NEMC yataja sababu ugumu kudhibiti mifuko ya plastiki

Dodoma. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa udhibiti wa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini, ni kutokana na ukosefu wa mamlaka kamili ya kisheria.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya baraza hilo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, jijini Dodoma, leo Machi 24, 2025.

Dk Semesi amesema changamoto inayozuia ufanisi wa utendaji wa NEMC ni kutokuwa na mamlaka kamili katika udhibiti wa mazingira.

Hali hiyo imefanya utekelezaji wa sheria na taratibu kuingiliana na mamlaka nyingine, hasa katika suala la udhibiti wa mifuko ya plastiki.

“Ni imani yetu kuwa NEMC ikiwa na mamlaka kamili, itakuwa na uwezo wa kusimamia vyema utunzaji wa mazingira, na hivyo kudhibiti matumizi holela ya mifuko ya plastiki, uharibifu wa milima, uchafuzi wa vyanzo vya maji, pamoja na utiririshaji wa kemikali migodini na viwandani,” amesema Dk Semesi.

Katika kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki, NEMC imekuwa ikiendesha shughuli kwa kushirikiana na taasisi 14, ambazo zote zina lengo moja.

Hata hivyo, Dk Semesi amesema  NEMC imekuwa ikitwishwa mzigo mkubwa wa kufanya utekelezaji wa marufuku hiyo peke yake, ilhali taasisi nyingine kama vile Wizara ya Viwanda na Biashara, Idara ya Uhamiaji, na mamlaka za serikali za mitaa pia zina jukumu hilo.

Matumizi ya mifuko ya plastiki yalipigwa marufuku na Serikali mwaka 2019 kutokana na madhara kutokana na mifuko hiyo kuwa na madhara katika mazingira.

Dk Semesi amesema licha ya juhudi za NEMC, bado kuna upungufu wa wataalamu elekezi katika sekta na ulinzi wa mazingira, jambo linalokwamisha juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mifuko ya plastiki.

Amesema NEMC inaendelea kufanya tafiti kuhusu mifuko mbadala ya non-woven, ambayo inatajwa kuwa ni suluhisho la mazingira, ili kujua kama ina uwezo wa kuoza haraka, tofauti na ya plastiki inayochukua miongo kadhaa kuoza.

Gugumaji Ziwa Victoria

Katika hatua nyingine Dk Semesi ameeleza kuhusu uvamizi wa aina mpya ya gugumaji katika Ziwa Victoria, ambalo limeathiri hali ya mazingira ziwani humo.

Amesema kuwa magugu hayo yanaenea  kwa kasi na yana madhara makubwa yakiwemo kuziba injini za vivuko, kuathiri miundombinu ya uvuvi, na kuchafua mazingira ya ziwa.

“Gugumaji hili limeathiri vivuko na vizimba vya samaki, na hali hiyo inasababisha athari kubwa kwa uchumi wa eneo hilo. Tunasimamia mikakati ya haraka ili kupunguza madhara hayo,” amesema Dk Semesi.

Amesema udhibiti wake unaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, pamoja na wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria.

Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano wa taasisi 12 na mamlaka za bonde ili kuhakikisha athari za gugumaji hilo zinapungua.

Dk Semesi amesema kuwa hatua za haraka zinazochukuliwa ni pamoja na kuvuna gugumaji hili kwa kushirikiana na wavuvi, ili kurejesha hali ya usafi katika ziwa hilo.

 “NEMC inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wavuvi, wataalamu wa mazingira na mamlaka za Serikali ili kuhakikisha Ziwa Victoria linakuwa salama na endelevu kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *