
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa tahadhari za kimazingira na namna watu wanavyoweza kuepuka mafuriko, maporomoko ya udongo kufuatia mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha katika msimu ujao kama ilivyotangazwa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Miongoni mwa tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa ni kupambana na watu wanaotupa taka ngumu katika mifumo ya maji ili kuzua athari za mafuriko zinazoweza kutokea, pindi mvua zitakapoanza kunyesha.
Msingi wa kauli ya NEMC ni kutokana na kilichoelezwa na TMA, Januari 23 mwaka huu, ambapo ilitabiri uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Pia mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza na ikitarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mbali na rai hiyo, pia NEMC imetangaza kuwa Februari mwaka huu inatarajiwa kuzindua mfumo utakaokuwa ukiratibu ukusanyaji taka ili waweze kujua kila wilaya inazikusanya kiasi gani, huku wakihamasisha kuzitenga kutokana mahali zinapozalishwa.
Akizungumza na wanahabari, leo Februari 2, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi amesema ni wakati sasa wa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama ili kuepusha mafuriko na mlipuko wa magonjwa ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada za katika ujenzi wa Taifa.
“NEMC tunawatahadharisha wananchi kujiepusha kwa namna yoyote ile na vitendo vyenye kuchangia uharibifu wa mazingira. Pia mamlaka za Serikali za serikali za mitaa hususan jijini Dar es Salaam zianze kuchukua hatua stahiki kupambana na watu wanaotupa taka ngumu katika mifumo ya maji ambapo ikiziba athari zake ni kutokea mafuriko,” amesema.
Ili kuepukana na hali hiyo pia amewataka wananchi kuchukua tahadhari za kuepuka maeneo ya fukwe za bahari ikiwa ni pamoja na miamba ya maziwa na mito ili kujinusuru na mafuriko na athari zake.
Pia rai imetolewa kwa wale wanaoishi kwenye maeneo ya kandokando ya milima au miinuko mikali kuchukua tahadhari ili kuepukana na athari za maporomoko ya ardhi.
“Tunaziomba Mamlaka za Serikali kufuatilia kwa karibu maeneo ya uchimbaji madini na vifusi ili kuhakikisha jamii husika inakuwa salama na majanga yanayoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na udhibiti wa taka ngumu ili zisizagae na kuingia kwenye mifereji ya maji ya mvua na mifumo ya majitaka na kuziba,” amesema
Haya yanasemwa wakati ambao miaka ya hivi karibuni, mataifa kadhaa yamekumbwa na majanga mbalimbali yanayosababishwa na athari za shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Athari hizo ni kuongezeka kwa joto, ukame, mafuriko na maporomoko ya ardhi. Upande wa Tanzania maeneo yaliyopatwa na athari hizo ni Katesh, Wilaya Hanang Mkoa wa Manyara, Kawetere Wilaya ya Mbeya Mkoa wa Mbeya, Mamba Miamba katika Wilaya Same Mkoa wa Kilimanjaro.
Kuhusu mfumo
Dk Semesi amesema mfumo utakaozinduliwa baadaye mwezi huu utaanza kufanya kazi ili kujua ni taka kiasi gani zinazalishwa na zipi zinaweza kutumika kuzalisha umeme, gesi ya kupikia au vifaa vingine kupitua urejeleshwaji
Ili kufanikisha hilo watahakikisha kunakuwapo miundombinu ya kuzitenganisha na kuzikusanya huku wakihamasisha wajasiriamali wengine kutumia taka kutengeneza bidhaa.
Amesema mfumo huo unaanza kazi wakati ambao hakuna takwimu sahihi za uzalishaji taka badala yake zinakadiriwa.
“Mfano tu jiji la Dar es Salaam, sehemu pekee ambayo taka kukusanywa ni Pugu lakini jiji ni kubwa kiasi gani kwa kuangalia makazi na shughuli za uzalishaji zilizopo. Ukilinganisha na taka zinazozalishwa majumbani au maeneo mbalimbali ya uzalishaji haziendani na zinazofika Pugu,” amesema.
Amesema ingekuwa taka zote zinazozalishwa jijini Dar es Salaam zinapelekwa dampo la Pugu basi kungekuwa na mlima mkubwa, huku akisema miundombinu iliyopo haionyeshi kama taka zote zinazokusanywa ndiyo zinafika Pugu.
“Dar es Salaam ni mji wa biashara maana yake uzalishaji taka ni mkubwa, haiwezekani mkazi wa Bunju taka zake zipelekwe Pugu huwa zinaisha hapa katikati kwani zinazofika Pungu ni wastani wa tani 400,000 kwa mwezi, lakini hii haikusanyi taka zote zinazozalishwa jijini,” amesema.