
Dua za Kylian Mbappe zimetimia baada ya leo Real Madrid kupangwa kukutana na Atletico Madrid katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kabla ya droo ya kupanga hatua ya 16 bora, Mbappe alinukuliwa akitamani Real Madrid ikutane na mahasimu wao wa jadi, Atletico Madrid ili wasisafiri sana.
“Kiukweli ni bora tupangwe dhidi ya Atletico (Madrid). Wao na Bayern (Munich) ni timu mbili kubwa na itakuwa ngumu kila upande. Lakini kwa raundi ijayo itakuwa bora sana kwetu kama hatutosafiri sana,” alisema Mbappe.
Na leo droo ya hatua ya 16 bora iliyochezwa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa) imezikutanisha timu hizo zinazotoka katika jiji moja la Madrid huko Hispania jambo ambalo linatimiza hamu ya Mbappe.
Katika droo hiyo iliyofanyika leo kwenye makao makuu ya Uefa, Nyon, Switzerland, Arsenal imepangwa kukutana na PSV, Liverpool dhidi ya PSG, Club Brugge itacheza na Aston Villa, Benfuca dhidi ya Barcelona, Borussia Dortmund na Lille, Bayern Munich dhidi ya Bayer Leverkusen na Feyernoord itavaana na Inter.
Droo hiyo imeonyesha pia njia ambazo timu zitapita katika hatua ya robo fainali na nusu fainali.
Mshindi baina ya PSV na Arsenal atacheza dhidi ya mshindi wa Real Madrid dhidi ya Atletico Madrid.
Timu itakayofuzu baina ya PSG na Liverpool itacheza na mshindi baina ya Club Brugge na Aston Villa.
Timu mbili zitakazopita katika njia hizo zitakutana katika hatua ya nusu fainali.
Mechi nyingine za hatua ya 16 bora zitakuwa ni baina ya Barcelona na Benfica, Dortmund na Lille, Bayern Munich dhidi ya Bayern Leverkusen na Feyenoord dhidi ya Inter Milan.