni.