
KIPA wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Said Mohammed ‘Nduda’ ameikumbushia Dabi ya Kariakoo aliyosimama langoni na kufungwa mabao manne wakati Yanga ikifa 5-0 mbele ya Simba katika pambano lililopigwa Mei 6, 2012, akisema limebaki kichwani mwa watu kutokana na kipigo hicho.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kufungia msimu wa 2011-2012, Nduda alimpokea kipa Yew Berko aliyetanguliwa kufungwa bao moja lililowekwa kimiani na Emmanuel Okwi katika dakika ya kwanza tu, kabla ya kumpisha yeye kipindi cha pili na kutunguliwa mabao manne yalioingia katika rekodi kwake.
Nduda aliyewahi kukipiga pia Mtibwa Sugar, alifungwa mabao hayo na Okwi pamoja na penalti tatu zilizopigwa na Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Felix Sunzu na kuiacha Yanga ikilala 5-0 kabla ya mwaka juzi kulipa kisasi kwa kuifumua Simba mabao 5-1 mechi iliyopigwa Novemba 23, 2023.
Nduda alisema kipigo hicho ni rekodi ambayo inapaswa kutumiwa na mastaa waliopo Simba na Yanga kuangalia namna wanavyozitumikia timu hizo watengeneze rekodi za aina gani watakazowaachia kumbukumbu nzuri za kuwapa heshima, kutokana na mechi za dabi ya Kariakoo kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na jamii.
Alisema mchezaji wa timu hizo mbili zinazogusa sehemu kubwa ya Watanzania ni lazima wafanye mambo yatakayowafanya waendelee kuimbwa kwa heshima na sio rekodi mbaya ambazo wakati mwingine humnyima mtu raha, kama ilivyo kwake kila mara kukumbukwa kama mmoja wa makipa waliofungwa mabao mengi katika dabi ya Kariakoo.
“Nilidaka mechi moja tu ya dabi nikiwa Yanga, lakini ni mechi hiyo hiyo ilinifanya niingie katika rekodi mbaya na haiepukiki kunitaja, ingawa dabi ina mambo mengi hivyo huwezi kujitetea kwa namna yoyote ile, lakini wapo wengine walioichezea Dabi na kuacha rekodi ya heshima kama mtu pekee kufunga hat trick ya kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni aliyoiweka kabla Nduda hatujazaliwa lakini inatajwa hadi sasa,” alisema Ndunda na kuongeza;
“Ukicheza Simba na Yanga utaondoka na vitu viwili heshima ama aibu ndio maana mastaa waliopo wanapaswa kuitumia vyema fursa hiyo, ili wanapoenda timu nyingine wabakie kusimuliwa kwa kufanya makubwa, kwani rekodi zinazohusu Dabi ya Kariakoo hazifutiki kirahisi.”
Kipa huyo aliyeanza kuwika na Majimaji Songea kabla ya kutua Yanga na baadae kwenda Mtibwa na Ndanda na kudakwa na Simba, mara ya mwisho kuonekana uwanjani alikuwa na Ihefu (sasa Singida BS), amebaki kujihusisha na mambo ya kifamilia, japo amesema anatarajia kurejea uwanjani msimu ujao licha ya kuwa na umri wa miaka 35 kwa sasa.
Nduda amekumbushia Dabi hiyo ya 2012 ikiwa ni siku chache tangu kushindwa kufanyika kwa mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara msimu huu baina ya vigogo hao kutokana na Bodi ya Ligi kutangaza kuiahirisha saa chache baada ya Simba kudai isingeenda uwanjani kwa sababu ya kuzuiwa na makomandoo wa Yanga kufanya mazoezi ya mwisho kulingana na kanuni za ligi.
Mechi hiyo bado haijapangiwa tarehe mpya, huku Yanga ikichimba mkwara kwa kuiandikia barua Bodi juu ya kutocheza tena mchezo huo, kwani uliahirishwa bila kuzingatiwa kanuni.