Ndumbaro atangaza kiama watumishi wanaosababisha migogoro ya ardhi

Arusha. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ametangaza kiama kwa watumishi wa umma wanaosababisha migogoro mbalimbali nchini, ambayo inawanyima wananchi kupata haki zao.

Amewaelekeza wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwasilisha mapendekezo ya suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi nchini pamoja na ukuaji wa miji kiholela.

Waziri huyo ameyasema hayo leo Jumanne Machi 4, 2025, alipokuwa akizungumza katika wiki ya wanawake, kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8, 2025 ambayo kitaifa mwaka huu yatafanyika Arusha.

Amesema ameagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kushughulikia migogoro ya wananchi ambapo kuna timu ya wanasheria zaidi ya 50 watakaoshirikiana na wizara nyingine watatatua kero za wananchi.

“Rais Samia ameagiza mtumishi yoyote wa umma ambaye ndiye chanzo cha migogoro hii nihangaike naye, kwa hiyo ewe mtumishi wa umma ambaye ndiye umekuwa chanzo cha kuwadhulumu wananchi, 40 zako zimefika.

“Rais Samia ameandaa dawa ya kwako imechemka, imeiva nimekuja kukunywesha. Tutahakikisha kila Mtanzania na mwanaArusha anapata haki yake, nimezunguka kwenye mabanda yote kujionea huduma za kisheria na mimi nimeandaliwa dawati nikae niwasikilize na nitafanya hivyo kwa siku tatu,” amesema.

Dk Ndumbaro amesema lengo la kampeni maalumu ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid ni kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria kwa haki, usawa amani na maendeleo na kuwa jamii ikishapata haki itakuwa na usawa kwani kutakuwa hakuna anayemuona au kumdhulumu mwingine.

“Lakini wataalamu wa sheria wanasema haki inapokelewa kwenye mikono safi, kama mikono yako ni michafu huwezi kupokea haki, usije ukadhulumu halafu ukaja ukasema unataka haki, lazima uwe umetenda haki ndipo uidai,” ameongeza.

Waziri huyo amesema katika utatuzi wa kero hizo zipo zinazoisha na ambazo wananchi watapewa wataalamu wa kisheria ili waendelee kuwasimamia.

Kuhusu wataalamu wa ardhi, amesema wakati kampeni hiyo inaendelea, moja ya changamoto kubwa iliyojitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini ni migogoro ya ardhi na kuwataka wataalamu hao kuandaa mkakati wa kisera ambao utakuwa suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Urasimishaji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nicholaus Mwakasege amesema migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na mazingira mbalimbali ikiwemo wananchi kutozingatia taratibu za ununuzi, uendelezaji na uvamizi wa ardhi.

“Mbali na kutoa huduma hapa, sisi kama wizara tumekuwa na kliniki zetu endelevu zinazofanyika kila mkoa na tumekuwa tukiwaelimisha wananchi mambo muhimu ya kuzingatia wanapotaka kununua ardhi.”

“Wananchi wanapotaka kununua ardhi wafike ofisi za ardhi ili wapewe taarifa kuhusu eneo husika, mfano hapa Arusha tuna mpango wa matumizi bora ya ardhi, hivyo muhimu mwananchi kujua asije kununua eneo kwa ajili ya makazi kumbe limetengwa kwa ajili ya kiwanda,” amesema.